Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Leo ikiwa ni jumamosi ya ushawishi, tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI, BALI UNACHOMSHAWISHI
Kabla hatujaendelea na somo zuri la leo, tujikumbushe kidogo kile tulichojifunza wiki iliyopita.
Wiki iliyopita kwenye somo la ushawishi tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya tisa ambayo ni; wafanye wengine kufurahia unachopendekeza wafanikiwe.
Na kwenye kanuni hii tulifanikiwa kujifunza kwamba kama unataka watu wawe tayari kufanya kile unachotaka wafanye,na wajitume kweli kwenye kukifanya, basi wafanye wafurahie kufanya kitu hicho.
Kifanye kuwa kitu muhimu au wape nafasi ya kipekee katika kukifanya na watakuwa tayari kukifanya kitu hicho vizuri.
Kwa kuzingatia kanuni hii, utakuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine, watakuwa tayari kufanya kile unachowataka wafanye kwa sababu wanajua watanufaika.
Kwa kuwa watu ni wabinafsi, wanaojali mambo yao kuliko ya wengine, hakuna anayeweza kukataa kufanya kile kinachomnufaisha.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Tisa
Habari njema zaidi ni kwamba, leo kwenye somo letu la jumamosi ya ushawishi tunakwenda kujifunza Kanuni Kuu Yenye Ushawishi Mkubwa Kwa Wengine Itakayokusaudia Kujenga Na Kuimarisha Mahusiano Yako.

Tokea tuanze kujifunza masomo ya ushawishi mpaka sasa tumeshajifunza kanuni tatu za kukabiliana na watu, njia sita za kuwafanya watu wakukubali, kanuni 12 za kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako na jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki na tukajifunza kanuni tisa za kuwa kiongozii bora.
Kwenye vitabu vya kidini, tumeona ni kwa namna gani hapo awali watu walivyokuwa na amri nyingi, Musa aliwapa watu wake amri zaidi ya mia 6 kutoka katika torati.
Amri zilikuwa nyingi sana, kiasi kwamba watu walishindwa kuzishika zote.
Baadaye Musa, akazungumza na Mungu, akampatia 10 za Mungu ambazo waumini wa dini za Kikristu wanazitumia mpaka leo.
Licha ya mambo kurahisishwa kutoka mia 6 mpaka 10 bado watu jamii ya kale waliona ni nyingi.
Baada ya ujio wa Yesu, yeye alikuja kuhitimisha amri zote kuwa amri moja. Baada ya watu kuona amri 10 ni nyingi, yeye akaja na amri kuu ambayo ni moja tu ukiifuata basi umeshika amri zote ambayo ni amri kuu ya upendo.
Ukiishi kwa ukamilifu amri ya upendo basi umeishi amri zote.
Vivyo hivyo katika masomo yetu ya ushawishi, tumejifunza vitu vingi, kwa kuwa una mambo mengi na huwezi kushika kila kitu, basi nimekurahisishia kazi, utaweka juhudi kidogo tu na kupata matokeo mazuri.
Nimekuletea kanuni zote tulizojifunza kwenye masomo ya ushawishi na kuwa kanuni MOJA. Kwa kuweka zote kwa pamoja tunakwenda kutoka na kanuni kuu ambayo tukiweza kuishi kwenye kila siku ya maisha yetu, tutakuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine, kitu kitakachopelekea kujenga ushawishi na kuimarisha mahusiano yetu na wale tunaohusiana nao.
Kwa sababu, kwenye maisha hatupati kile tunachostahili bali tunachoshawishi.
Na kanuni hiyo ni; jali wengine na weka maslahi yao mbele.
Hiyo kanuni imemaliza kila kitu, kwa sababu tumejifunza jinsi ambavyo kila mtu anajijali yeye mwenyewe.
Hivyo wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, ukiacha kujijali mwenyewe tu na kuanza kuwajali wengine, utakuwa wa tofauti na watu wataona unawathamini kiasi cha kuwa tayari kukubaliana na wewe.
Kuishi kanuni hii, inakutaka uende kinyume na maisha yako. Kwa nini?
Kwa sababu, kwa mazoea huwa tunajijali sana sisi wenyewe, tunataka kupata tunachotaka, tunaongea kile kinachokuja kwenye mawazo yetu na kukosoa kila tunachokiona.
Kumbe basi, unapaswa kujizuia kuendelea na mazoea yako. Kabla hujafanya chochote ni muhimu sana kujiuliza kama hicho unachotaka kufanya, je kitamfanya mtu huyo ajione ni wa thamani na kujisikia vizuri?
Tahadhari nyingine, tumeona nguvu ya kanuni hizi, hivyo zitumie vizuri kwa uaminifu na kwa usahihi. Kwa nini tunasema hivyo?
Kwa sababu unaweza kuzitumia kwa njia isiyo ya sahihi na uaminifu. Zitakupa matokeo unayotaka lakini zikaharibu nafasi za mbeleni.
Wanasema hivi, paka mwenye malengo hali panya mwenye mimba.
Wewe kuwa kama paka mwenye malengo. Usiharibu uwekezaji mzuri ulikuwa nao na watu, kiasi kwamba ukashindwa kunufaika kwa mbeleni.
Kumbuka pia, kanuni hizi hazilingani, siyo zote zitafanya kazi kwenye kila eneo na kila wakati.
Hivyo, unapaswa kupima hali unayokabiliana nayo na kuona kama kanuni husika itasaidia.
Lakini kumbuka kwamba, mwongozo wako mkuu unapaswa kuwa kuweka maslahi ya mtu mwingine mbele, kumfanya ajione ni wa muhimu na wa kipekee.
Mwisho kabisa, usiikatae kanuni kabla hujaijaribu, kumbuka inafanya kazi kama ukiifanyia kazi. Usijiambie hii haiwezi kufanya kazi kwa upande wangu, jaribu kwanza.
Mwandishi Dale Carnegie anasema, kama unaridhika na matokeo unayopata sasa, basi endelea kufanya kile unachofanya.
Lakini, kama matokeo unayopata hayakuridhishi, kuna ubaya gani ukajaribu kitu kipya na kuona matokeo yake?
Kulingana na changamoto za mahusiano au ushawishi unazokabiliana nazo, chagua kanuni inayoendana na kile unachopitia na ijaribu. Usiseme kanuni haifanyi kazi kama hujaijaribu, kumbuka, inafanya kazi kama ukiifanyia kazi.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504