3556; Tatizo ni ujuzi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kitu ambacho kimekuwa kinakukwamisha wewe kupata mafanikio unayoyataka ni ujuzi.
Kwenye kila eneo ambalo hupati matokeo unayotaka, siyo kwa sababu huwezi, bali ni kwa sababu hujui.
Kama huna fedha, tatizo siyo huwezi kupata fedha, maana kuna ambao wana uwezo wa chini kuliko wewe, ila wana fedha nyingine kuliko wewe.
Tatizo ni huna ujuzi wa kupata, kutunza na kuzalisha fedha.
Kama hupati watu sahihi, tatizo siyo kwamba watu hao hawapatikani, wapo sana, ila wewe huna ujuzi wa kuwapata na kuwatunza.
Afya, mahusiano na mengine yote kwenye maisha, yana ujuzi ambao mtu unapaswa kuwa nao ndiyo uweze kupata matokeo mazuri kadiri ya unavyotaka.
Unapoona tatizo ni kukosa uwezo, unakuwa umejiwekea ukomo kwenye kupata yale unayotaka.
Ukishajiambia huwezi, umejipa hukumu ya milele juu ya kitu hicho.
Lakini ukiona tatizo ni ujuzi, unakuwa umefungua fursa ya kupata yale unayotaka.
Kwa kuwa ujuzi ni kitu ambacho kila mtu anaweza kujijengea, unakuwa na fursa ya kujenga ujuzi huo ili kupata unachotaka.
Kama unataka kuyarahisisha maisha yako na kupata kila unachotaka kwa uhakika, angalia kila tatizo kama ukosefu wa ujuzi.
Kwa kila tatizo unalokuwa nalo kwenye maisha, jua linatokana na kukosa ujuzi wa aina fulani.
Wajibu wako ni kujua ni ujuzi upi uliokosa mpaka kutengeneza tatizo ulilonalo.
Ukishajua ujuzi uliokosa, wajibu wako ni kujijengea ujuzi huo kwa uhakika.
Kadiri unavyokuwa na ujuzi mahiri kwenye maeneo mengi, ndivyo unavyotatua matatizo mengi na kuvuka changamoto zinazokukabili ili kupata unachotaka.
Hiyo ndiyo inafanya kujifunza endelevu na kuweka kwenye matendo yale unayojifunza kuwa hitaji la msingi kwenye maisha.
Hivyo ndivyo ujuzi unavyojengwa, kwa kujifunza na kuchukua hatua.
Hata unapokutana na watu ambao wamekuzidi kwenye maeneo mbalimbali, jua kuna ujuzi walionao ambao wewe umeukosa.
Ukiweza kujijengea ujuzi huo, kwa hakika na wewe utaweza kufika na kupata waliyonayo.
Rafiki, kwa matatizo na changamoto kubwa zinazokukabili sasa, ni ujuzi upi unaoona umeukosa?
Ainisha ujuzi wote ambao huna na anza kujijengea kupitia kujifunza na kuweka kwenye vitendo.
Tatua kila tatizo na vuka kila ukomo kwa kujijengea ujuzi sahihi kwako.
Fanya kujifunza na kuchukua hatua kuwa kitu endelevu kwenye maisha yako.
Hivyo ndivyo unavyoweza kujenga mafanikio makubwa na yasiyo na ukomo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe