Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Safari ya mafanikio kwenye maisha siyo njia iliyonyooka. Bali ina kona nyingi, pamoja na vilima na mabonde ya kila aina. Inapokuja kwenye mauzo, safari ndiyo ina changamoto nyingi zaidi kutokana na kukataliwa ambapo ni kwa wingi.
Ili kupata mafanikio makubwa kwenye eneo lolote la maisha yetu, tunapaswa kuwa tayari kuanza upya pale tunapopitia nyakati ngumu na zinazofanya mafanikio kuonekana magumu kuliko tulivyodhani.
Wajapani huwa wana methali inayosema; “Nana korobi ya oki” (ikimaanisha; anguka mara saba, inuka mara ya nane). Methali hiyo inaeleza vizuri dhana hii ya kuwa tayari kuanza upya kila unapoanguka kwenye safari ya mafanikio.
Kila mtu unayemwona amefanikiwa, alianzia chini kabisa, akiwa hana mafanikio aliyonayo sasa. Lakini zaidi ni kila aliyefanikiwa kuna kipindi alianguka na kuwa kwenye hali ambayo wengine waliona hawezi kuinuka tena.

Lakini kwa wao kujua kile walichotaka na kutokubali kutokukipata, waliweza kuamka na kuanza upya na baadaye kupata mafanikio makubwa kuliko yale waliyoyapoteza.
ILI KUWA TAYARI KUANZA UPYA NA KUWA MUUZAJI BORA ANAYEFANYA MAUZO MAKUBWA, ZINGATIA YAFUATAYO.
1. Jua Mafanikio Ni Wewe Kupata Unachotaka.
Huwa ni rahisi kusahau maana halisi ya mafanikio kwako pale unapokuwa unapambana kufanikiwa. Ni rahisi kujikuta unaiga yale ambayo wengine wanafanya, ambayo hayaendani na kile unachotaka wewe. Hivyo ni muhimu kila mara kujikumbusha kwamba mafanikio ni wewe kupata kile unachotaka. Baada ya kujikumbusha hilo, unakuwa wajibu wako kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili kuyapata mafanikio.
Hatua; Kila mara jikumbushe nini hasa unachotaka ili upambane kukipata ambayo ndiyo mafanikio ya kweli kwako.
2. Jua Njia Haijanyooka, Utakutana Na Changamoto.
Hakuna njia ya mafanikio ambayo imenyooka, kwamba utapata kila unachotaka kwa urahisi. Utakutana na vikwazo na changamoto za kila aina kwenye safari yako ya mafanikio. Kila unapokutana na ugumu, jua siyo mwisho wa safari, bali ni sehemu ya safari. Tena ni sehemu muhimu inayokukomaza wewe ili uweze kuyafikia mafanikio kwa uhakika kama unavyotaka.
Hatua; Jikumbushe kwamba vikwazo na changamoto ni sehemu ya kawaida ya safari yako ya mafanikio. Unapokutana navyo usione huo ndiyo mwisho wa safari, bali jua unakomazwa kwenye safari yako.
3. Jua Hujakamilika, Utafanya Makosa Mengi.
Huwa tunadhani mafanikio ni ukamilifu, kutokufanya makosa kabisa. Lakini hilo siyo sahihi, hakuna mtu aliyekamilika, ambayo hafanyi makosa kabisa. Kukosea ni ubinadamu, kwa sababu wote hatujakamilika. Hata baada ya kupiga hatua fulani kwenye maisha yetu, haiondoi hali ya kukosea ambayo tayari ipo ndani yetu. Kujua hili kunatupa tahadhari ya kutokuwa na kiburi pale tunapopiga hatua kwa kudhani hatuwezi kukosea. Kinachofanya wale waliopiga hatua kidogo kuanguka sana huwa ni kiburi cha kudhani hawawezi kukosea. Ukijua utaendelea kufanya makosa, utaweza kuchukua hatua sahihi pale unapokuwa umekosea.
Hatua; Jikumbushe hujakamilika, bado utaendelea kufanya makosa. Hivyo kila wakati jitathmini kama unayofanya ni sahihi au umekosea. Kama umekosea chukua hatua sahihi ili kupata kile unachotaka.
SOMA; Kuwa Jasiri Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
4. Wajibu Wako Ni Kujifunza Kwenye Makosa Na Kutokuyarudia.
Ukweli kwamba hujakamilika na utakosea haikupi wewe tiketi ya kuwa mzembe ambaye mara zote unakosea. Wajibu wako ni kujifunza kwenye kila makosa unayofanya na kuhakikisha huyarudii makosa hayo. Ndiyo utakosea, lakini unapaswa kujifunza kilichosababisha makosa uliyofanya ili usirudie tena makosa hayo. Huwa wanasema upumbavu ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile, kisha kutegemea matokeo ya tofauti. Wewe usiwe mpumbavu, badala yake kuwa mwerevu na jifunze kutokana na makosa yako ili usiyarudie.
Hatua; Usifiche uzembe kwenye kivuli cha kutokuwa umekamilika, kila unapokosea jifunze nini kimepelekea ukosee kisha hakikisha hurudii tena makosa hayo. Unapaswa kuendelea kuwa bora kwa kila hatua unayopiga.
5. Jifunze Kwa Wengine Walioanguka Na Kusimama.
Wewe siyo wa kwanza kupita njia unayokuwa unapita, kuna wengi ambao wamepita njia hiyo na kuweza kupata kile walichotaka. Wapo watu wengi ambao walianguka, ila waliweza kusimama na kuendelea na hatimaye kufanikiwa. Hao ni watu unaopaswa kuwajua na kujifunza kutoka kwao ili na wewe uweze kuvuka nyakati hizo ukiwa imara. Pale unapojua kwamba kuna wengine walipitia hali kama yako na bado wakaweza kufanikiwa, inakupa moyo kwamba na wewe utafanikiwa.
Hatua; Chagua kuwa na watu wa mfano kwako, watu waliopitia magumu sana, lakini bado wakafanikiwa. Kila unapojikuta kwenye ugumu na kutaka kukata tamaa, waangalie watu hao ili upate nguvu ya kuendelea na safari.
6. Haijaisha Mpaka Imeisha.
Tunapokuwa tumepitia magumu kwa muda mrefu huwa tunaweza kuona mafanikio siyo kwa ajili yetu. Pale tunapojaribu kila kitu na tukashindwa, tunaweza kuona tumemaliza nafasi zetu za kufanikiwa. Lakini huo siyo ukweli, hakuna ambacho ni mwisho kwako kama bado uko hai. Huwa kuna kauli inasema; ‘Haijaisha mpaka imeisha.’ Hii ikiwa na maana kwamba kama bado upo hai, bado una nafasi ya kufanikiwa. Haijalishi umeshindwa mara ngapi, bado nafasi ya kufanikiwa ipo ndani yako kama bado unapumua. Kwa kujua hilo, kamwe hupaswi kukata tamaa na kuiacha safari yako ya kupata mafanikio unayotaka.
Hatua; Kila siku unayoamka ukiwa hai na mzima wa afya, shukuru kwa nafasi nyingine unayokuwa umeipata ya kwenda kupambania ndoto yako ya mafanikio. Kamwe usikate tamaa kama bado upo hai, hata kama unapitia magumu kiasi gani, kama bado upo hai, jua bado unayo nafasi ya kufanikiwa.
Mpango wako wa kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa ni mzuri na wenye uhakika kufikia. Lakini hautakuwa rahisi kwenye utekelezaji kama ilivyo kwenye kupanga. Ukiingia kwa kudhani itakuwa rahisi, utakwama na kukata tamaa haraka. Tambua mipango siyo matumizi, changamoto zipo na utakosea. Wajibu wako ni kuhakikisha unaendelea kung’ang’ana na safari mpaka upate unachotaka kwa kujifunza kutokana na makosa yako na safari ya wengine. Kama upo hai, bado ndoto zako zote zinawezekana, zipambanie bila ya kujali unakutana na nini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.