Tunaishi kwenye zama ambazo msaada pekee unaoonekana wa maana ni msaada wa fedha. Siku hizi hata ushauri unaombwa na unachukuliwa kwa wenye fedha kwa kuaminika kwamba wao ndio wenye ushauri mzuri. Hata ule usemi wa msaada wa hali na mali umebaki kama usemi tu ila watu wanangalia mali kwanza ndio wachukue ama kutoa msaada hata wa mawazo.

  Haipaswi kuwa hivi, kila mtu anakitu anachoweza kumsaidia mwingine, ndio namaanisha hata wewe una vitu vingi sana unavyoweza kuwasaidia wanaokuzunguka na ukaleta mabadiliko makubwa hata kama huna hata shilingi elfu moja mfukoni mwako.

toa6

  Hivi hapa ni vitu vitatu ambavyo kila mtu anaweza kuvitoa kwa wengine, akabadili maisha yao na asipungukiwe na chochote hata kama atatoa mara elfu kwa siku.

   Kitu cha kwanza unachoweza kumsaidia yeyote ni neno. Neno lako ni muhimu sana kwa wengine, neno linaweza kuwa ushauri, kutia moyo na kupongeza.  

  Kila mtu anahitaji ushauri kwa jambo lolote analofanya, kila mtu anahitaji ushauri kwenye maisha yake ya kawaida. Kama una lolote unalojua juu ya kitu mtu anafanya, ushauri wako ni muhimu sana ili aweze kufikia malengo yake.

  Katika safari ya maisha kuna vikwazo vingi sana, kuna kupanda na kushuka na kuna kuanguka. Kama kuna watu wakututia moyo tunapokuwa kwenye nyakati ngumu ni msaada mkubwa sana kwetu. Mpe moyo mtu anaepitia matatizo, mpe moyo mtu anaekazana kufikia ndoto zake na kwa hakika utakuwa wa msaada sana kwenye maisha yake.

  Hakuna kitu kizuri kama pale unapopongezwa kwa jambo ulilotumia muda wako kulifanya. Pongezi zinakufanya utake kufanya zaidi na zaidi ili kutowaangusaha wanaokubali unachofanya. Mpongeze mtu anaefanya jambo fulani na ukalifurahia. Hutopoteza chochote kwa kumpongeza mtu kwa alichofanya na utakuwa umemsaidia sana kuweza kuwa mbunifu zaidi na kufanya kwa moyo zaidi.

  Kitu cha pili unachoweza kutoa kwa watu ni tabasamu. Unaweza kuona kama utani ila tabasamu lako ni muhimu sana kwa wanaokuzunguka. Toa tabasamu halisi popote ulipo, ongea na watu huku ukitabasamu, toa huduma zako ukiwa umejawa na tabasamu. Utajikuta unawavutia watu wengi na kuweza kubadili hali za watu. Kwa kuonesha sura ya kununa ama isiyo na tabasamu ni ujumbe tosha wa kuwafukuza watu wasikusogelee. Toa tabasamu na kama kuna utakachopoteza kwa kutabasamu nitafute nikulipe.

toa4toa5

  Kitu cha tatu unachoweza na unachotakiwa kutoa kwa watu ni shukrani. Mshukuru kila mtu anaefanya jambo lolote kukusaidia wewe ama jamii inayokuzunguka. Neno asante lina maajabu makubwa yanayoweza kubadili maisha ya watu. Unajisikiaje pale unapofanya kitu halafu watu wanakushukuru? unajiona na wewe ni wa muhimu na kuna kitu umebadili, hivyo basi washukuru wote wanaofanya jitihada fulani za kubadili maisha yako na ya wengine.

  Unapotoa vitu hivi ni vyema ukatoa kutoka moyoni na usifanye unafiki. Usimpngeze ama kumtia moyo kwa unafiki, ni rahisi sana mtu kukugundua unafanya unafiki na utampoteza mara moja.

  Ni vigumu sana kwa watu kutoa vitu hivi vitatu, jifunze kuanza kuvitoa na utabadili maisha yako na ya wanaokuzunguka. Unaweza kuanza kwa kuweka neno lolote kwenye comment hapo chini iwe ushauri, pongezi ama shukrani kwa yale unayoyasoma kwenye mtandao huu.