Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Moja ya kanuni muhimu za mafanikio ni kutimiza yale unayoahidi. Yaani unapaswa kusema kitu, kisha kufanya kile ambacho umesema. Inaweza kuonekana ni kitu rahisi sana kwa kusema, lakini kwenye kutekeleza ni vigumu sana.
Watu huwa ni wepesi sana kuahidi mambo, lakini inapofika wakati wa kutekeleza wanakuwa wazito. Inawawia vigumu sana kwenye utekelezaji wa yale ambayo wameahidi wao wenyewe. Matokeo yake wanashindwa kuaminika na hilo linawanyima fursa nzuri za kupata yale wanayotaka.
Kwenye mauzo, kama unataka kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, unapaswa kuwa mtu wa kutekeleza yale yote unayowaahidi wateja wako. Ni kupitia kufanya hivyo ndiyo unajijengea sifa ya kuwa mtu anayeaminika na kuweza kufanya mauzo makubwa.

NGAZI TATU ZA KUAHIDI NA KUTIMIZA KWENYE MAUZO.
Kwenye mauzo, huwa kuna ngazi tatu za kuahidi na kutimiza, ambazo ndiyo zinaamua ni mafanikio kiasi gani ambayo mtu atayapata. Zijue ngazi hizo hapa na hatua za kuchukua ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Moja; Kutoahidi Na Kutotimiza.
Hii ni ngazi ya chini kabisa ambapo muuzaji haahidi chochote na wala hakuna anachotimiza na kikamfanya mteja avutiwe na kumwamini muuzaji. Kwenye ngazi hii, mtu anauza tu kwa mazoea na hata kwenye hayo mazoea, bado huduma ambayo wateja wanapata ni mbovu.
Kitu pekee kinachowafanya wateja kununua kwa wauzaji wasioahidi wala kutimiza ni wanapokuwa na mahitaji makubwa ambayo hawayapati mahali pengine au hawajajua pengine pa kuyapata. Wateja wa aina hiyo huwa wanaondoka haraka sana pale wanapopata mahali pengine wanapoweza kutimiza mahitaji yao.
Biashara na wauzaji walipo kwenye ngazi hii, ambao ni wengi, kila mara huwa wanapoteza wateja kitu kinachofanya mauzo kuwa magumu kwao. Wateja wakinunua kwao mara moja huwa ni vigumu kurudi tena kununua. Kwa sababu hakuna thamani kubwa ambayo wanaona wanaipata kwa watu hao.
Hatua ya kuchukua; Epuka sana kufanya mauzo kwa mazoea, kwa kutokuahidi na kutokutimiza. Usidhani kwamba tayari wateja wanajua nini wanapata kwa kununua kwako. Kila mara jikumbushe kwamba wateja wanapaswa kusikia upya ahadi ya biashara yako na kuona ikitimizwa ili kuwa na imani.
Mbili; Kuahidi Na Kutokutimiza.
Hii ni ngazi ya kati ambapo muuzaji anawaahidi wateja, lakini hatimizi kile ambacho anakuwa ameahidi. Kwenye ngazi hii, mteja anavutiwa na ahadi ambayo anakuwa ameisikia kwa muuzaji, kitu kinachokuwa kimempa mategemeo fulani. Lakini mteja anapochukua hatua ya kuchukua, matokeo yanakuwa tofauti kabisa na matarajio.
Kwa mteja kutokupata kile ambacho alitegemea kupata, anakosa imani kwenye biashara na wakati mwingine hashawishiki kununua. Kuahidiwa kitu na kisitimizwe kinawafanya wateja waone kama wamedhulumiwa kile ambacho walistahidi.
Biashara na wauzaji walio kwenye ngazi hii, ambao ni wengi, huwa wanapoteza wateja na kujijengea sifa mbaya ya kuonekana watu ambao wanajinufaisha kupitia wengine. Wanakuwa wamewapa watu matarajio makubwa na kisha kuwaangusha kwenye utekelezaji. Wengi huwa wanatoa sababu mbalimbali za kushindwa kutekeleza yale waliyoahidi, lakini huwa haisaidii. Kwa sababu wateja wakishakosa kile ambacho waliahidiwa, imani yao inashuka, kwa sababu wamekuwa wanakutana na hali hiyo mara nyingi.
Hatua ya kuchukua; Unapokuwa kwenye mauzo na hata maisha kwa ujumla, tekeleza yale yote ambayo umeyaahidi. Hiyo ndiyo ngazi ya chini kabisa ya mafanikio, itakayopelekea uaminike na watu. Ni afadhali hata uahidi madogo na kutimiza makubwa kuliko uahidi kawaida na kutokutimiza kabisa. Kama umemwambia mteja atapata A, B, C na D, kisha ukampa A, B na C, utakuwa hujatimiza uliyoahidi na hivyo kupoteza imani. Lakini kama umemwambia mteja atapata A na B, kisha ukampa A, B na C, utakuwa umetimiza zaidi ya ulivyoahidi, kitu kitakachopelea uaminike zaidi. Utaona kwenye mifano hiyo miwili, kilichotekelezwa ni kile kile, A, B na C, lakini imani ni tofauti kutokana na ahadi inayokuwa imetolewa.
Tatu; Ahidi Makubwa Na Timiza Makubwa.
Hii ni ngazi ya juu kabisa ambapo muuzaji anawaahidi wateja makubwa na kisha kutimiza zaidi ya alivyoahidi. Kwenye ngazi hii mteja anashangazwa na thamani kubwa sana anayoipata, ambayo hakutegemea kuipata na wala hajawahi kuipata mahali pengine.
Kwa mteja kupata zaidi ya alivyotegemea, anakuwa na imani kubwa kwenye biashara, kitu kinachomfanya arudi tena kununua. Lakini pia hilo litamfanya mteja aisemee vizuri biashara kwa watu wengine, kitu kinachopelekea wateja wengi wapya kuijua biashara na kuvutiwa kuja kununua ili nao wapate thamani kubwa.
Biashara zinazoahidi makubwa na kutimiza kwa ukubwa, ambazo ni chache sana, huwa zinakuwa na wateja waaminifu na wanaodumu kwenye biashara. Wateja hao pia huwa ni watangazaji na wauzaji wazuri wa biashara hiyo, kwa sababu huwa hawakai kimya. Husema mazuri ya biashara kwa wengi zaidi, kitu kinachopelekea biashara kujulikana na wengi.
Hatua ya kuchukua; Kujitofautisha na wauzaji wengine wote, ahidi makubwa kisha yatimize kwa ukubwa. Makubwa ya kuahidi ni yale ambayo washindani wako hawayaahidi na wala hawawezi kuyatekeleza, ila wewe umejitoa kuhakikisha unayatekeleza ili wateja kupata thamani kubwa. Hapa unahakikisha kuna vitu ambavyo wateja wanaweza kuvipata kwako tu na siyo kwa wengine. Kisha piga kelele kubwa kwenye hilo, ahidi mara zote na timiza kwa ukubwa. Kwa kufanya hivyo, utaweza kujenga imani kwa wateja na kufanya mauzo makubwa.
SOMA; Igiza Mpaka Iwe Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Kuahidi Makubwa Na Kutimiza Kwa Ukubwa.
Katika kufanyia kazi dhana ya kuahidi makubwa na kutimiza kwa ukubwa, zingatia yafuatayo ili kupata matokeo mazuri.
1. Kuwa na ahadi kubwa ambayo inaitofautisha biashara yako na washindani. Hii ni ahadi ya kitu cha kipekee ambacho wateja wanaweza kukipata kwenye biashara yako ila hawawezi kukipata mahali pengine popote.
2. Ahadi hiyo kubwa ielezwe kwenye kelele zote ambazo biashara inapiga. Kwenye kutangaza na kufikia wateja wengi wapya, ahadi kubwa inapaswa kuwa ndiyo ujumbe mkuu unaokwenda kwa wateja.
3. Kila wakati kuwa na vitu vya kuwashangaza wateja. Hapa ndipo unawapa vitu ambavyo hawakutegemea kabisa kupata. Kuwa mbunifu na badilika badilika kila wakati ili usizoeleke. Wafanye wateja warudi kununua wakiwa na shauku ya kutaka kujua nini cha tofauti watakachopata.
4. Tumia shuhuda za wale ambao hawakuamini ahadi kubwa waliyosikia, lakini wakapata zaidi ya walivyotegemea. Unapotoa ahadi kubwa, wateja wengi watajiambia ni kawaida kwa wauzaji kuahidi lakini huwa hawatimizi. Utaweza kuvunja hilo kwa kuwa na shuhuda za wateja ambao nao walikuwa wanafikiria hivyo, lakini walipojaribu wakaishia kupata zaidi ya walivyotegemea. Uzuri ni wateja huwa tayari kutoa shuhuda za aina hiyo pale wanapopata makubwa kuliko walivyotegemea. Hivyo ahidi makubwa, timiza kwa ukubwa kisha waombe wateja wakupe shuhuda zao na uzitumie pale wateja wengine wanapokuwa na wasiwasi juu ya ahadi kubwa unayotoa.
5. Fanya kila namna utimize uliyoahidi, usiwe mtu wa kutoa sababu au visingizio. Unaweza kuahidi, lakini ikatokea hali inayokukwamisha kutekeleza uliyoahidi. Unapokutana na hali kama hizo, ni bora kuingia gharama kutekeleza uliyoahidi kuliko kutoa sababu na visingizio. Kwa sababu hata kama sababu ni za kweli, kushindwa kutimiza kunaondoa imani ambayo unataka wateja wawe nayo kwako. Ukishaahidi, hakikisha unatimiza, hata kama ni kwa gharama.
Kuahidi makubwa na kutekeleza kwa ukubwa ndiyo njia ya uhakika ya kujitofautisha na washindani kwenye biashara. Hakikisha unakuwa na kitu kikubwa unachowaahidi wateja, ambacho hawawezi kukipata kwa wengine. Nenda hatua ya ziada kwenye kutekeleza ahadi hiyo ili upate ushuhuda mzuri wa wateja na kuutumia kuwafikia na kuwashawishi wengi zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
