Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.
Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.
Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.
Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 59 na 60
Kwenye mbinu namba 59 tulijifunza ukamilishaji wa mtu muhimu.
Na kwenye ukamilishaji wa namba 59 tulijifunza mara zote chukua muda wa kumtambua na kumthamini mteja, na pale unapokutana na mtu mwenye ushawishi na umaarufu, mwonyeshe unatambua na kuthamini hilo. Watu wanapenda sana kutambuliwa, kuthaminiwa na kuonekana ni wa muhimu. Ukionyesha hilo kwa watu utaweza kukamilisha mauzo zaidi.
Na kwenye ukamilishaji wa mtu wa tatu, mbinu namba 60 tulijifunza kwamba unatumia ukamilishaji huu pale unapohitaji uthibitisho wa mtu mwingine kwenye mauzo.
Kwa kumuuliza mteja kama nikimshawishi muuzaji akakubalina na hilo, je utakua tayari kukamilisha mauzo sasa, unamfanya mteja aone uko upande wake na hivyo kukubali kukamilisha mauzo.
SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 59-60
Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 61 na 62.





Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;
- Ukamilishaji wa kujipongeza.
Watu wengi wanaona maisha ni ya mateso na hivyo kutokuyafurahia.
Pale mteja anapoona analipa gharama kubwa, mkumbushe kwamba anapaswa kuyafurahia maisha, hivyo ajipongeze.
Kwa mfano, mteja anakuambia gharama ni kubwa, unamjibu hivi;
“Ni kweli gharama ni kubwa, lakini siyo kitu unachofanya kila siku. Jipongeze leo. Weka sahihi yako hapa, kamilisha malipo ili uende ukafurahie uwekezaji wako mzuri, lipia sasa, ipi njia nzuri kwako kukamilisha malipo sasa?
- Ukamilishaji wa kufanya kazi kwa juhudi.
Watu wengi wanafanya kazi kwa juhudi, lakini bado hawathamini hilo. Wakumbushe kwamba sababu ya wao kufanya kazi kwa juhudi ni kupata vitu vizuri kama unachomuuzia na atakuwa tayari kuwa nacho
Kwa mfano, mteja anakuambia gharama ni kubwa,
Unamjibu hivi;
“Najua ni gharama kubwa. Na ndiyo maana watu kama wewe mnafanya kazi kwa juhudi, ili kuweza kumudu vitu vizuri kwenye maisha. Weka sahihi yako hapa, tafadhali lipia, ipi njia nzuri kwako kukamilisha malipo?
Lipia sasa ili uende ukafurahie juhudi zako”
Mwisho, Ukamilishaji ni hatua muhimu kwa kila mtu kupata kila anachotaka kwenye maisha yake.
Kwenye mazungumzo yoyote yale na mteja, hakikisha kuna kitu unakamalisha. Usikubali kutoka mikono mitupu, pambana kuhakikisha juhudi ulizoweka haziendi bure.
Kama umekosa mauzo, basi upate hata miadi, namba ya simu ya kuendelea kumfuatilia na mteja wa rufaa.
Kauli yetu inasema ABC-always be closing mara zote unapaswa kukamilisha wateja.
Nenda kakamilishe mauzo makubwa kadiri ya malengo yako uliyojiwekea leo.
Nenda leo ukawe mkamilishaji bora kabisa kuwahi kutokea na ukauze zaidi kupitia mbinu ulizojifunza leo na mbinu nyingine za nyuma ulizojifunza.
Shika kichwa chako na jiambie kauli hii; Mimi … (Taja jina lako)
Ni muuzaji bora kuwahi kutokea.
Mimi ni mkamilishaji bora wa mauzo na leo ninakamilisha mauzo ya Tsh….Taja kiasi kwa kila mteja niliyemweka kwenye mchakato wa mauzo
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy, 0717101505