Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kutengeneza wateja wapya ni wajibu namba moja wa kila biashara. Kwani ni kupitia wateja hao wapya ndiyo biashara inaweza kupata ukuaji mkubwa kadiri ya inavyotaka.

Kuwashawishi wateja kununua kwa mara ya kwanza kwenye biashara siyo zoezi rahisi. Hiyo ni kwa sababu wateja hao wanakuwa hawana imani na biashara, kwa sababu hawaijui na hawajawahi kununua.

Njia bora ya kuwafanya wateja waiamini biashara ni kuiona na kuisikia mara kwa mara. Ndiyo maana matangazo ya biashara huwa ni muhimu, kwani kadiri mtu anavyoona na kusikia kitu mara kwa mara, ndivyo anavyokizoea na kuwa tayari kukitumia.

Ukiacha matangazo ya aina mbalimbali, ambayo biashara huwa zinafanya ili kuwafikia wateja wengi, zipo njia nyingine za kuiwezesha biashara kuwafikia wateja, tena kwa gharama nafuu kuliko matangazo.

Moja ya njia hizo ni kutumia vifungashio vya bidhaa ambazo wateja wananunua.

Vifungashio ambavyo biashara inawapa navyo wateja bidhaa na vitu vingine, ni njia nzuri ya kuendelea kuwafanya wateja hao na wengine wapya kujua kuhusu biashara na kuendelea kuifikiria kwa muda mrefu zaidi.

AINA ZA VIFUNGASHIO VYA KUTUMIA KUWAFIKIA WATEJA WENGI ZAIDI.

Kuna vifungashio vya aina mbalimbali ambavyo biashara huwa zinatumia kuwapa wateja bidhaa na vitu vingine. Chochote ambacho mteja anapata kutoka kwenye biashara ni fursa ya biashara kuendelea kuwa mbele ya mteja. Hapa kuna aina za vifungashio ambavyo vinaweza kutumiwa kuwafikia wateja wengi zaidi.

1. Vifungashio vya bidhaa za biashara.

Kwa biashara ambayo inauza bidhaa kwa wateja, ambazo zinawekwa kwenye vifungashio, hiyo ni fursa kwa biashara kutumia vifungashio hivyo kama sehemu ya matangazo na kufikia wateja wengi zaidi. Vifungashio hivyo vinaweza kuwa bahasha, mifuko, maboksi, makopo na vingine vingi kulingana na aina ya biashara.

Hatua; Kama biashara inawapa wateja bidhaa zake kwa kutumia vifungashio, havipaswi kuwa tu vifungashio vya kawaida, bali viwe vifungashio maalumu vinavyoendelea kuitangaza biashara kwa wengi zaidi.

2. Vifungashio vya bidhaa za biashara nyingine.

Matumizi ya vifungashio kutangaza biashara hayaishii tu kwa biashara husika, bali kuna fursa ya kutumia bishara nyingine kufanikisha hilo. Hapa biashara inashirikiana na biashara nyingine kwa kuipa vifungashio ambavyo biashara hiyo itatumia kwa wateja wake. Biashara inayotoa vifungashio inapata fursa ya kufikia wateja wengi, huku biashara inayopokea vifungashio ikipunguza gharama za kupata vifungashio.

Hatua; Angalia biashara ambazo siyo washindani wa moja kwa moja, ila zinalenga aina ya wateja ambao biashara yako inalenga. Zile ambazo hazina utaratibu wa kutumia vifungashio kutangaza, ingia nao makubaliano ya kuwapa vifungashio bure, ambavyo vina taarifa za biashara yako. Hilo likikubaliwa biashara inakuwa imeweza kuwafikia wateja hao ambao huenda hawakuwa wanaijua.

3. Mbadala wa vifungashio kwenye biashara za huduma.

Kwa biashara ambazo haziuzi bidhaa, yaani zile ambazo zinatoa huduma, huwa hazina vifungashio kwa ajili ya kile kinachouzwa. Lakini hilo halimaanishi kwamba njia hii ya kutumia vifungashio kuwafikia wengi zaidi haiwezi kufanyiwa kazi. Kuna vitu vingine ambavyo biashara inafanya kwenye kuwafikia wateja ambao inawahudumia. Mfano ni kuwatumia taarifa mbalimbali kwa jumbe na barua. Hapo biashara inaweza kutumia kama njia ya kutangaza. Mfano pale biashara inapotuma taarifa ya malipo yanayopaswa kufanya, karatasi inayokuwa na ujumbe, pamoja na bahasha inayobeba karatasi hiyo inaweza kutumika kuitangaza zaidi biashara.

Hatua; Tumia vitu vingine ambavyo biashara inavitumia kuwafikia wateja hata kama haiuzi bidhaa, kama bahasha za kutumia jumbe mbalimbali ili kuwafikia wateja wengi zaidi.

SOMA; Tumia Ushirikiano Wa Kibiashara Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

MAMBO MUHIMU KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA VIFUNGASHIO KUFIKIA WATEJA WENGI.

Kama ambavyo tumeona, vifungashio na vitu vingine ambavyo wateja wanapewa, vina nguvu ya kuwafikia watu wengi zaidi. Ili hilo likamilike na kuwa na tija, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa;

1. Vifungashio viwe imara ili kuweza kutumika zaidi ya mara moja.

Kifungashio kinachotumika mara moja na kutupwa hakiwezi kufanikisha mpango wa kufikia wengi zaidi. Hivyo vifungashio vinapaswa kuwa imara kiasi cha kuweza kutumika zaidi ya mara moja. Hilo litaongeza fursa ya kifungashio hicho kuwafikia watu wengi zaidi.

2. Mwonekano mzuri wa kuvutia watu kutumia.

Vifungashio vinapaswa kuwa na mwonekano mzuri na unaowavutia watu kuvitumia. Watu huwa wanapenda na kuvutiwa na vitu vizuri, hivyo vifungashio vinapaswa kuwa na muundo mzuri. Pia jina la biashara linapaswa kujengwa kwa ukubwa na uaminifu kiasi cha wateja kutaka kuonekana wakiwa na kitu chenye nembo ya biashara hiyo.

3. Maudhui yanayosomeka na yenye ushawishi.

Maelezo yanayowekwa kwenye vifungashio yanapaswa kusomeka vizuri na kuwa na ushawishi mkubwa. Hilo halimaanishi yawe ni maandishi mengi, bali yanapaswa kuwa ya msingi kumtosheleza mtu kupata taarifa na kushawishika kuchukua hatua.

4. Mawasiliano yanayoonekana hata kwa mbali.

Kitu kikubwa na muhimu ambacho hakipaswi kukosekana kwenye kila kifungashio ni mawasiliano. Lengo la kifungashio kuwa na taarifa za biashara ni kuwapa watu hatua za kuchukua ili kunufaika. Hatua hizo zinachukuliwa kupitia mawasiliano yanayokuwa yamewekwa.

5. Kuwa mbele ya mteja mara zote.

Kutengeneza wateja wapya na kuwafuatilia wateja, vitu viwili muhimu sana kwenye mauzo ni vitu vinavyokutaka kima mara kuwa mbele ya wateja wako. Wanapaswa kukusikia, kukuona na kukufikiria muda wote. Huu  ni wajibu muhimu ambao kila muuzaji na mfanyabiashara anapaswa kuuzingatia. Hivyo kila wakati unapaswa kuangalia ni namna gani unaweza kufikia wengi zaidi na chukua hatua.

Chochote kinachotoka kwenye biashara na kwenda kwa mteja, kinapaswa kuwa kwenye hali ambayo kitatumika kuwafikia wengi zaidi. Vifungashio ni njia nzuri ya kuitangaza biashara pale vinapokuwa imara na kuwa na mwonekano wa kuvutia. Tumia vifungashio kwenye bidhaa na huduma za biashara yako na biashara za wengine ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.