Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Wakati naanza kujifunza kwenye tasnia hii ya maendeleo binafsi, fedha na biashara, nilikutana na dhana moja ambayo sikuwahi kuijua kabisa. Dhana hiyo ilitoka kwa Peter Drucker, aliyekuwa mshauri mkubwa kwenye eneo la usimamizi wa biashara. Drucker alikuwa anasema; “Dhumuni la biashara siyo kutengeneza faida, bali kutengeneza na kutunza mteja.”

Nakumbuka nilijifunza hili wakati nafanya utafiti wa kuandaa masomo ya mafunzo niliyokuwa naenda kutoa kwa wafanyakazi wa biashara fulani, hiyo ilikuwa mwaka 2014. Nikaona hiyo ni dhana muhimu sana na kuijumuisha kwenye masomo. Ilichukua zaidi ya nusu saa tukibishana kwenye dhana hiyo, kwa sababu watu wote waliamini dhumuni la biashara ni kutengeneza faida.

Kwa sababu ilikuwa dhana geni kwangu pia, ilichukua muda kuweza kuielezea kwa namna ambavyo wengi wangeweza kuielewa na kuona inarudije kwenye kutengeneza faida.

Kama bado na wewe unashangaa iweje dhumuni la biashara iwe ni kutengeneza wateja na siyo faida, nitaeleza kwa kifupi hapa ili twende sawa. Ni kweli, biashara haiwezi kwenda bila faida. Na faida haiwezi kuwepo bila mauzo. Na mauzo hayatafanyika kama hakuna wateja. Kwa hiyo basi, unaona hapo, ukianza na wateja, ni rahisi kupata faida. Lakini ukianza na faida, utakwama, kwa sababu utakuwa huna kile kinacholeta hiyo faida.

Kwenye barua hii tunaenda kujenga kutokea hapo, kwenye dhumuni la biashara kuwa kutengeneza na kutunza wateja. Halafu tutaona aina ya wateja tunaowahitaji ili tuweze kupata faida kubwa zaidi na itakayotupa utajiri mkubwa kadiri ya tunavyotaka.

1. Wengi Wanaingia Kwenye Biashara Kinyume.

Watu wengi wanaingia kwenye biashara kwa sababu wamepata wazo zuri au wana bidhaa au huduma wanayoona ni bora sana na wanaweza kuiuza. Hizo ni njia sahihi za kuingia kwenye biashara, kwa sababu lazima uwe na thamani ambayo unaitoa kwenye soko.

Na kama una bidhaa au huduma nzuri, inayotatua tatizo ambalo lipo, utaweza kuuza. Na pia utaweza kujenga biashara, inayoweza kuwa na mafanikio, kadiri ya unavyoweza kuuza bidhaa au huduma uliyonayo kwa wengi.

Lakini kuanza na wazo, bidhaa au huduma haiwezi kukupa utajiri mkubwa sana kupitia biashara. Utapata matokeo, lakini siyo ambayo ni makubwa sana yanayoweza kupatikana.

Kuingia kwenye biashara kwa kuanza na thamani ni kuingia kinyume. Ndiyo unakuwa umeingia, lakini si kwa mlango ambao utakupa matokeo makubwa sana. Na hili halina tatizo, kama lengo lako ni kuwa kwenye biashara inayokufanya uridhike.

Lakini kama lengo lako ni kuwa kwenye biashara itakayokupa utajiri mkubwa, ubilionea na utrilionea, kuanza na thamani ni kujikwamisha kufikia malengo hayo makubwa.

Njia sahihi ya kuingia biashara ambayo itakupa utajiri mkubwa sana ni kuanza na wateja. Ni kuangalia wateja ambao wapo kwa wingi sana, na kujua nini ambacho wanakihitaji sana na kuwapatia hicho. Kadiri biashara inavyokuwa na wateja wengi na ambao wanaitegemea kwenye kufanya maisha yao yakamilike, ndivyo inavyofanya mauzo makubwa na kutengeneza faida kubwa pia.

Biashara zote kubwa na zilizotengeneza mabilionea, zina wateja wengi ambao wanazitegemea kwenye maisha yao ya kila siku. Bidhaa au huduma zinazotolewa zinaweza kuwa za kawaida kabisa, lakini wateja ndiyo wanaoleta tofauti.

Labda nikuulize swali ambalo litakufungua zaidi kwenye hili;

Ukitaka kuvua samaki, unaenda wapi? Ni lazima uende kwenye maji.

Na hata ukienda kwenye maji, utachagua eneo gani? Ni lazima uchague eneo ambalo samaki wanapatikana kwa wingi.

Na hata ukiwa kwenye eneo lenye samaki wengi, utawakamataje? Lazima uwe na ndoano au wavu na kuwe na chambo ya kuwanasa samaki hao.

Hilo hapo ndiyo somo kamili la kujenga biashara itakayokupa utajiri mkubwa. Unaanza na eneo lenye samaki wengi na unakuwa na chambo na kitu cha kuwanasa. Samaki ni wateja, chambo ni bidhaa/huduma na biashara ni ndoano au wavu unaowanasa kwa muda mrefu.

Huwezi kujenga biashara inayokupa utajiri mkubwa kwa kuwa na bidhaa au huduma bora pekee. Ni lazima uwe na wateja, ambao ni wengi na wanaojirudia rudia.

Huwezi kujenga biashara inayokupa utajiri kwa kuwa na wateja wanaonunua mara moja na hawarudi tena au wananunua mara chache chache. Biashara inayokupa utajiri mkubwa ni ile ambayo mteja akishanasa, amenasa, ananunua kwa maisha yake yote.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekuongoza jinsi ya kujenga wateja wa biashara ambao wanaitegemea na kuiwezesha biashara yako kukupa utajiri mkubwa.

Soma barua hiyo hapa; #BZK070; Kujenga Utajiri Mkubwa Kupitia Biashara, Unahitaji Wateja Wa Aina Hii