Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Zipo njia nyingi za kufikia wateja wapya na kuwashawishi kununua kwenye biashara yako. Popote ambapo wateja unaowalenga wapo, unapaswa kuhakikisha wanajua kuhusu biashara yako na kushawishika kununua kwako.

Moja ya njia unazoweza kuwafikia wateja wengi ni kutumia wapambe. Hawa wana nguvu ya kuwafikia watu wengi na kuwa na ushawishi mkubwa kwao kama watatumiwa vizuri.

Kwenye somo hili utakwenda kujifunza jinsi ya kutumia wapambe sahihi kwa biashara yako ili kufikia wateja wengi na kuwashawishi kununua.

Wapambe Ni Watu Gani?

Wapambe ni watu ambao wana watu wengi wanaowajua na wana ushawishi mkubwa kwao kwenye kufanya maamuzi ya aina fulani. Tofauti ya wapambe (affiliates) na mabalozi (ambasadors/influencers) ni mabalozi huwa wanawafanya watu wajue kuhusu uwepo wa kitu fulani, wakati wapambe wanawashawishi watu kuchukua hatua.

Kwa mfano biashara inaweza kuwa na mabalozi, ambao ni watu wenye ushawishi wanaoitangaza na kuielezea biashara. Kwa sababu watu hao wanakuwa wanajulikana na wengi, biashara pia inajulikana na wale wanaowafuata mabalozi hao.

Kwa wapambe hali ni tofauti kidogo, watu hao wenye ushawishi na kujulikana na wengi huwa wanawashawishi watu wao kufanya manunuzi kwenye biashara. Hiyo ni kwa sababu ni kupitia manunuzi ambayo watu wanayafanya ndiyo wapambe wananufaika.

Kunakuwa na makubaliano kati ya biashara na wapambe ambapo wale wanaowashawishi wanunue wanapokuja kununua, wapambe hao wanapata kamisheni kutokana na manunuzi hayo.

Wakati mabalozi wanalipwa kwa kuitangaza biashara, wapambe wanalipwa pale wateja waliowashawishi wanapofanya manunuzi.

Faida Za Kutumia Wapambe Kufikia Wateja.

Kutumia wapambe kufikia wateja wengi kuna faida nyingi, baadhi ya hizo ni;

1. Ushawishi ni mkubwa, kwa sababu malipo ya mpambe yanategemea mtu kununua. Hilo linawasukuma wawashawishi wateja kununua ili wapate malipo.

2. Gharama ni ndogo kwa biashara, kwa sababu mpambe halipwi mpaka mteja amenunua. Tofauti na njia nyingine za kutangaza biashara ambapo gharama zinalipwa hata kama wateja hawajanunua.

3. Uwezo wa kutumia wapambe wengi bila ya ukomo. Kwenye njia nyingine za kufikia wateja huwa kuna ukomo, hasa wa gharama au upatikanaji wa nafasi. Lakini kwa wapambe hakuna ukomo, unalipa pale mteja anaponunua na wanaoweza kuwa wapambe ni wengi.

Kwa faida hizi, kila biashara na kila muuzaji anapaswa kutumia wapambe kuwafikia wateja wengi zaidi.

Jinsi Ya Kuchagua Wapambe Sahihi Wa Biashara Yako.

Wanaoweza kuwa wapambe wa biashara yako ni wengi, lakini siyo wote wanakuwa sahihi kutumia. Hivyo ni muhimu kujua jinsi ya kuchagua kwa usahihi wapambe wa biashara yako ili waweze kuwa na tija. Kuchagua wapambe sahihi kwa biashara yako, zingatia haya;

1. Wapambe wawe wanajulikana na wengi. Hilo ni muhimu ili hata kama watu hawatanunua wawe wameijua biashara. Na kwa kuwa unawalipa wapambe kwa manunuzi, unakuwa umepata matangazo ya bure kwa kujulikana kwa watu hao ambao wapambe wanawajua.

2. Wapambe wawe na ushawishi mkubwa kwa wale wanaowajua. Mtu anaweza kujulikana na wengi, lakini bado asiwe na ushawishi mkubwa kwao. Ni muhimu wapambe unaowachagua wawe na ushawishi mkubwa kwa wale wanaowajua, ambapo wakiwashauri kitu wanachukua hatua. Ni kwa njia hiyo ndiyo wanaweza kuwashawishi watu wao kununua kwako.

3. Wapambe wawe wateja au watumiaji wa kile unachouza. Huwa ni vigumu kwa mtu kuwashawishi watu wengine kufanya kitu ambacho yeye mwenyewe hajafanya. Kwenye kuchagua wapambe, zingatia wale ambao ni wateja na watumiaji wa kile unachouza ili wawe mashahidi wa kwanza kwenye manufaa ya kitu hicho. Ni kupitia ushuhuda wao binafsi ndiyo wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Zingatia haya ya msingi kwenye kuchagua wapambe sahihi wa kuwatumia kufikia wateja wengi na kuwashawishi kununua.

SOMA; Tumia Vifungashio Vya Bidhaa Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

Makundi ya wapambe unaoweza kuwatumia kufikia wateja wengi.

Tumeona jinsi ya kuchagua wapambe wa kutumia ili kufikia wateja wengi. Kuna makundi mbalimbali ambapo ndani yake tunaweza kupata wapambe sahihi kutuwezesha kuwafikia wengi. Karibu ujifunze makundi hayo hapa ili uweze kuchukua hatua na kuwapata wapambe sahihi.

1. Wateja wako.

Wateja ulionao sasa kwenye biashara yako ni chanzo kizuri cha kupata wapambe ambao watakuletea wateja zaidi. Kwa kuwa tayari wananunua, wana imani fulani kwenye biashara yako. Kwa imani waliyonayo kwenye biashara yako, wanaweza kuwashawishi wengine nao wanunue. Kwa kuwa na mpango mzuri wa upambe unaweza kuwageuza kuwa chanzo cha wateja.

2. Wafanyabiashara wengine.

Wafanyabiashara wengine, ambao tayari wanawahudumia wateja unaowalenga wanaweza kuwa njia nzuri ya kupata wateja. Unachofanya ni kuingia makubaliano na wafanyabiashara hao kwamba wakileta wateja kwenye biashara yako kuna namna wananufaika.

3. Watoa maudhui.

Watu wanaotoa maudhui kwa njia mbalimbali, iwe ni kwa maandishi, sauti, picha na video huwa wanakuwa na wafuasi. Watoa maudhui huwa wanaaminika sana na wafuasi wao, hivyo husikilizwa. Kwa kuwajua watoa maudhui wenye wafuasi ambao ni wateja unaowalenga utaweza kuwatumia kama wapambe.

4. Watu wanaofikiwa na wengi mara kwa mara.

Kuna watu ambao huwa wanafikiwa na watu wengi mara kwa mara kutokana na nafasi zao au shughuli zao. Kwenye nafasi, viongozi mbalimbali huwa wanafikiwa na watu wengi. Kwenye shughuli, madereva wa usafiri wa kukodi, wenye migahawa na saluni huwa wanafikiwa na watu wengi. Wateja wa maeneo hayo huwa wanauliza sehemu wanazoweza kupata vitu vingine wanavyotaka. Kwa kushirikiana na watu hao wanaweza kuwa wanawaelekeza watu kwako pale wanapoulizia kile unachouza.

5. Watu wenye ushawishi.

Watu wenye ushawishi, ambao wana wafuasi wengi, iwe ni kwenye mitandao au nje ya mitandao unaweza kuwatumia kama wapambe. Badala ya kuwalipa kukutangaza, unawapa mpango wa malipo kwa kila manunuzi ambayo watu wanaotokana naye wanafanya. Mpango ukiwa mzuri unakuwa na manufaa kwa pande zote kuliko kufanya matangazo pekee.

Kwa makundi uliyojifunza hapa, angalia yale ambayo yanaweza kufanya kazi vizuri kwa biashara yako kisha yatumie kutekeleza mpango wa wapambe.

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Kutumia Wapambe Kufikia Wateja Wengi.

Kwenye kutumia wapambe kuwafikia watu wengi, kuna mambo ya kuzingatia ili zoezi zima liwe na tija kwa biashara. Baadhi ya mambo hayo ni kama ufuatavyo;

1. Kuingia makubaliano ya malipo.

Hatua muhimu kwenye mpango wa wapambe ni makubaliano ya malipo. Hili lazima liwe wazi na kueleweka vizuri kwa pande zote. Kama malipo ni kamisheni kutoka kwenye malipo, basi ijulikane ni kiasi gani na inalipwaje. Mpango wa malipo usipojulikana huwa inaleta mkanganyiko na mpango mzima kushindwa.

2. Kuwa na njia ya kupima wateja wanaotoka kwa mpambe.

Ni muhimu kuwe na njia ya kujua wateja ambao wametoka kwa mpambe fulani ili kuweza kumlipa stahiki yake pale mteja anaponunua. Kwa wateja ambao wanatoka kwenye mtandao, unaweza kuwa na kiungo (link) maalumu ambayo mpambe ndiyo anawapa wateja anaowashawishi kununua waitumie, hapo utajua ni nani kamleta mteja. Kwa biashara nyingine zinazotumia mawasiliano, kunaweza kuwa na neno fulani la siri (code) ambalo mteja anapaswa kulitumia ili kujulikana ametoka kwa mpambe gani. Na kwa biashara ambazo hazihusishi mtandao wala mawasiliano, kunaweza kuwa na kadi maalumu ambazo biashara inawapa wapambe, kisha wapambe wanawapa wateja wanaowashawishi kadi hizo waje nazo kwenye biashara. Hapo biashara itajua mteja ametoka kwa mpambe yupi.

3. Kuwalipa wapambe kulingana na makubaliano.

Mpambe anapoleta wateja, alipwe kulingana na makubaliano yaliyopo, hata kama malipo yanaonekana ni makubwa sana. Huwa kuna tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kusumbua kufanya malipo pale mpambe anapoonekana kupata malipo makubwa. Hupaswi kuwa hivyo, wewe walipe wapambe kulingana na makubaliano, watakuamini na kuendelea kushirikiana na wewe.

4. Kuwakumbusha wapambe pale wanapokuwa hawaleti wateja.

Unaweza kuwa na wapambe wengi na wakawa hawakuletei wateja kama unavyojua inawezekana. Wakumbushe mara kwa mara kuhusu mpango wenu na jinsi ambavyo wanakosa malipo kutoka kwako kwa sababu hawaleti wateja. Hatua hiyo ya kuwakumbusha inawasukuma kuchukua hatua ya kuwashawishi wateja kuja kununua ili wapate malipo. Ukiona kimya kumbushia, usiridhike tu.

5. Kuendelea kuongeza wapambe zaidi bila ukomo.

Usijiwekee ukomo ni wapambe kiasi gani unataka kufanya nao kazi. Wewe endelea kuongeza wapambe kadiri fursa zinavyojitokeza. Kwa kila mteja unayemuuzia mpe mpango wako wa wapambe na manufaa watakayopata. Kwa wafanyabiashara unaokutana nao na wanahudumia wateja unaowalenga, wape mpango wako wa wapambe. Fanya hivyo kwa makundi mengine tuliyojifunza ili kukuza mtandao wako a wapambe na kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi.

Kutumia wapambe kufikia wateja wengi ni njia yenye nguvu kubwa na ambayo haina gharama kubwa kwa biashara, kwa sababu mpambe analipwa pale mteja anaponunua. Kwa kuwa na wapambe sahihi na mpango bora wa malipo, wapambe hao watafanya kazi ya kuitangaza biashara yako kwa ukubwa kitu kinachoiwezesha biashara kuwafikia watu wengi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.