3564; Biashara inayolipa zaidi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Swali la biashara gani inayolipa zaidi limekuwa linaulizwa kila mara.

Hiyo ni kwa wote, waliopo kwenye biashara na wanaotaka kuingia kwenye biashara.

Jibu la swali hilo ni kila biashara inalipa.
Kila biashara inayotoa thamani kwa watu inalipa vizuri.

Kitakachoamua kama biashara italipa vizuri au la ni mtu anayeifanya.

Biashara italipa zaidi kama mtu;
1. Atakuwa na uwezo wa kipekee kwenye ufanyaji wa kile kilocho kikuu kwenye biashara husika.

2. Ataweka kazi na juhudi kubwa kwenye kuifanya.

3. Ataifanya kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha.

4. Ataendelea kuwa bora zaidi kwenye kuifanya, kwa kujifunza endelevu na kukuza hatua ambazo zinafikiwa.

Watu wanapouliza swali la biashara gani inalipa zaidi, wanachotaka kujua ni biashara rahisi kupata faida kubwa bila kufanya kazi kubwa, kitu ambacho hakipo.

Mwenendo wa uchumi tu hauwezi kuruhusu upatikanaji wa faida kubwa bila ya kutolewa kwa thamani kubwa.

Hivyo swali halipaswi kuwa ni biashara gani inayolipa zaidi, bali biashara gani itakayokulipa wewe zaidi.

Na biashara itakayokulipa wewe zaidi ni ile ambayo unaweza kutoa thamani kubwa kwa watu wengi na muda mrefu zaidi.

Rafiki, je ni thamani ipi kubwa unayoweza kutoa kwa wengi na muda mrefu? Hapo ndipo ufunguo wa biashara itakayokulipa zaidi ulipo.
Badala ya kuhangaika kutafuta fursa za nje zitakazokulipa zaidi, anza na fursa za ndani yako mwenyewe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe