Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Mafanikio kwenye maisha hayatokei mara moja kama ajali. Bali mafanikio ni mkusanyiko wa mambo madogo madogo ambayo yamefanywa vizuri. Kwa bahati mbaya sana watu wamekuwa wanapuuza mambo madogo madogo yanayojenga mafanikio makubwa na matokeo yake wanashindwa kufanikiwa.

Ili kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha, unapaswa kuweka umakini kwenye mambo madogo madogo ambayo ndiyo yanachangia mafanikio hayo. Kama unataka kupata ushindi mkubwa, anza kwa kupata ushindi mdogo mdogo kwenye maeneo mengi ya maisha yako.

Kwenye mauzo, ushindi ni mteja kukubali kununua. Hicho ndiyo kitu ambacho kila muuzaji huwa anakazana kukipata kwenye mambo yote anayoyafanya. Lakini kila muuzaji anajua wateja wengi huwa hawakubali kununua mara ya kwanza wanaposhawishiwa kununua. Wengi hukataa na kutoa sababu mbalimbali.

Kama muuzaji atahesabu ushindi ni mauzo pekee, mara zote atajihesabu kuwa mtu aliyeshindwa. Kwa sababu kila anapomtaka mteja anunue kwa mara ya kwanza, atakataa.

Uzuri ni kwamba mauzo huwa ni mchakato ambao una hatua mbalimbali. Kabla ya kufika hatua ya mwisho ya mteja kununua, kuna hatua nyingi ambazo mtu akiweza kumvusha mteja anakuwa amejisogeza karibu zaidi na ushindi wa mwisho ambao ni mteja kununua.

Hivyo kama unataka kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa, unapaswa kuwa na njia ya kupata na kusherekea ushindi mdogo mdogo kwenye mchakato mzima wa mauzo.

USHINDI MDOGO MDOGO WA KUKUSANYA KWENYE MCHAKATO WA MAUZO.

Mchakato wa mauzo una hatua mbalimbali ambazo mteja anapaswa kuvushwa ili ashawishike kununua. Muuzaji anayetaka kupata ushindi wa mwisho, anapaswa kuweka umakini wake kushinda hatua hizo za mchakato ili ushindi wa mwisho uwe uhakika kwake.

Ufuatao ni ushindi mdogo mdogo ambao muuzaji anaweza kukusanya na kujihakikishia ushindi wa mwisho ambao ni kukamilisha mauzo.

1. Kumpata mteja tarajiwa mwenye sifa.

Kupata mteja tarajiwa mwenye sifa ambazo biashara inalenga ni ushindi mkubwa. Kumfuatilia mteja tarajiwa mwenye sifa kunakusogeza karibu zaidi na mauzo kuliko kufuatilia mteja ambaye hana sifa.

Ushindi; hakikisha unapata wateja tarajiwa wenye sifa ili ushindi wa mauzo uwe wa uhakika.

2. Mteja kujua kuhusu uwepo wa biashara.

Mteja anapojua kuhusu biashara yako na kile unachouza ni ushindi mkubwa. Moja ya vikwazo vya mauzo ni wateja kutokujua kuhusu uwepo wa biashara. Yaani biashara inaweza kuwa na suluhisho la matatizo ambayo watu wanayo, lakini watu hao wenye matatizo wasijue kama biashara hiyo ipo.

Ushindi; hakikisha watu wengi zaidi wanajua kuhusu biashara yako ili wale wenye sifa wajitokeze na waweze kufuatiliwa.

3. Uwasilishaji kufanyika kwa mteja.

Mteja anapopata uwasilishaji wa bidhaa au huduma inayouzwa, akaelezwa thamani anayokwenda kupata na jinsi maisha yake yanakwenda kuwa bora ni ushindi mkubwa. Kwa kujua jinsi anavyoweza kunufaika, inafanya awe rahisi kushawishika.

Ushindi; fanya uwasilishaji kwa wateja wengi zaidi na utawafanya wenye uhitaji kushawishika kununua kwa kuona thamani watakayopata.

4. Mteja kutoa mapingamizi.

Hapa ndipo wauzaji wengi huwa hawaelewi, wakiwasilisha kwa mteja na kumtaka anunue halafu akatoa mapingamizi, huwa wanaona wameshindwa kuuza. Ukweli ni wateja wenye mapingamizi ndiyo wateja wazuri kununua. Wanakuwa na mapingamizi kwa sababu wanakitaka kitu ila kuna namna haijakaa sawa kwao. Ukiyajibu mapingamizi ni rahisi kuwashawishi.

Ushindi; pata mapingamizi mengi ya wateja na kuwa na majibu ya mapingamizi hayo ili uweze kuwashawishi kununua.

SOMA; Jenga Mtandao Wako Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

5. Mteja kuendelea kufuatiliwa.

Mteja anapokataa chochote anachokuwa amefanyiwa, iwe ni kuombwa kuwasilishiwa au kutokujibu mawasiliano yanayofanyika, siyo mwisho wa mchakato wa mauzo. ufuatiliaji endelevu huwa unawalainisha wateja hao mpaka wanashawishika kununua.

Ushindi; usiache kumfuatilia kila mteja unayemweka kwenye mchakato wa mauzo, hata kama ametoa majibu ya aina gani.

6. Mteja kukubali kununua kwa mara ya kwanza.

Mteja anapokubali kununua kwa mara ya kwanza ni ushindi mkubwa. Hilo linakuwa limetokea baada ya ufuatiliaji wa muda mrefu bila kukata tamaa. Lakini pia ndiyo mwanzo wa safari ya kuendelea kumuuzia mteja kwa muda mrefu.

Ushindi; kazana mpaka mteja akubali kununua japo kwa mara ya kwanza, baada ya hapo inakuwa rahisi zaidi kumuuzia.

7. Mteja kurudi tena kununua.

Unaweza kutumia mbinu nyingi kumshawishi mteja akubali kununua kwa mara ya kwanza. Lakini kama hatapata thamani aliyotegemea, hatorudi tena kununua hata utumie mbinu gani. Hivyo mteja anaporudi tena kununua ni kiashiria amepata thamani nzuri na huo ni ushindi.

Ushindi; usikubali mteja kununua kwako mara moja na asirudi tena, jenga mahusiano mazuri na wateja ili waendelee kununua.

8. Mteja kuleta wateja wengine.

Mteja anaweza kununua mwenyewe lakini asiwe tayari kuleta wengine kwa sababu hataki kuonekana ni mbabaishaji. Mteja akikubali kuleta wateja wengine nao wanunue kwako ni ushindi. Hapo ameonyesha ana uhakika na biashara yako na yupo tayari kuwaleta wengine nao wanufaike kama yeye.

Ushindi; waombe wateja wakupe wateja wengine kutoka kwa watu wanaowajua, ni njia rahisi ya kupata wateja bora.

9. Mteja kutoa ushuhuda.

Mteja anapotoa ushuhuda wa jinsi kile alichonunua kimemsaidia, inakuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine ambao bado hawajanunua. Watu wanaamini ushuhuda wa waliotumia kitu kuliko maelezo yako muuzaji. Na kama mteja atakubali kutoa ushuhuda, maana yake amenufaika kweli.

Ushindi; waombe wateja wakupe ushuhuda wa jinsi walivyonufaika na walichonunua na tumia ushuhuda huo kushawishi wengine.

10. Mteja kuwa shabiki wa kweli.

Mteja ambaye ni shabiki wa kweli ni yule anayeitetea biashara mahali popote pale bila hata ya kutakiwa kufanya hivyo. Mteja anakuwa ameikubali sana biashara na anataka kuiona ikipiga hatua na kufanikiwa. Wateja ambao ni mashabiki wa kweli huwa ni kama wauzaji wa biashara hiyo, wanakuwa na ushawishi mkubwa wa kuleta watu wengine.

Ushindi; wape thamani kubwa wateja na jenga nao mahusiano bora ili waikubali biashara na kuwa mashabiki wa kweli ambao wataitangaza na kuitetea biashara kila mahali wanapokuwa.

PATA USHINDI KILA SIKU.

Kwenye hatua hizo zote za mchakato wa mauzo, unaona kuna ushindi mwingi mdogo mdogo unaoweza kupata kila siku. Hakikisha kila siku yako ya mauzo unakusanya ushindi mwingi mdogo mdogo. Hakikisha kwa kila mteja unayemgusa kwa siku, kuna ushindi umepata.

Hata kama mteja hajakubali kununua siku hiyo, hakikisha unatoka na ushindi wowote mdogo kama tulivyojifunza kwenye hizo hatua 10 hapo juu. Kupata hapana ya mteja ni ushindi kuliko kutokumgusa mteja kabisa. Kwa sababu mteja aliyekuambia hapana anajua kuhusu uwepo wako, wakati ambaye hujamfikia kabisa hajui hata kama upo.

Kila mchakato unaotekeleza kwenye mauzo ni nafasi ya kupata ushindi ambao utakusogeza karibu na kukamilisha mauzo. Usihesabu ushindi wa mauzo pale unapokamilisha mauzo pekee. Badala yake hesabu na sherekea kila hatua unayomgusa mteja bila ya kujali matokeo gani umeyapata. Kwani kitendo cha kumgusa tu mteja, kinakusogeza karibu zaidi na kukamilisha mauzo kuliko kutokumgusa mteja kabisa. Kila siku kusanya ushindi mdogo mdogo kwa wateja wote unaowagusa na utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.