3519; Thamani ya pesa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Unapotoa fedha yako kulipia kitu chochote kile, huwa unazingatia sana ni thamani gani unayopata kwa fedha unayokuwa umeweka.

Kama umelipa gharama kubwa lakini unapata thamani ndogo, huwezi kukubali kabisa.
Lazima utataka upate thamani sawasawa na fedha uliyolipa.

Kwa mfano kama umeajiri mfanyakazi wa mauzo ambaye unamlipa fedha nyingi, hutaridhika pale utakapomkuta anatumia nusu ya siku yake ya kazi kusafisha ofisi.

Kwa fedha nyingi unayomlipa unataka atumie muda wake mwingi kukamilisha majukumu ambayo matokeo yake yatafidia kiasi hicho kikubwa unachomlipa.

Unakuwa sahihi kabisa pale unapotaka kupata thamani ya pesa yako.

Tatizo lako ni unakuwa na upendeleo kwenye kudai thamani ya pesa yako.
Kwani kuna mtu ambaye unamlipa sana, ila anatekeleza majukumu ambayo hayana thamani kabisa.

Fikiria mtu ambaye unamlipa zaidi kwenye biashara au kazi yako, lakini muda wake mwingi wa siku anautumia kufanya majukumu ambayo hayana tija kabisa.

Mtu huyo ni wewe mwenyewe.
Ukilinganisha kiasi cha fedha unachojilipa kutoka kwenye biashara au kazi yako na majukumu unayoyapa muda wako, haviendani kabisa.

Unahangaika na majukumu ambayo hayana thamani kabisa.
Majukumu ambayo japokuwa ni muhimu yakamilishwe, kuna wengine wanaweza kuyafanya kwa gharama kidogo.

Matokeo yake ni unajichosha sana na kujizuia kukuza zaidi biashara yako na kuingiza kipato kikubwa zaidi.

Ni wajibu wako namba moja kuhakikisha majukumu unayotekeleza ni yenye thamani kubwa kulingana na kile unachojilipa.

Majukumu yote ambayo wengine wanaweza kuyakamilisha vizuri na ukawalipa kiasi kidogo cha fedha kuliko unachojilipa wewe, wape wayafanye majukumu hayo.

Kufanya hivyo kutakupa muda mwingi wa kufanya majukumu ya thamani ya juu zaidi na kukupa ukuaji mkubwa.

Ukianza kujidai wewe mwenyewe ujipe thamani sahihi kama unavyowadai wengine unaowalipa, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com