3562; Udhibiti ulionao.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa yanataka mtu awe na udhibiti mkubwa kwenye maisha yake.
Kwa hali ilivyo sasa, watu wengi sana hawatapata mafanikio makubwa, siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu wanakosa udhibiti.
Usumbufu umekuwa mwingi kiasi cha kuwapoteza watu kabisa.
Fursa zimekuw mpya na nyingi kila wakati kiasi cha kuwavuruga watu.
Na watu wanahangaika na mengi ambayo yapo nje ya uwezo wao na kuona hawana uwezo wa kupata au kufika kule wanakotaka.
Rafiki, leo nataka nikukumbushe udhibiti ulionao na jinsi unavyoweza kuutumia kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Una udhibiti wa kukataa kuhangaishwa na usumbufu ambao umekuwa unakukwamisha.
Ukiangalia usumbufu mwingi unatokana na vitu ambavyo una udhibiti navyo kabisa.
Ni simu yako janja, mitandao, habari na mengine ya aina hiyo.
Una udhibiti wa kusema HAPANA kwa kila sina ya usumbufu.
Una udhibiti wa kuchagua kuweka umakini wako kwenye kitu kimoja mpaka kikupe matokeo makubwa.
Pamoja na fursa nyingi zinazokuja kwako na kukutamanisha, unaweza kutohangaika nazo ili umakini wako uuweke kwenye fursa kuu uliyochagua.
Ukishachagua fursa moja, sema hapana kwa nyingine nzuri zinazokuja ili uifanyie kazi vizuri hiyo moja badala ya kugusa juu juu nyingi.
Una udhibiti wa kuhangaika na yaliyo ndani ya uwezo wako na kuachana na yaliyo nje ya uwezo wako.
Unajua kabisa yapi yako ndani ya uwezo wako na nini cha kufanya, hangaika na hayo.
Pia unajua yale yaliyo nje ya uwezo wako na huna cha kufanya, yakubali kama yalivyo.
Tunachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kwamba maisha yako yanadhibitiwa na yale unayoyapa umakini wako.
Ukidhibiti umakini wako, umedhibiti maisha yako na utaweza kupata chochote unachotaka.
Rafiki, ni kwa kiasi gani una udhibiti na umakini wako? Hapo ndipo penye kila unachotaka kwenye maisha yako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe