3520; Ni hatua kwa hatua.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye maisha kila kitu huwa kina ngazi ambazo kinapitia.
Kabla ya kwenda ngazi za juu, lazima ngazi za chini zikamilishwe kwanza.

Mfano dhahiri ni mtoto mdogo, ambaye huwa anaanza na hatua ya kukaa, kisha kutambaa, kutembea na hatimaye kukimbia.

Hakuna atakayemshangaa mtoto ambaye anaanza kujifunza kukaa kabla hajakimbia.
Lakini kila mtu atamshangaa mtoto ambaye anakimbia kabla hata hajakaa.

Inapokuja kwenye safari ya mafanikio, mchakato ni huo huo wa kwenda hatua kwa hatua.

Cha kushangaza huku watu hawaelewi, wanataka wakimbie kabla hata hawajakaa.

Wanahangaika sana na kutafuta njia za mkato za kwenda ngazi ya juu kabla ya kupita ngazi za chini.

Lakini matokeo yake hayajawahi kuwa mazuri.
Hakuna kitu chochote kwenye asili kinachovuka hatua zake za msingi na kikabaki salama.

Kwenye safari yako ya mafanikio, zijue hatua zote unazopaswa kupitia ili kufika kule unakotaka.

Ukishazijua hatua hizo, kazi yako kubwa ni kupita hatua zote, bila ya kuruka yoyote ile.

Unaweza kupita baadhi ya hatua kwa kasi kubwa, lakini huwezi kuruka hatua yoyote na ukapita salama.

Ukiona kupita hatua zote ni kupoteza muda, jaribu kuzikwepa baadhi ya hatua na uone jinsi utakavyopoteza muda mwingi zaidi.

Nenda hatua kwa hatua na utafika kwa uhakika.
Muhimu ni wewe tu usiiache safari.
Mara zote fanya kilicho sahihi na matokeo utayapata.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com