3535; Tatizo siyo mawazo, bali hatua.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanahangaika sana na mawazo mapya ya kupiga hatua na kufanikiwa kwenye maisha yao.
Na kwa bahati mbaya sana, mawazo mapya ni mengi sana.
Mengi kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kuyafanyia kazi mawazo yote mazuri anayokuwa nayo.
Tena kitendo cha mtu kukimbizana na mawazo mapya kila wakati, kinakuwa kikwazo kwa mtu kupiga hatua kubwa anazotaka.
Kama kila wakati kuna wazo jipya unalokimbizana nalo, hupati muda na umakini wa kutosha kufanyia kazi wazo moja mpaka likupe matokeo makubwa unayoyataka.
Tunachoweza kusema ni kwamba watu wanashindwa siyo kwa sababu wamekosa mawazo mazuri.
Bali wengi wanashindwa kwa sababu ya kuwa na mawazo mengi.
Kwa wingi wa mawazo wanayokuwa nayo, wanashindwa kufanyia wazo moja kazi kwa uhakika mpaka lilete matokeo wanayotaka.
Huwa inakuwa hivi;
1. Mtu anapata wazo fulani zuri sana, ambalo linaonekana kuweza kuleta mapinduzi makubwa kwake.
2. Anaanza kulifanyia kazi kwa shauku kwa kuamini ndiyo litaleta mapinduzi makubwa kwake.
3. Wakati anaendelea, anapata wazo jingine linaloonekana kuwa bora kuliko la awali.
4. Anaona hilo ndiyo la kuanza kufanyia kazi mara moja na kuacha lile alilokuwa anafanyia kazi.
5. Mzunguko unajirudia tena.
Ni huo mzunguko ndiyo umekuwa unafanya watu kujikuta wameganda pale pale au wanarudi nyuma kwenye safari yao ya mafanikio.
Namna pekee ya kuvuka hilo ni kutambua kwamba kitakachokukwamisha kufanikiwa siyo kukosa mawazo mazuri, bali kukosa utekelezaji mzuri.
Mawazo mazuri tayari unayo, unachokosa ni nidhamu ya kuchagua wazo moja na kulifanyia kazi kwa uhakika mpaka likupe matokeo makubwa unayoyataka.
Na hilo ndiyo unalopaswa kulisimamia sana kwenye maisha yako.
Chagua wazo moja ambalo utalipa muda, nguvu, akili na umakini wako wote kwenye kulitekeleza.
Mengine yote yapumzishe kwanza mpaka utekeleze wazo moja kwa uhakika.
Fanya hivyo, kuwa mtekelezaji mzuri na utafanikiwa.
Vipi kama utapata wazo la fursa nzuri ambayo haiwezi kujirudia tena?
Moja, hakuna fursa nzuri ambayo haiwezi kujirudia tena, hivyo endelea na wazo lako kuu, huku ukipumzisha fursa hiyo mpya uliyoipata.
Mbili, weka wazo hilo jipya kwenye orodha ya mawazo utakayokuja kufanyia kazi huko mbeleni.
Kwa sasa endelea na wazo ambalo tayari umechagua kulifanyia kazi.
Ukiweza kuvuka huo ushawishi wa kuhangaika na mawazo mapya kila wakati na ukawa na utulivu mkubwa kwenye kutekeleza wazo moja mpaka likupe matokeo, utafanya makubwa.
Mara zote jikumbushe hili; hushindwi kwa kukosa mawazo mazuri, bali unashindwa kwa kukosa utekelezaji mzuri. Chagua kuwa mtekelezaji wa uhakika na utaweza kufanya makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe