3507; Bora, Haraka na Nafuu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye kuongeza ufanisi wa kitu chochote kile, maeneo matatu yanapaswa kuzingatiwa; ubora, muda na bei.

Kitu kinapaswa kuwa bora zaidi ili kutoa thamani kubwa kwa wale wanaokitumia.
Ubora ni eneo muhimu linalofanya kitu kuwa vile kinavyopaswa kuwa.

Kitu kinapaswa kufanyika kwa haraka ili kuwa na tija zaidi. Muda ni kitu ambacho watu hawana, hivyo unapohitajika kwa uchache kwenye kitu, inasaidia.

Kitu kinapaswa kuwa nafuu ili watu waweze kukimudu. Watu huwa wanazingatia bei kwenye kufanya maamuzi juu ya kitu fulani.

Changamoto kubwa kwenye mambo hayo matatu ni ukigusa eneo moja, inaathiri kwenye hayo maeneo mengine.

Ukiongeza ubora itachukua muda zaidi au kuongeza gharama.

Ukipunguza muda, itashusha ubora au kuongeza bei.

Na ukipunguza bei, ubora utashuka au muda utaongezeka.

Njia pekee ya kuongeza ufanisi kwenye kitu ni kuongeza kimoja bila kuathiri vingine viwili.

Uongeze ubora huku muda na bei vikibaki vile vile.
Upunguze muda huku ubora na bei vikibaki vile vile.
Au upunguze bei huku ubora na muda vikibaki vile vile.

Njia pekee ya kuweza kufanikisha hilo la kuongeza eneo moja bila kuathiri maeneo mengine ni kuja na ugunduzi mpya.

Kuboresha tu yale yaliyopo hakuwezi kupandisha eneo moja bila kushusha maeneo mengine.

Lazima uje na namna mpya ya kufanya mambo ndiyo utaweza kufanikisha.
Ni namna hiyo mpya inayoleta mapinduzi na manufaa makubwa kwenye kile ambacho mtu anafanya.

Matokeo yoyote bora unayotaka kufanya, cheza na vitu hivyo vitatu. Ukiweza kuongeza kimoja huku ukihakikisha vingine viwili havishuki utapata matokeo bora.

Rafiki, kwenye shughuli zako kuu, unawezaje kupandisha angalau eneo moja kwenye ubora, uharaka na unafuu, bila ya kushusha maeneo mengine mawili?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uweze kuja na njia za kipekee za kuongeza ufanisi kwenye kile unachofanya.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe