3517; Siyo fedha pekee.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Watu wamekuwa na malalamiko kwamba fedha haiwezi kununua furaha.

Hii ni kauli maarufu sana, hasa kwa wale ambao hawana fedha nyingi.

Ni kweli kabisa kwamba fedha haiwezi kununua furaha.

Lakini siyo fedha peke yake, bali ni kila kitu kwenye maisha hakiwezi kununua furaha.

Vitu vyote tunavyokuwa navyo kwenye maisha huwa vinaweza kutupa raha ya muda mfupi, ambayo huwa ni ya kupita tu.

Furaha ya kudumu kwenye maisha yetu huwa haiwezi kutoka nje yetu.
Hakuna kitu au mtu mwenye uwezo wa kutupa furaha inayodumu kwenye maisha yetu.

Furaha ni kitu kinachoanzia ndani ya mtu mwenyewe, kwa jinsi alivyo na yale anayoweza kufanya.

Kutegemea furaha itoke nje ni kujiandaa kuangushwa, kwa sababu ni kitu kisichowezekana kabisa.

Fedha, kama ilivyo kwa vitu vingine kwenye maisha, ni rasilimali ambayo tukiweza kuitumia vizuri, tutaweza kunufaika zaidi.

Kama huna furaha, usianze kuangalia vitu vya nje ambavyo unaona vimeshindwa kukupa furaha.
Badala yake anzia ndani yako mwenyewe, angalia ni nini ambacho umeshindwa kufanya mpaka ukakosa furaha.

Tusichanganye mambo na kujifariji kwenye yale ambayo hayajaweza kutupa kile tunachotaka hasa.

Kila kitu kwenye maisha yako unawajibika nacho wewe mwenyewe.
Shika hatamu ya maisha yako na chagua kuwajibika kwa kila kitu ili maisha yako yawe vile unavyotaka.

Rafiki, ni vitu gani umekuwa unalalamikia kwamba havikupi kile unachotaka kwenye maisha yako? Je unajua wewe peke yako ndiye unayewajibika kwenye maisha yako? Nini unaanza kufanya sasa ili kushika hatamu ya maisha yako?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili ufanyie kazi kweli na kunufaika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe