Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Tabia huwa zina mchango mkubwa kwenye mafanikio yetu kwa sababu yale tunayofanya kwa kujirudia rudia ndiyo yanayojenga maisha yetu. Lakini tabia siyo kitu ambacho tunazaliwa nacho, bali ni kitu tunachojifunza kwa kurudia rudia kufanya kwa muda mrefu.

Kwa kipindi kirefu ilikuwa ikiaminika kwamba hisia na fikra zetu ndiyo zilizoathiri matendo yetu, hivyo kwa mtu kuhisi na kufikiri kwa namna fulani, aliweza kutenda kwa namna hiyo. Mwanasaikolojia William James aliweza kuonyesha kwamba matendo pia yanaathiri hisia na fikra zetu. Kwamba mtu anapotenda kwa namna fulani, inachochea kufikiri na kuhisi kwa namna hiyo pia.

Ugunduzi huo uliweza kutuonyesha kitu kimoja kikubwa sana, ambacho ni tunaweza kujenga tabia ya aina yoyote ile, kama tutarudia rudia kuifanya bila kuacha. Na hapo ndipo dhana ya Igiza Mpaka Iwe (Fake It Until Yo Umake It) inapopata nguvu. Kwa dhana hii, tunaweza kuigiza kuwa watu wa aina fulani na kwa kurudia rudia kuigiza hivyo, tukaweza kuwa watu wa aina hiyo kwa uhalisia kabisa.

Dhana hiyo ya igiza mpaka iwe, inafanya kazi vizuri kabisa kwenye mauzo. Kwa kuigiza kwa namna fulani, tunaweza kuwa hivyo na hatimaye kufanikiwa kwenye mauzo.

MAENEO YA KUIGIZA MPAKA IWE KWENYE MAUZO.

Ili kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea, kuna maeneo ambayo tunaweza kuigiza kama ndivyo tulivyo na kuweza kujenga tabia sahihi ambayo itatupa mafanikio tunayotaka. Yafuatayo ni maeneo ambayo tukiweza kuigiza mpaka iwe, tutaweza kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

1. Igiza Kujiamini.

Kujiamini wewe mwenyewe ni hitaji kubwa sana kwenye kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Kabla ya wateja hawajaamini kile unachowaambia na kununua, lazima wakuamini kwanza wewe. Na ili wakuamini wewe ni lazima ujiamini wewe mwenyewe.

Changamoto kubwa ni kwamba wauzaji wengi hawajiamini. Hivyo wakipewa mapingamizi kidogo wanashindwa kuendelea. Mapingamizi mengi ya wateja huwa ni ya kupima unajiamini kiasi gani kwenye kile unachowaeleza.

Unaweza kujijengea kujiamini kwa kuigiza mpaka iwe. Unachofanya ni kuigiza kama mtu unayejiamini hata kama hujiamini. Onyesha kujiamini kwa kufanya mambo ambayo wanaojiamini wanayafanya. Kwa wateja kuona unajiamini, wanakuamini na kununua. Kwa wateja kununua inakupelekea kujiamini kweli na kuzidi kuwashawishi na kuwauzia wengi.

Unaanza kwa kuigiza kujiamini, wateja wanakuamini kweli na hilo linapelekea ujiamini kweli.

2. Igiza Shauku.

Shauku ni hisia muhimu sana kwenye mauzo. Huwezi kuuza kama huna shauku, kwa sababu mauzo ni maambukizo ya shauku. Wateja wananunua pale wanapopata shauku, kutokana na shauku ambayo muuzaji anakuwa nayo.

Changamoto ni watu wauzaji wengi huwa hawana shauku kubwa. Wanaongea kwa sauti ya chini kama vile hawataki kitu ambacho kinawafanya wateja wasivutiwe sana na kile wanachoambiwa.

Unaweza kuigiza kuwa mtu mwenye shauku, kitu kinachowapa wateja shauku kubwa na kuwashawishi kununua. Kwa wateja kupata shauku kutokana na maigizo yako na wakanunua, unapata shauku ya kweli na hivyo kuweza kuwashawishi wateja zaidi na kuwauzia wateja zaidi.

Kila unapokutana na wateja, au hata watu wengine wowote, jichochee shauku kubwa ndani yako. Ongea kwa sauti, kwa mapenzi makubwa na kujiamini na hilo litaibua shauku kubwa kwa wanaokusikiliza na kushawishika na wewe.

Hata kama watu tayari wanakuchukulia ni mtu usiye na shauku, wewe anza kuigiza shauku. Watakuambia umebadilika, lakini pia watashawishika na kukubaliana na wewe zaidi.

SOMA; Kuwa Bora Kwenye Majadiliano Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

3. Igiza Tabasamu.

Uso wako ni moja ya viungo muhimu kwenye kuwashawishi wateja kukubaliana na wewe. Uso wenye tabasamu huwa una ushawishi mkubwa kwa watu. Wauzaji wanaotabasamu wanauza zaidi kuliko wasiotabasamu. Uso wenye tabasamu unafungua mioyo ya wengine na kuweza kuwashawishi.

Tabasamu ni kitu ambacho unaweza kuigiza kama siyo kitu kinachotokea kwa urahisi kwako. Unachofanya ni kuigiza kuvaa uso wa tabasamu muda ambao uko peke yako. Simama mbele ya kioo na igiza tabasamu. Jiangalie ukiwa unaigiza tabasamu mpaka upate namna ambayo ukilazimisha tabasamu itaonekana ni halisi mbele ya wengine.

Kisha vaa tabasamu hilo la kuigiza muda wote, hasa pale unapokuwa na watu. Kwa kulazimisha tabasamu, uso wako utaambia fikra na hisia zako kwamba unajisikia vizuri, kitu ambacho kitapelekea ujisikie vizuri kweli. Kwa uso wenye tabasamu na hali ya kujisikia vizuri utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wateja na kuuza zaidi.

4. Igiza Ujasiri.

Hofu ni moja ya vitu vinavyowakwamisha watu kwenye maeneo mengi ya maisha yao. Wanakuwa wanajua wanachotaka na wanachopaswa kufanya, lakini hofu inawazuia kuchukua hatua. Wale wanaofanya kwa ujasiri huwa wanaonekana kama hawana hofu. Kiuhalisia wanakuwa na hofu kama wengine, lakini wanafanya licha ya hofu wanayokuwa nayo.

Unaweza kuvuka hofu kwa kuigiza ujasiri, kwa kufanya licha ya kuwa na hofu. Kwa kuigiza ujasiri, utaweza kufanya yale unayohofia na kuishinda hofu. Kwa sababu mara zote dawa ya hofu ni kufanya yale unayokuwa unahofia kufanya.

Kwa kuweza kuvuka hofu, utaweza kuwakabili wateja wa kila aina, utaweza kuwa na ung’ang’anizi na hatimaye kufanya mauzo makubwa. Igiza ujasiri hata kama una hofu kubwa ndani yako na utaweza kufanya makubwa ambayo umekuwa unayahofia.

5. Igiza Muuzaji Bora.

Kuwa muuzaji bora ni tabia ambayo inajengeka kutokana na matokeo ambayo mtu umekuwa unayapata. Pale unapofanya mauzo makubwa, unajichukulia kuwa muuzaji bora na kuendelea kupata mauzo makubwa zaidi.

Unaweza kuanza kuigiza kama muuzaji bora na hilo likapelekea uwe muuzaji bora kweli. Unachopaswa kufanya ni kujichukulia kama tayari wewe ni muuzaji bora. Kwa kila unachofanya, jione tayari wewe ni muuzaji bora. Fanya yale yote ambayo muuzaji bora anayafanya.

Kwa kuigiza kama muuzaji bora utaweza kufanya hiyo kuwa tabia yako na ikakuwezesha kuleta matokeo ambayo wauzaji bora wanayazalisha. Unaigiza kuwa muuzaji bora, hilo linapelekea uuze zaidi na kuwa muuzaji bora kweli.

Tahadhari Muhimu.

Dhana ya kuigiza mpaka iwe siyo kudanganya au kuwahadaa watu, bali ni kujilazimisha wewe mwenyewe kujenga tabia sahihi ambazo zitaleta matokeo ya halisi kwako.

Japokuwa ndani yako utaanza kufanya kwa kuigiza, kwa wateja ni lazima uwapatie matokeo halisi. Kama unaigiza kujiamini, ni lazima mteja umpe matokeo ya mtu anayejiamini kweli. Kadhalika unapoigiza ujasiri, lazima uchukue hatua za kijasiri zinazomnufaisha mteja.

Kwa kuwapa wateja matokeo halisi, hawatajali sana kama unaigiza au ndivyo ulivyo, wao watafurahia kunufaika na ile thamani unayowapa. Hivyo usijikwamishe kuigiza mpaka iwe kwa sababu unaona siyo sahihi, kwa sababu unachofanya ni sahihi kwa wateja na hilo ndiyo muhimu zaidi.

Kuigiza mpaka iwe ni dhana muhimu inayokuwezesha kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Kwa kuigiza kuwa mtu unayejiamini, mwenye shauku kubwa, unayetabasamu, jasiri na muuzaji bora itakufanya kuwa na ushawishi mkubwa kwa wateja na kuwa muuzaji bora na anayefanya mauzo makubwa kwa uhalisia.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.