Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka kwenye programu yetu ya  CHUO CHA MAUZO.

Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.

Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.

Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 65 na 66

Kwenye mbinu namba 65 tulijifunza Ukamilishaji wa Muhtasari.

Na kwenye ukamilishaji wa namba 65 tulijifunza kwamba ukamilishaji huu unatumika mara baada ya kufanya mazungumzo na mteja na kumueleza kile unachouza.
Sasa unakuja kuhitimisha yale ambayo mmekubaliana kwa kumpa muhtasari.

SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 65-66

Na kwenye ukamilishaji wa namba 66,  Ukamilishaji huu unakufanya ujihakikishie kwamba kikwazo pekee kwao ni fedha. Na hivyo ukiweza kuwaonyesha njia za kupata fedha, wananunua. Ila kama fedha siyo kikwazo pekee, hawatakubali, hivyo utapaswa kujua kikwazo halisi.

Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 67 na 68

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;

  1. Ukamilishaji wa Ben Franklin.

Unatumia ukamilishaji huu kumwonyesha mteja thamani ya kitu ili ashawishike kufanya maamuzi. Onyesha faida zilivyo nyingi kuliko hasara.

Kwa mfano, pale mteja anapokupa pingamizi la kushindwa kufanya maamuzi ya kununua. Unatumia ukamilishaji huu na kumwambia hivi;

“Naelewa ni vigumu kiasi gani kufanya maamuzi. Inasemekana kwamba Ben Franklin, mmoja wa waasisi wa taifa la Marekani, alipokuwa na maamuzi magumu ya kufanya, aliandika faida na hasara za kitu kisha kufanya maamuzi kulingana na upande wenye vitu vingi.

(Chukua karatasi) Hivyo tuorodheshe faida na hasara za wewe kufanya haya manunuzi, kama faida zitakuwa nyingi kuliko hasara, nunua. Ila kama hasara zitakuwa nyingi kuliko faida, usinunue.”

Hivyo basi, tumia ukamilishaji huu kumwonyesha mteja thamani ya kitu ili ashawishike kufanya maamuzi. Onyesha faida zilivyo nyingi kuliko hasara.

  1. Ukamilishaji wa kulinganisha uwekezaji.

Ukamilishaji huu unamwonyesha mteja thamani kubwa anayokwenda kupata kwa tofauti ndogo ya malipo anayokwenda kufanya.
Kwa mfano, pale mteja anapokupa pingamizi la bei, unatumia ukamilishaji huu wa kulinganisha na manufaa anayokwenda kupata.

“Wacha tulinganishe kile ulichonacho sasa na hiki unachokwenda kupata.
Ukweli ni unalipa laki mbili na nusu kwa mwezi kwa sasa na malipo mapya yatakuwa laki 5 kwa mwezi.

Tuangalie manufaa unayokwenda kupata; eneo zuri, usalama zaidi na vitu vipya, yote hayo kwa tofauti ya elfu 8 tu kwa siku.”

Ukamilishaji huu unakufanya ujihakikishie kwamba kikwazo pekee kwao ni fedha. Na hivyo ukiweza kuwaonyesha njia za kupata fedha, wananunua. Ila kama fedha siyo kikwazo pekee, hawatakubali, hivyo utapaswa kujua kikwazo halisi.

Mwisho, Ukamilishaji ni hatua muhimu kwa kila mtu kupata kila anachotaka kwenye maisha yake.
Kwenye mazungumzo yoyote yale na mteja, hakikisha kuna kitu unakamalisha. Usikubali kutoka mikono mitupu, pambana kuhakikisha juhudi ulizoweka haziendi bure.
Kama umekosa mauzo, basi upate hata miadi, namba ya simu ya kuendelea kumfuatilia na mteja wa rufaa.

Kauli yetu inasema ABC-always be closing mara zote unapaswa kukamilisha wateja.
Nenda kakamilishe mauzo makubwa kadiri ya malengo yako uliyojiwekea leo.

Nenda leo ukawe mkamilishaji bora kabisa kuwahi kutokea na ukauze zaidi kupitia mbinu ulizojifunza leo na mbinu nyingine za nyuma ulizojifunza.

Shika kichwa chako na jiambie kauli hii;  Mimi … (Taja jina lako)
Ni muuzaji bora kuwahi kutokea.
Mimi ni mkamilishaji bora wa mauzo na leo ninakamilisha mauzo ya Tsh….Taja kiasi kwa kila mteja niliyemweka kwenye mchakato wa mauzo

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504