Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kwenye maisha, watu wanaopata mafanikio huwa wanafanya vitu ambavyo wasiofanikiwa hawapendi kuvifanya. Na hao waliofanikiwa siyo kwamba wanapenda sana kufanya vitu hivyo, bali wanajua lazima wavifanye ndiyo wafanikiwa, hivyo wanavifanya.

Ili mtu aweze kufanya vitu anavyopaswa kufanya, hata kama havipendi, ni lazima aweze kujidhibiti yeye mwenyewe. Kujidhibiti mwenyewe ni kuondokana na yale mambo ambayo yanakukwamisha kupata yale unayokuwa unayataka.

Huwezi kufanya makubwa na kufanikiwa kwenye maisha yako kama unafanya yale tu unayojisikia kufanya. Ni lazima uweze kujisukuma kufanya yale ambayo hujisikii kufanya, lakini ni muhimu yafanyike ili kuzalisha matokeo makubwa.

Ili uwe muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa, ni lazima uweze kujidhibiti wewe mwenyewe. Lazima ufanye yale yote yanayopaswa kufanywa kwenye mchakato wa mauzo ndiyo uweze kupata matokeo mazuri.

KUJIDHIBITI KWENYE MCHAKATO WA MAUZO.

Mchakato wetu mkuu wa mauzo unahusisha hatua sita ambazo kila muuzaji anapaswa kuzifanyia kazi.

Moja ni kuwa na maendeleo binafsi, ambapo mtu anapaswa kujifunza na kuchukua hatua ili kuwa bora zaidi. Ili uwe bora, ni lazima ujidhibiti mwenyewe kwenye kufanya yale yanayopelekea uwe bora.

Mbili ni kusaka wateja wapya tarajiwa, ambapo mtu anawafikia wateja ambao hawakuwa wanaijua biashara. Ili kuwafikia wateja wapya, ni lazima ujidhibiti mwenyewe na kuvuka hofu ya kukataliwa.

Tatu ni ukamilishaji, kugeuza wateja wapya tarajiwa kuwa kamili, ambapo mtu anawashawishi wateja kununua kwa mara ya kwanza. Kujidhibiti mwenyewe kunahitajika sana kwenye ukamilishaji ili kwenda na wateja mpaka wakubali kununua.

Nne ni uhudumiaji, ambapo wateja wanatimiziwa kile ambacho wameahidiwa wakati wanashawishiwa kununua. Ili kutoa huduma bora, mtu lazima aweze kujidhibiti mwenyewe na kufanya yote yanayopaswa kufanyika.

Tano ni ufuatiliaji, ambapo wateja wanafuatiliwa kwa msimamo bila kuachwa, ili wasiisahau biashara na biashara isiwasahau. Kujidhibiti mwenyewe kunahitajika ili ufuatilie wateja hata pale wanapoonekana hawana mwelekeo.

Sita ni kuwa na ushawishi, ambapo mtu anajijengea ushawishi wa kuwafanya watu kukubaliana naye kwenye kile anachowaambia. Ni lazima uweze kujidhibiti mwenyewe ili kutekeleza yale yanayowashawishi wateja kukubaliana na wewe.

Hatua zote sita zinahitaji sana muuzaji uweze kujidhibiti mwenyewe ili ufanye yale yanayopaswa kufanyika bila ya kukata tamaa na kuishia njiani.

Muuzaji anayefanya yale yanayopaswa kufanyika anapata matokeo mazuri. Wakati ambao hawafanyi yanayopaswa kufanyika wanaishia kupata matokeo hafifu.

SOMA; Kuwa Bora Kwenye Majadiliano Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

MADARAJA YA WAUZAJI.

Kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO, wauzaji wamegawanyika kwenye madaraja matano kulingana na ari wanayokuwa nayo katika kutekeleza majukumu yao kimauzo.

Madaraja hayo ndiyo yanayopima mafanikio ambayo mtu anayapata kwenye mauzo. Kujidhibiti mwenyewe kunahitajika sana ili mtu kuweza kuwa kwenye madaraja ya juu na kufanikiwa kwenye mauzo.

Madaraja ya wauzaji ni kama ifuatavyo;

Daraja la Kwanza (Division One); Wale wanaofanya kilicho sahihi bila kuambiwa.

Hawa ni wauzaji ambao wanatekeleza mchakato wao wa mauzo bila ya kusubiri kuambiwa. Wanayajua majukumu yao na wanayafanya vizuri. Hawa ndiyo wanaopata mafanikio makubwa zaidi kwenye mauzo na kuwa wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea.

Daraja la Pili (Division Two); Wale wanaofanya kilicho sahihi baada ya kuambiwa mara moja.

Hawa ni wauzaji ambao hawawezi kujiongoza wenyewe kwenye nini wafanye, lakini wanapoambiwa kile wanachopaswa kufanya, huwa wanatekeleza mara moja. Hawasubiri kurudia kuambiwa au kusukumwa ndiyo wafanye. Hawa pia huwa wanajidhibiti wenyewe na wanapata matokeo mazuri lakini siyo kama wale wa daraja la kwanza. Hawa huwa wanakuwa wauzaji wazuri.

Daraja la Tatu (Division Three); Wale wanaofanya kilicho sahihi baada ya kuambiwa zaidi ya mara moja.

Hawa ni wauzaji ambao mpaka wasukumwe sana ndiyo wanatekeleza majukumu yao ya mauzo. Ni mpaka warudie rudie kuambiwa na wakati mwingine kuadhibiwa ndiyo wafanye. Hawa hawawezi kijidhibiti wao wenyewe hivyo wanaishia kudhibitiwa. Huwa wanaishia kuwa wauzaji wa kawaida na kupata matokeo ya kawaida kwenye mauzo.

Daraja la Nne (Division Four); Wale wanaofanya kilicho sahihi baada ya kusukumwa na mahitaji waliyonayo.

Hawa ni wauzaji ambao watafanya mchakato wa mauzo pale wanapokuwa na shida ya kutimiza mahitaji waliyonayo. Wakishakamilisha mahitaji yao, hawafanyi tena. Hawa hawawezi kabisa kujidhibiti kufanya na wala hawawezi kudhibitiwa. Wanaishia kupata matokeo ya chini na kuwa wauzaji wasio bora.

Daraja Sifuri (Division Zero); Wale ambao hawafanyi kilicho sahihi hata baada ya kuambiwa, kuonyeshwa na kulazimishwa wafanye.

Hawa ni wauzaji ambao hawafanyi chochote wanachopaswa kufanya hata wafanywe nini. Hawa hawawezi kujidhibiti wala kudhibitiwa na matokeo yake hawadumu kabisa kwenye mauzo.

Wauzaji wanaofanya mauzo makubwa wanakuwa kwenye daraja la kwanza na daraja la pili. Chini ya hapo wanakuwa wauzaji ambao siyo bora na mauzo yao yanakuwa siyo makubwa.

Ili kuwa daraja la kwanza na la pili, ni lazima uweze kujidhibiti wewe mwenyewe kwenye ufanyaji. Kwa sababu usipoweza kujidhibiti mwenyewe, hata usukumwe kiasi gani, hutaweza kuwa bora na kufanya mauzo makubwa.

TATHMINI BINAFSI.

Kutokana na haya uliyojifunza kwenye somo hili, jifanyie tathmini hii fupi binafsi;

1. Je umekuwa unajidhibiti mwenyewe kwa kufanya yanayopaswa kufanyika hata kama hujisikii kufanya?

2. Kwenye madaraja matano ya wauzaji, wewe unajiona uko kwenye daraja gani?
3. Kwa daraja unalojiona, toa ushahidi halisi wa kwenye mauzo unaofanya uwe kwenye daraja hilo.

Jidhibiti wewe mwenyewe kwa kutekeleza yale yanayopaswa kufanyika kwenye mauzo hata kama hujisikii kufanya. Ni kwa njia hiyo ndiyo unakuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa. Hakikisha unakuwa kwenye daraja la kwanza au la pili la wauzaji ili kuwa bora na kuuza kwa ukubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.