Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Mafanikio kwenye maisha yanatokana na yale ambayo mtu amefanya na siyo kupanga pekee. Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi licha ya kuwa na malengo makubwa na mipango mizuri. Kinachokuwa kinawakwamisha ni kutokuchukua hatua ya kufanyia kazi malengo na mipango waliyonayo.
Ili mtu kupata matokeo makubwa, ambayo hajawahi kuyapata kwenye maisha yake, lazima afanye vitu vikubwa na vya tofauti, ambavyo hajawahi kufanya kwenye maisha yake. Hapo ndipo penye changamoto na vikwazo vinavyowazuia watu kufanya makubwa.
Watu wanakuwa vizuri sana kwenye kupanga nini wanataka kufanya, lakini inapofika wakati wa kuchukua hatua ili kuwa vile wanavyopanga, wanakwama. Wanakwama kwa sababu hawafikii hatua ya kuanza kufanya yale wanayopaswa kufanya.
Kila wakati wa kuanza kufanya unapofika, wanaahirisha na kusema wataanza wakati mwingine. Kinachowafanya watu waahirishe yale waliyopanga ni kujiona bado hawajawa tayari kuanza. Wanajiona hawajawa tayari kwa sababu kuna vitu ambavyo wanaona wanapaswa kuwa navyo au kuvifikia ndiyo waweze kuanza.
Kwa maneno mengine, watu wanajiona hawajakamilika kuweza kuanza kile wanachopaswa kufanya ili wapate matokeo makubwa na ya tofauti. Kuahirisha kufanya kwa kuona mtu hujawa tayari ingeweza kuonekana ni jambo la busara, kama mtu angechukua hatua ya kufanya maandalizi sahihi yanayohitajika ili awe tayari kuanza.
Lakini hilo siyo linalotokea, kwani mtu anaendelea na maisha yake kama kawaida, bila ya kufanyia kazi mambo ambayo yangemfanya awe tayari kuanza.
Kumbe basi kinachokuwa kinawakwamisha watu kufanya yale wanayopaswa kufanya ili kufanikiwa siyo kukosa ukamilifu, bali ni kukosa utayari wa kuanza. Hivyo basi, kama mtu unataka kufanya unayopaswa na kupata matokeo ya tofauti, lazima uwe tayari kuanza pale unapotaka kuanza, bila kujali kama umekamilika au la.
Yaani hupaswi kusubiri ukamilifu ili kuanza kufanya, badala yake unapaswa kuanza kufanya kama ulivyopanga, kisha kwenda ukiboresha kulingana na matokeo unayoyapata.
Njia ya uhakika ya kufanya makubwa kwenye maisha na mauzo siyo mtu kusubiri mpaka ukamilike ndiyo uanze, badala yake kuanza vile ulivyo na kwenda ukiboresha kulingana na matokeo unayoyapata.

JINSI YA KUTUMIA DHANA YA KUTOSUBIRI UKAMILIFU KUWA MUUZAJI BORA NA KUFANYA MAUZO MAKUBWA.
Kama ambavyo tumeona, kusubiri mpaka uone umekamilika ndiyo uanze kufanya, kamwe huwezi kuanza. Kwa sababu kila wakati kuna kitu ambacho utaona hujakijua vizuri. Kutumia dhana ya kutosubiri ukamilifu kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, zingatia yafuatayo;
1. Tayari Unajua Ya Kutosha Kuanza.
Mambo ya mtu kujua ni mengi sana, ambayo hakuna mtu anaweza kujua yote. Pale mtu unapolinganisha unayojua na unayopaswa kujua, unaona wazi kwamba bado una safari ndefu kwenye kujua. Lakini hilo halipaswi kukukwamisha kwa sababu yale unayojua tayari yanakutosha kuanza kufanya. Hupaswi kusubiri mpaka ujue kila kitu ndiyo uanze, kwani hakuna wakati utajua kila kitu. Tumia yale unayojua kuanza kufanya na mengine utajifunza kadiri unavyoendelea kufanya.
Hatua; Ukishapanga makubwa ya kufanya, anza kufanya kwa kutumia yale ambayo tayari unajua, usisubiri mpaka ujue zaidi. Anza kufanya na utaendelea kujifunza wakati unafanya.
2. Kilicho Muhimu Ni Kuwasaidia Wateja.
Kwenye mauzo, wateja hawajali sana unajua nini, bali unawasaidiaje. Wateja hawakulipi kwa unachojua, bali wanakulipa kwa thamani unayowapatia. Unaweza kukwama kuanza kwa sababu unaona kuna vitu hujajua, wakati kwa ambayo unayajua tayari ungeweza kuwasaidia sana wateja unaowalenga. Hivyo wewe usiangalie unajua au hujui nini, bali angalia ni kitu gani unaweza kuwasaidia wengine, ni thamani gani unaweza kuwapa. Ukianzia hapo, unakuwa na cha kufanya hata kama unajiona hujawa tayari.
Hatua; Mara zote jiulize ni kitu gani unaweza kuwasaidia wateja kufanya, thamani gani unaweza kuwaongezea na fanya hivyo. Una kitu unachoweza kuwasaidia nacho wateja, kitumie hicho.
3. Ni Rahisi Kuendelea Kufanya Kuliko Kuanza.
Kanuni ya mwendo inasema kitu ni rahisi kuendelea kwenye hali ambayo kipo kuliko kubadilika. Hivyo kitu kilichosimama ni rahisi kuendelea kusimama wakati kilichopo kwenye mwendo ni rahisi kuendelea na mwendo. Kabla hujaanza, huwa ni rahisi kubaki kwenye kutokuanza kuliko kuanza kufanya. Kadhalika ukishaanza kufanya, ni rahisi kuendelea kufanya kuliko kuacha. Jua kwamba kinachokufanya ujione hujawa tayari ni vile hujaanza, jilazimishe kuanza na itakuwa rahisi kwako kuendelea kufanya.
Hatua; Kila unalopanga kufanya, jitahidi uanze tu kufanya hata kama unajiona hujawa tayari. Ukianza kufanya ni rahisi kuendelea kufanya, anza hata kama unajiona bado kabisa.
SOMA; Ahidi Makubwa Na Kuyatimiza Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
4. Huwezi Kuboresha Sifuri.
Kinachofanya kusubiri ukamilifu ndiyo mtu aanze kiwe kikwazo ni kutokuanza kabisa hakuna kitu mtu anajifunza. Kwa sababu hakuna ambacho mtu amefanya, hakuna anachoweza kuboresha. Ni bora mtu kufanya na kukosea kuliko kutokufanya kabisa. Kwa sababu ukiwa na ulichokosea unaweza kukiboresha na kuleta matokeo mazuri. Lakini ukiwa hujafanya kabisa, huna cha kuboresha na hivyo kubaki chini ambapo mtu unaanzia.
Hatua; Kila unapojiona hujawa tayari kuanza kwa sababu utakosea, jua ni bora ukosee kwa sababu utakuwa na kitu cha kurekebisha kuliko kutokuanza kabisa. Utaweza kujifunza kwenye yale uliyokosea na siyo ambayo hujayafanya kabisa.
5. Kushindwa Ni Kutokufanya Kabisa.
Hofu ya kushindwa imekuwa sababu ya watu kusubiri ukamilifu ndiyo waanze. Na kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa hawafikii ukamilifu huo. Hilo limekuwa linapelekea wasiweze kuanza kabisa. Ili uweze kuanza, badili maana yako ya kushindwa. Kufanya na ukakosea siyo kushindwa, bali kutokufanya kabisa ndiyo kushindwa. Ukifanya na ukakosea, ni ushindi, kwa sababu umefanya na unajua wapi pa kurekebisha. Kutokufanya kabisa ndiyo kukosea, kwa sababu hujui wapi pa kurekebisha.
Hatua; Badili maana yako ya kushindwa, usichukulie kukosea kama kushindwa, bali chukulia kutokufanya kabisa ndiyo kushindwa. Kama hutaki kushindwa, anza kufanya hata kama unajiona hujawa tayari.
Kwa kuwa hakuna wakati mtu utajiona umekamilika kwa ajili ya kuanza kitu, unapaswa kuanza kabla hata hujawa tayari. Jiamini tayari una ujuzi na uzoefu wa kutosha kuwasaidia watu wengine kwa kuwapa thamani kubwa. Na hata kama utakosea kwenye kufanya, unakuwa hujashindwa, bali umejifunza kipi hakifanyi kazi. Kwa kuboresha hicho ambacho hakifanyi kazi, unajiweka kwenye nafasi ya kupata mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.