3567; Epuka kupoteza.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio kwenye maisha hayatokani tu na kupata kitu, bali kuweza kukitunza pia.
Kuna wengi ambao huwa wanapambana mpaka wanapata kitu walichokuwa wanataka.
Lakini wanashindwa kutunza walichopata na hivyo kuishia kukipoteza.
Hiyo ni kwa sababu anachofanya mtu ili kupata kitu ni tofauti na anachopaswa kufanya ili kukitunza.
Mfano mzuri ni kwenye biashara.
Wengi hupiga kelele za kutangaza biashara zao ili kupata wateja.
Kweli wanapata wateja, lakini hawadumu nao kwa muda mrefu.
Kiuhalisia, wateja wengi hununua mara moja na wasirudi tena.
Kupata wateja wa biashara, unapaswa kutangaza kwa msimamo na ukubwa.
Kuwatunza wateja hao ili usiwapoteze, kuna vitu vya tofauti unapaswa kufanya;
1. Unapaswa kuwapa zaidi ya ulivyowaahidi, unatakiwa kuwashangaza kwa thamani kubwa unayowapa tofauti na matarajio waliyokuwa nayo.
2. Unapaswa kuendelea kuwafuatilia kwa karibu. Mauzo hayaishii pale mteja anaponunua, bali ndiyo yanaanza. Ufuatiliaji endelevu ndiyo unaowaweka wateja karibu na biashara na kuwafanya wasiisahau.
3. Omba rufaa. Waombe wateja ulionao wakupe wateja zaidi. Watu wanapokuwa tayari kukupa wateja, ni kiashiria wamekukubali na wataendelea kununua kwako. Kwa sababu hawawezi kuwapeleka watu wao wa karibu mahali halafu wakawaacha hapo.
4. Omba wakupe ushuhuda. Watu wakikupa ushuhuda wanakuwa na deni la kutimiza ushuhuda huo. Na pia ushuhuda huo unakuwa na ushawishi mzuri kwa wengine.
5. Angalia njia za kuwasaidia zaidi. Wateja ni zaidi ya biashara yako, unapaswa kwenda hatua za ziada kuwapa thamani kiasi cha kukutegemea wewe zaidi. Haitoshi tu kuwauzia wateja kile unachouza, unapaswa kwenda hatua ya ziada kwa kuwasaidia kwenye mambo mengine wanayokuwa wanakwama.
Rafiki, ni mara ngapi umekuwa unapoteza vitu ambavyo umeshavipata na kujikuta kama unaanza upya kila wakati?
Ukiweka juhudi kubwa kuepuka kupoteza yale ambayo umeshayapata, utaweza kupata mafanikio na kudumu nayo kwa muda mrefu.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe