3565; Zaidi ya uwezo na vipaji.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu hudhani kinachowakwamisha kufanikiwa ni kukosa uwezo wa vipaji vinavyohitajika.
Lakini kuna wengi ambao wana uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee, ila hawafanikiwi.
Sababu kubwa ikiwa ni mafanikio makubwa yanahitaji zaidi ya uwezo na vipaji.
Uwezo na vipaji ni kama tiketi ya kuingia kwenye mchezo wa mafanikio makubwa.
Ushindi kwenye mchezo huo unategemea vitu vingine vya ziada.
Moja ya vitu hivyo ni matumizi mazuri ya muda.
Muda ni rasilimali muhimu sana kwenye safari ya mafanikio, lakini yenye ukomo na uhaba mkubwa.
Muda ndiyo rasilimali pekee ambayo watu wote tumepewa kwa usawa.
Lakini jinsi tunavyoutumia inatofautiana na ndiyo inaamua kama tutafanikiwa au la.
Kwa kuwa muda una ukomo, ukishatumia muda kwenye jambo moja, huwezi kuutumia tena kwenye jambo jingine.
Hivyo ili uweze kutumia vizuri muda wako, ni lazima uachane na yale yasiyokuwa muhimu na kupeleka muda wako kwenye yaliyo muhimu pekee.
Ni lazima uwe na vipaumbele kwenye matumizi ya muda wako, uupeleke kwenye yale muhimu zaidi ambayo yana mchango kwenye mafanikio yako.
Ukiwasikia jinsi watu wanavyouongelea muda, utaona kwa nini ndiyo kikwazo kikubwa kwao kufanikiwa.
Utawasikia watu wakisema muda haupo, na hapo unashindwa kuelewa wanamaanisha nini.
Kivipi inakuwa muda haupo wakati watu wote tumepewa muda kwa usawa?
Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wana muda sawa.
Jinsi wanavyotumia muda huo ndiyo inaleta tofauti kati yao.
Rafiki, ni kwa namna gani wewe unapangilia na kutumia muda wako ili uweze kufanya makubwa zaidi?
Kwenye matumizi ya muda ndipo unaweza kujitofautisha na wengi, weka uzito hapo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe