Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya SABA ambayo ni Mpe Mtu Sifa Kwenye Kile Unachotaka Awe.
Na kwenye kanuni hiyo ya SABA, tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Kama kuna jinsi unataka mtu abadilike, mpe sifa ya kile ambacho unataka awe. Watu wanapopewa sifa fulani, huwa wanaishi kwa sifa hiyo.
Kwa mfano, mtu akipewa sifa ya uchelewaji au utoro basi ataishi kutunza sifa hiyo.
Kwenye mabadiliko unayotaka kwa mtu, mpe sifa ambayo atakazana kuiishi kila siku. Kama unataka awe msafi mpe sifa za msafi na atakuwa msafi.
Hivyo basi, tuwasifie watu kwenye yale mazuri tunayotaka kuyaona kutoka kwao. Kwani watu wanapenda msimamo, hivyo watafanya chochote kulinda msimamo wao. Wape watu sifa fulani na watahakikisha wanaiishi sifa hiyo.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Saba
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya NANE ambayo ni; Wape watu moyo na onesha kosa ni rahisi kusahihisha.
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Kama kuna kitu unatakiwa kukiepuka kwenye maisha yako ni kuwakatisha tamaa watu. Epuka sana kuwakatisha watu tamaa kwenye kosa ambalo wamefanya, hata kama ni kosa kubwa kiasi gani.




Watie watu moyo kwamba wanaweza kuwa bora zaidi ya hapo walipo sasa. Na kwa kosa ambalo mtu amefanya, usiegemee sana kwenye ubaya na ukubwa wa kosa, badala yake egemea kwenye njia za kusahihisha kosa hilo.
Kwa kufanya hivyo, watu wanapata matumaini kwamba wanaweza kufanya vizuri na pia kuona kosa walilofanya linarekebishika.
Kwa namna hii utaweza kujenga ushawishi kwa watu bila kuibua hasira au chuki.
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504