Tumefikia mahali ambapo ubora wa vitu unapimwa kwa thamani ya hela. Yaani kila kitu sasa hivi kinaangaliwa bei yake ndio watu wakithamini.

  Hii ndio imesababisha watu kuthamini zaidi fedha na vitu ambavyo fedha inaweza kununua. Baadhi ya binadamu wako radhi kufanya hata mambo ya hatari ili tu wapate fedha ili waweze kununua vile wanavyothamini.

vitu bora2

Kutokana na vitu vilivyobora kuwa bure basi watu hawavithamini na badala yake kuthamini vyenye thamani ya fedha. Watu tunatumia hovyo vitu tulivyopewa bure bila ya kujua kwamba ndio vitu bora zaidi maishani.

  Kutokana na thamani hii kubwa fedha iliyopewa, kila kitu kwenye maisha sasa kimewekewa bei ama kinapimwa kwa fedha. Hata mapenzi kwa sasa yanapimwa kwa fedha, wapo wanaodiriki kusema hapendwi mtu pale pochi yake. Ni wachache sana walio na mapenzi ya dhati na hawa ni wale waliokwisha elewa mipaka ya thamani ya fedha. 

  Fedha inaweza kununua vifuatavyo, starehe zote za dunia, mali za kifahari kama majumba, magari, madini mbalimbali na vitu vingine vyote watu wanavyoona vya thamani.

  Fedha haiwezi kununua vifuatavyo muda, maisha, upendo wa dhati, furaha ya kweli na amani ya nafsi

  Kati ya vitu ambavyo fedha inaweza kununua na ambavyo fedha haiwezi kununua vipi ni bora? Vitu ambavyo fedha haiwezi kununua ndio bora kwa sababu huwezi kuvipata baada ya kuvipoteza ila vitu ambavyo fedha inaweza kununua ni rahisi kuvipata hata ukivipoteza.

  Tuangalie vitu ambavyo fedha haiwezi kununua na jinsi tusivyovithamini.

  MUDA, kila mtu ana masaa 24 kwa siku, hakuna anaeweza kununua hata dakika moja ya ziada kwa siku. Muda ulioko nao ni bure kabisa na unaamua ni jinsi gani utakavyoutumia. Ila kwa vile hatuulipii basi tunaamua tu kuutumia hovyo.

  MAISHA, hakuna mtu alienunua uhai ama anaelipia uhai anaoishi hapa duniani. Kwa kuwa maisha ni ya bure basi baadhi yetu wameamua kuyatumia tu hovyo, watu wameshindwa kuona thamani ya maisha yao na kujiingiza kwenye mambo maovu.

  Upendo wa dhati na furaha ya kweli. Hivi navyo hakuna kiwango cha fedha kinachoweza kununua, upendo ama furaha inayotokana na fedha ni ya kinafiki na ukomo wake huwa pale fedha inapokwisha. Ila upendo na furaha ya kweli inakuwepo hata fedha isipokuwepo.

vitu bora

   Amani ya nafsi inapatikana kwa kutenda mema na kuishi vizuri na watu. Huwezi kununua amani ya nafsi. Nadhani sote tunajua maisha magumu ya watu waliopata utajiri kwa dhuluma wizi ama ufisadi. Ni vigumu sana kufurahia utajiri uliopatikana kwa njia hizi.

  Ni kitu kizuri kuwa na fedha nyingi ama kuwa tajiri, na ni kitu kizuri zaidi kuwa na vitu ambavyo fedha haiwezi kununua.

  Wakati tunaweka nguvu zetu kwenye kuusaka utajiri tusisahau pia kuvisaka vitu ambavyo fedha haiweza kununua. Hapo ndipo tunapoweza kuwa na maisha bora kwetu na kwa wanaotuzunguka.