3506; Wape wanachotaka.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Safari ya mafanikio tayari ni ngumu,  lakini watu wamekuwa wanaifanya kuwa ngumu kuliko inavyopaswa kuwa.

Moja ya namna ambavyo watu wamekuwa wanaifanya safari yao ya mafanikio kuwa ngumu ni kuongeza hatua zisizokuwa muhimu.

Tayari kunakuwa na hatua ambazo mtu akizichukua anapata mafanikio.
Lakini mtu anachagua kuongeza hatua nyingine zinazorefusha mchakato, lakini zisizokuwa na umuhimu wowote.

Kwa mfano mafanikio kwenye biashara ni kuweza kupata pesa.
Na namna pekee ya kupata pesa ni kuwapa wateja suluhisho la matatizo ambayo wanayo.

Hivyo njia rahisi ya kufanikiwa kwenye biashara ni kuwapa wateja kile wanachotaka ili na wao wakupe wewe pesa.

Kuna mengi unayoweza kuona ni muhimu kuyafanya hapo katikati, lakini ni hatua za ziada ambazo zitakuchelewesha kupata kile unachotaka.

Kwa mfano unaweza kuona huwezi kuanza mpaka uwe umeweza kutumia kila aina ya teknolojia mpya iliyopo. Lakini wateja hawataki teknolojia mpya, wanataka suluhisho, ambalo unaweza kuwapa bila hata kusubiri teknolojia mpya.

Wengi wamekuwa wanaona bado hawajawa tayari kuanza mpaka wakamilishe hatua za aina fulani, ambazo hazihusiani kabisa na kuwapa watu kile wanachotaka.

Kadiri unavyochelewa kuwapa watu kile wanachotaka, ndivyo unavyoacha wazi fursa hiyo kwa wengine kuifanyia kazi.

Usidhani fursa unayokuwa umeiona ni wewe tu umeona, kuna wengine wengi ambao wanakuwa wameiona.
Anayefanikiwa ni yule anayekuwa na kasi kwenye kuwapa watu kile wanachotaka.

Kwenye chochote unachofanya au kupanga kufanya, angalia ni hatua zipi za msingi ambazo zitakupa matokeo unayoyataka bila ya kusubiri kwa muda mrefu.

Hicho ndiyo unachotaka, kuwapa watu kile wanachotaka bila ya kukwamishwa na chochote ili na wao wawe tayari kukupa wewe kile unachotaka.

Rafiki, ni hatua zipi zisizokuwa na umuhimu ambazo umekuwa unaziongeza kwenye safari yako ya mafanikio na zinakuchelewesha?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uweze kuziacha hatua hizo na kuwapa watu kile wanachotaka na wao wakupe unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana, Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe