Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Pale tunapotaka matokeo ya uhakika kwenye eneo lolote la maisha yetu, huwa tunawatafuta wale waliobobea kwenye eneo hilo. Kwa mfano unapokuwa unaumwa na unataka kupona kwa uhakika, unahakikisha unapata matibabu kutoka kwa daktari aliyebobea.
Unapokuwa na uwezo wa kumudu unachotaka na huna muda wa kupoteza, unahakikisha unajihusisha na wale wenye ubobezi. Hiyo ni kwa sababu wenye ubobezi wanakupa matokeo mazuri na ya uhakika mara zote. Wenye ubobezi wanajua kitu kwa kina na wana uzoefu mkubwa unaowawezesha kupata matokeo mazuri.

Ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, unapaswa kujijengea ubobezi kwenye maeneo mbalimbali ambayo tutakwenda kujifunza hapa. Ni ubobezi huo ndiyo utakuwezesha kuwapa watu matokeo makubwa na kuwafanya wawe tayari kufanya kazi na wewe.
FAIDA ZA UBOBEZI KWENYE MAUZO NA MAISHA KWA UJUMLA.
Ubobezi una faida nyingi kwenye kila eneo la maisha. Zifuatazo ni faida za msingi ambazo kila mwenye ubobezi huwa anazipata.
1. Kuaminika zaidi.
Wenye ubobezi huwa wanajiamini wao wenyewe na kuaminika zaidi na watu wengine. Pale mtu anapotaka matokeo ya uhakika, huenda moja kwa moja kwa wale wenye ubobezi kwa sababu anaamini atapata kwa uhakika.
Kwenye mauzo, unapokuwa na ubobezi, unaaminika zaidi na wateja.
2. Kuweza kushindana vizuri sokoni.
Ubobezi huwa unampa mtu nguvu kubwa ya kuweza kushindana vizuri sokoni. Pale kunapokuwa na watu wengi wanaofanya kitu, wateja huchagua wenye ubobezi kama mambo mengine yako sawa.
Kwenye mauzo, unapokuwa na ubobezi, wateja wanakuja zaidi kwako kuliko kwenda kwa washindani wako.
3. Kuwa na nguvu kwenye majadiliano.
Kwenye maisha hupati unachostahili bali unachoweza kujadiliana. Kwa kuwa na ubobezi unakuwa na nguvu kwenye majadiliano, kwa sababu watu wanakusikiliza na kuzingatia yale unayotaka wewe.
Kwenye mauzo, unapokuwa mbobezi, unasikilizwa zaidi na hivyo kupata kile unachotaka kwenye majadiliano.
4. Kuongeza mauzo na kipato.
Wenye ubobezi huwa wanaingiza kipato kikubwa kuliko ambao hawana ubobezi. Kwa kuaminika, kuwa na nguvu ya ushindani na kuweza kujadiliana vizuri, unajikuta ukifanya mauzo makubwa na kuongeza kipato chako.
Kwenye mauzo, wenye ubobezi wanafanya mauzo makubwa na kuwa na kipato kizuri.
5. Kupata wateja wa rufaa.
Watu huwa wanaambiana kuhusu matokeo mazuri waliyoyapata kutoka kwa wale wenye ubobezi. Kwenye mauzo hilo hupelekea kupata wateja wa rufaa kwa urahisi zaidi, kitu ambacho kina manufaa makubwa. Wateja wanaoambiwa na wateja wengine huwa ni wazuri kwa sababu wanakuwa na imani kubwa.
Kwenye mauzo, unapokuwa na ubobezi unapata wateja wengi wanaoambiana wao wenyewe na kuja wakiwa na imani kubwa.
Kwa faida hizi na nyingine nyingi, ni muhimu kila muuzaji kujenga ubobezi mkubwa. Swali ni ubobezi gani wa kujenga ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa? Majibu yako hapo chini.
SOMA; Kuwa Tayari Kuanza Upya Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
MAENEO YA KUBOBEA ILI KUWA MUUZAJI BORA NA KUFANYA MAUZO MAKUBWA.
Kuna maeneo mengi ya kubobea kwenye biashara na mauzo ili mtu kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Hapa tunakwenda kujifunza maeneo ya msingi ambayo yeyote anayetaka kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa anapaswa kuyabobea.
1. Bidhaa/huduma unayouza.
Unapaswa kujiua kwa kina bidhaa na huduma unayouza. Uweze kuwaelezea watu jinsi inavyowapa thamani kubwa kuliko gharama ambayo wanalipia. Unapaswa kujua maumivu ambayo wateja wanayo na jinsi yanavyotatuliwa kwa bidhaa au huduma unayouza.
Hatua; Ijue kwa kina bidhaa/huduma unayouza na jinsi inavyofanya maisha ya wateja wako kuwa bora zaidi na waeleze vizuri hayo.
2. Mchakato wa mauzo.
Mauzo ni mchakato ambao una hatua mbalimbali kama kupata wateja wapya, kuwashawishi wakubali kununua, kuwahudumia vizuri, kuwafuatilia kwa msimamo na kuwa na ushawishi. Unapobobea kwenye mchakato huo wa mauzo unaweza kuwa na wateja wengi, kuwashawishi kununua na kuwapa huduma nzuri inayowafanya waendelee kuja na kuleta wateja wengine wengi zaidi.
Hatua; Ujue kwa kina mchakato kamili wa mauzo na bobea kwenye kila hatua ya mchakato huo ili kupata wateja wengi na kufanya mauzo makubwa.
3. Saikolojia.
Kuna tabia za msingi za binadamu ambazo kila anayetaka kufanya vizuri kwenye maisha anapaswa kuzijua na kuzitumia kuwashawishi wakubaliane naye. Kwenye mauzo, watu hawanunui kwa kutumia mantiki, bali wanatumia hisia. Kwa kubobea kwenye saikolojia ya binadamu kunakuwezesha kujua tabia na hisia zinazowasukuma watu kwenye kufanya maamuzi.
Hatua; bobea kwenye saikolojia ya binadamu ili uweze kutumia tabia na hisia zao kuwashawishi wakubaliane na wewe.
4. Mawasiliano.
Mawasiliano ni nguzo muhimu kwenye kila eneo la maisha. Wanaoweza kuwasiliana vizuri kwa njia zote, yaani maandishi, maongezi na hata vitendo ndiyo wanaokuwa na ushawishi mkubwa.
Hatua; bobea kwenye mawasiliano ili uweze kueleweka vizuri kwenye yote unayoeleza kitu kitakachokupa ushawishi mkubwa na kupata unayotaka.
5. Mahusiano.
Mambo yote yakiwa sawa, watu huwa wananunua kwa watu wanaowajua na wanaowapenda na kuwakubali. Hivyo moja ya hitaji kubwa kwenye mauzo ni muuzaji kujenga mahusiano mazuri na wateja wake. Mahusiano hayo yanapaswa kujengwa kwa haraka na kudumishwa kwa muda mrefu. Ni waliobobea kwenye mahusiano ndiyo wanaoweza kujenga mahusiano ya haraka na kuyadumisha kwa muda mrefu.
Hatua; bobea kwenye mahusiano, ili uweze kukubalika kwa haraka na kwa muda mrefu, kitu kitakachokuwezesha kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Kwa kubobea kwenye maeneo haya uliyojifunza hapa, utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Hatua inayofuata ni kujua mambo ya kufanya ili kujenga ubobezi kwenye maeneo haya ya muhimu na kuwa muuzaji bora anayefanya mauzo makubwa.
MAMBO YA KUFANYA ILI KUJENGA UBOBEZI NA KUFANYA MAUZO MAKUBWA.
Ubobezi siyo kitu ambacho mtu anazaliwa nacho au kuanza nacho kwenye kitu chochote kile. Bali ni kitu ambacho kinajengwa na hiyo ni habari njema, kwani kila mtu anaweza kujijengea ubobezi. Ili wewe uwe muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, fanya mambo yafuatayo kwenye kujenga ubobezi.
1. Jifunze endelevu.
Ubobezi unajengwa kwa kujifunza ambapo hakuna ukomo. Yale ambayo mtu anakuwa anajua ni machache sana ukilinganisha na yaliyopo kwenye eneo hilo. Watu wote wenye ubobezi huwa wanajifunza bila ya ukomo. Kila wakati wanajifunza na kuwa bora kwenye yale wanayofanya.
Hatua; chagua kujifunza endelevu kwa kipindi chote cha maisha yako, jione bado hujui na kuwa tayari kujifunza. Kamwe usiwe na kiburi kwa kuona tayari umeshajua kila kitu.
2. Weka kwenye matendo.
Kujifunza pekee haitoshi kukupa ubobezi kwenye eneo unalojifunza. Kuweka yale unayojifunza kwenye matendo ndiyo kunakufanya uwe mbobezi. Hata ujifunze kiasi gani, kuna mambo huwezi kuyajua na kuyaelewa bila ya kuweka kwenye matendo yale unayojifunza. Kufanya kwa kurudia rudia ndiyo kunajenga ubobezi mkubwa.
Hatua; weka kwenye matendo yale yote unayojifunza kwa kufanya kwa kurudia rudia ili uelewe kwa kina na kuzoea kwenye kufanya. Kadiri unavyozoea kwenye kufanya ndiyo unafanya kwa ubora.
3. Jaribu vitu vipya.
Ubobezi ni kuwa mbele ya wengine kwenye eneo husika. Unakuwa mbele ya wengine pale unapokuwa tayari kujaribu vitu vipya. Watu wengi huwa hawapendi mabadiliko. Wakishapata kitu kinachofanya kazi, wataendelea na hicho tu. Kwa wewe kuwa tayari kujaribu vitu vipya, hata kama ulivyonavyo bado vinafanya kazi inakufanya kuwa mbele ya mabadiliko na wengine. Hilo linakufanya kuwa mbobezi na kunufaika na mabadiliko ambayo yanatokea mara zote.
Hatua; usifanye tu kwa mazoea, badala yake jaribu vitu vipya kila wakati. Hakikisha unakuwa mbele ya wengine mara zote.
4. Kuwa king’ang’anizi.
Kwenye kujifunza, kuchukua hatua na kujaribu vitu vipya utapata matokeo ambayo ni tofauti na ulivyotegemea. Kwa maneno mengine ni utakosea mara nyingi kuliko kupatia. Ni lazima uwe king’ang’anizi kama unataka kujenga ubobezi kwenye eneo lolote lile. Huwa kuna kauli inasema; ‘mbobezi ni mtu aliyefanya makosa yote yaliyopo kwenye eneo husika.’ Kama huna uvumilivu na ung’ang’anizi, utakata tamaa haraka pale unapokosea.
Hatua; kuwa king’ang’anizi usiyekata tamaa wala kurudi nyuma, bila ya kujali umepitia au kukutana na nini. Hivyo ndivyo unavyoweza kuvuka yote yanayokuzuia kwenye safari ya ubobezi.
5. Shirikiana na waliobobea.
Huwa kuna kauli inasema; ‘chuma hufua chuma’. Huwezi kuwa na ubobezi mkubwa kama unazungukwa na watu ambao hawana ubobezi. Kwenye kila tasnia, wote waliobobea huwa wanazungukwa na wabobezi wenzao. Ni kwa njia hiyo ndiyo wanasukumana na kushawishiana kuwa bora zaidi kwenye yale wanayofanya.
Hatua; shirikiana na wale waliobobea kwenye mauzo ili upate hasira, msukumo na ushawishi wa kubobea kama wao. Unapokaa na watu wenye tabia fulani, huwa unaiga tabia hizo. Shirikiana na waliobobea ili na wewe ubobee.
Kujenga ubobezi ni hitaji muhimu kwenye kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, hiyo ni kwa sababu ubobezi unapelekea kuaminika zaidi. Kubobea kwenye mchakato wa mauzo na maeneo mengine yanayohusika ni muhimu ili kua muuzaji bora. Kujifunza endelevu na kuweka kwenye matendo unayojifunza ni njia ya uhakika ya kujenga ubobezi kwenye kila eneo.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.