3550; Mauzo ambayo hayawezi kukosa wateja.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kuna kitu kimoja huwa kinashangaza sana.
Watu wanaweza kuwa kwenye umasikini wa kupindukia, wakakosa fedha hata za kukidhi mahitaji yao ya msingi.
Lakini inapokuja kwenye mambo ya burudani na starehe, watu hao huwa tayari kugharamia wasikose.

Kila eneo utakuta watu ambao ni masikini zaidi ndiyo pia walevi kupindukia.
Utakuta watu ambao wanasingizia kukosa mtaji wa biashara, wanatoa michango ya sherehe mbalimbali.

Hivi umewahi kwenda kumwomba mtu akusaidie kiasi fulani cha fedha utatue changamoto yako na akakuambia hana au kukupa kidogo. Halafu akaishia kukununulia pombe au kukulipia starehe nyingine ambayo gharama yake ni kubwa kuliko kiasi cha fedha ulichohitaji?
Hii hutokea mara kwa mara, mpaka unatamani kumwambia mtu ni bora angekupa hizo fedha badala ya kulipia anasa hizo.

Tunajua pia kwamba ukiwaomba watu wakuchangie fedha ya kuanza biashara, watakupa kila sababu kwa nini wanakwama kukamilisha hilo.
Lakini ukiwaomba watu wakuchangie fedha ya kufanya sherehe, watakuchangia kiasi kikubwa kuliko hata ambacho ungehitaji kuanzisha biashara.

Mara nyingi tumekuwa tunaona watu wanapata michango ya harusi inayozidi milioni 20 wakati wanakosa mtaji wa milioni 10 wa kuanzisha au kukuza biashara zao.

Sasa hayo yote ni mambo yanayoshangaza sana, ambayo kila tukiyatafakari hatuyapatii majibu.
Lakini ukweli ni kwamba watu huwa hawashindwi kugharamia kile kinachowapa raha.

Kwa maana hiyo basi, kama kuna kitu kimoja unachotaka kuuza na usikose kabisa wateja ni raha.
Uza raha na hakuna yeyote atakayeweza kukukatalia.
Kwa sababu watu wanapenda na kuthamini zaidi raha.

Hili halimaanishi uache kila unachofanya na uende kufungua baa, au biashara ya starehe na burudani.
Badala yake inamaanisha uweke kila unachofanya kwa namna ambayo kinawapa watu unaowalenga raha.

Mahangaiko yote ambayo watu wanayo kwenye maisha yao wanatafuta vitu vitatu tu; UTAJIRI, AFYA na FURAHA.

Hivyo kwa kila unachofanya na kuuza, waonyeshe watu jinsi kinavyotimiza hayo matatu.
Kwenye UTAJIRI waonyeshe kinavyowaongezea kipato au kuwapunguzia gharama.
Kwenye AFYA waonyeshe jinsi kinavyoboresha afya na mwonekano wao.
Na kwenye FURAHA, waonyeshe jinsi maisha yao yanakwenda kubadilika na kuwa vile wanavyotaka wao.

Usiuze tu kile unachouza, bali wauzie matokeo ya unachouza.
Na matokeo hayo yawe ni UTAJIRI, AFYA na FURAHA.

Rafiki, kile unachofanya au kuuza kinawawezeshaje watu kupata UTAJIRI, AFYA na FURAHA?
Ainisha hayo ili uweze kufanya mauzo ambayo ni ya uhakika kabisa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe