3501; Tatizo ni unachojifunza.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu vinavyofanya mafanikio yawe magumu ni yale tunayojifunza.

Huwa tunajifunza kupitia yale tunayofanya na matokeo tunayopata.

Hapo kwenye matokeo tunayopata huwa ni rahisi sana kujidanganya kwa kujifunza vitu ambavyo siyo sahihi.

Kuna nyakati ambazo huwa tunapata matokeo ambayo hayajatokana na kile tulichofanya.

Lakini bado sisi tunakuwa tunahusianisha matokeo hayo na juhudi tulizoweka.
Hivyo tunaendelea kuweka juhudi tulizohuanisha, lakini katokeo hayajirudii.

Hilo limekuwa linawavuruga wengi kwenye safari yao ya mafanikio.
Wanakazana kufanya yale wanayodhani ndiyo yamechangia matokeo, lakini hawayapati.

Mwisho wanaamini mafanikio ni magumu au hayawezi kutabirika.
Lakini ukweli ni kwamba siyo kila matokeo yanatokana na juhudi ambazo tumeweka.

Kuna nyakati ambazo matokeo yanatokana na nafasi tu.
Ni muhimu kuyajua na kuyatofautisha matokeo ya aina hiyo ili yasikuvuruge.

Ndiyo maana ni muhimu sana kujitathmini kwenye kila hatua.
Ni kupitia kujitathmini ndiyo utaweza kujua kama matokeo yametokana na juhudi ulizoweka au nafasi tu.

Unachohitaji ni kuwa na mchakato ambao unaufuata mara zote kwenye kuyaendea mafanikio unayoyataka.

Ukiurudia rudia mchakato kwa muda mrefu, unakuwa na matokeo mazuri yanayotabirika.

Unapofanya nje ya mchakato wako na ukapata matokeo fulani, ni rahisi kudhani matokeo hayo yametokana na ulichofanya.

Utajikuta unarudia kufanya hicho na kusahau kabisa mchakato wako ambao ni wa uhakika zaidi.

Mwisho wake unashindwa kupata mafanikio uliyotaka .

Rafiki, ni matokeo gani umewahi kuyapata na kujikuta unasahau au kupuuza mchakato wako sahihi na hilo kuathiri matokeo?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili tuone umuhimu wa kuzingatia mchakato.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE | 0678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com