3539; Manunuzi ya Kimafanikio.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye ukurasa wa 3538 uliopita, tulijifunza kuhusu Mauzo ya Kimafanikio.
Tuliona jinsi kile ambacho watu wanauza ndiyo kinaamua mafanikio wanayopata, au kukosa.
Kwenye ukurasa huu tunaangalia upande wa pili wa shilingi, ambao ni Manunuzi ya Kimafanikio. Hapa tutaangalia yale ambayo watu wanayapa kipaumbele kwenye matumizi ya fedha zao na jinsi yanavyoathiri mafanikio yao.
Matajiri wananunua muda.
Wanajua jinsi muda ulivyo rasilimali muhimu na adimu.
Wanajua wakipoteza fedha, wanaweza kupata nyingine. Ila wakipoteza muda hawaupati tena.
Wanajua ili wapate mafanikio zaidi, lazima wawe na muda zaidi.
Hivyo kila wanapopata fedha, wanakazana kununua muda zaidi.
Wanafanya hivyo kwa kuajiri watu na kutumia mifumo inayowapa muda mwingi zaidi.
Kwa kununua muda, wanakuwa wamefanya uwekezaji sahihi, ambao unawalipa zaidi baadaye.
Masikini wananunua vitu.
Wanapenda kutumia vitu hivyo wanapopata fedha wanakimbilia kuvinunua.
Wakiona watu wana vitu vipya, wanajiambia na wao lazima wavipate.
Wananunua vitu ambavyo hata hawana uhitaji navyo, ila tu wanataka kuonekana na wao wanavyo.
Kwa kutumia fedha zao kununua vitu, masikini wanazidi kuzama kwenye umasikini.
Hiyo ni kwa sababu fedha ikishatumika haiwezi tena kumnufaisha aliyeitumia.
Matumizi siyo uwekezaji, bali ni shimo linalomeza fedha.
Mbaya zaidi ni pale matumizi yanapokuwa ya kukopa, hapo yanakuwa gereza kabisa ambalo linachukua uhuru wa mtu.
Watu wenye ndoto kubwa wananunua ujuzi.
Wanajua kilichosimama kati yao na ndoto zao kubwa ni ujuzi waliokosa. Hivyo wanaweka kipaumbele kwenye kujijengea ujuzi ambao utawafikisha kwenye ndoto hizo.
Wenye ndoto za kufanikiwa kwenye biashara wananunua ujuzi wa masoko, mauzo, fedha, usimamizi na ujuzi mwingine.
Hawa huwa tayari kulipa fedha kujifunza yale ambayo yanawafikisha kwenye ndoto zao.
Uwekezaji kwenye ujuzi ni uwekezaji ambao unalipa sana, kwa sababu ujuzi unaopatikana unakuza zaidi kipato.
Wavivu na wazembe wananunua usumbufu.
Kwa uvivu wao hupenda vitu vya kujifurahisha tu. Wanatumia fedha zao kupata raha ambazo huwa ni za muda mfupi tu.
Usumbufu ambao wavivu na wazembe hupenda kujifurahisha nao ni vilevi vya aina mbalimbali na kufuatilia mambo yasiyo na manufaa kwao, kupitia mitandao ya kijamii na michezo mbalimbali.
Watatumia gharama kwenye huo usumbufu unaowafurahisha na kuishia kukwama kwenye maisha yao.
Rafiki, wewe ni manunuzi gani ambayo huwa unafanya na kipato chako?
Angalia kwa vipato vyako vya nyuma, ni wapi huwa unavipeleka zaidi?
Baada ya kujifunza hapa manunuzi ya kimafanikio, ni manunuzi gani utakayoyapa kipaumbele zaidi ili upate mafanikio unayoyataka?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe