3540; Nipe nikupe haijawahi kuchuja.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Iwe tunataka au hatutaki, mahusiano ya binadamu yamejengwa kwenye msingi wa nipe nikupe.
Nikune nikukune ndiyo kitu pekee kinafanya dunia iende.

Tunapenda kuzunguka zunguka kwenye mengi sana, lakini tunakwepa ukweli ulio mbele ya macho yetu.
Ukweli huo ni kwamba hakuna binadamu anayetoa kitu chochote bila ya kutegemea kupata kitu fulani.

Watu wanatoa pale wanapojua kuna kitu wanapata. Na hiyo imekuwa hivyo mara zote.

Wale wanaotaka kushawishi wapate wanachotaka, huwa wanaanza kwa kutoa. Wanapotoa wanatengeneza hali ya deni kwa wale wanaopokea, ambapo wanajiona wakiwajibika kulipa.

Mara nyingi anachotoa mtu na anachopokea vinaweza visiendane.
Lakini hakuna anayetoa na akabaki hajapokea chochote.

Hata mtu anapotoa msaada kwa asiyejiweza kabisa, bado anategemea kupokea sifa na heshima.
Unaweza kusema mtu ametoa kwa moyo tu na hategemei chochote.

Ukitaka kujua hilo msaidie mtu kitu, ambacho unajua kabisa hawezi kukulipa, halafu asikushukuru kabisa.
Au akulaumu kwamba hujamsaidia vya kutosha.
Lazima hilo litakuuma sana.
Sasa kwa nini uumizwe kama uliamua tu kumsaidia mtu?

Jibu lipo wazi, unaumizwa kwa sababu ulisaidia ukitegeme kupokea kitu fulani.
Unapokikosa, unajisikia vibaya.

Nitachotaka tukumbushane hapa rafiki ni kimoja, wape watu sababu ya kukupa kile unachotaka.
Utafanya hivyo kwa;
1. Kuanza kuwapa vitu na wao kujiona wana deni la kukulipa.
2. Kuwafanya waamini kwamba kwa kukupa wewe unachotaka, nao watapata wanachotaka.

Ukiweza kusimamia hilo, umeweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Toa upokee zaidi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe

Print the following sentence in your brain with a bulldozer.

No human being gives anything out without expecting something in return.

This rule is absolute.

No exception.