3568; Mzunguko wa Upendo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kama kuna kitu kimoja ambacho kinaweza kumpa mtu mafanikio kwa uhakika ni upendo.

Hiyo ndiyo nguzo kuu ambayo imebeba kila kitu.
Yeyote anayejenga mafanikio yake kwenye upendo, yanakuwa ya uhakika na ya kudumu.

Upendo unaanza na wewe mwenyewe, kwa kujipenda na kujikubali sana.
Halafu upendo huo unaenda kwa wengine, kwa kuwapenda na kuwakubali sana wote wanaokuzunguka.
Na mwisho upendo unaenda kwenye kile unachofanya, unapaswa kukipenda na kukikubali sana kama unataka kupata mafanikio makubwa.

Hivyo ndivyo upendo unavyogusa kila eneo la maisha na kuathiri mafanikio.

Kuna mzunguko wa upendo ambao ukiweza kuujenga kwenye biashara yako itakuwa yenye mafanikio makubwa sana.

Mzunguko huo unaanza na wewe kuwapenda wafanyakazi unaokuwa nao kwenye biashara hiyo.
Hapo lazima uwe unapenda biashara hiyo na kuweka watu sahihi ambao unafurahia kufanya nao kazi.

Mzunguko unaendelea kwa wafanyakazi wa biashara yako kuwapenda wateja wa biashara hiyo.
Hapo lazima wafanyakazi unaokuwa nao wapende kile wanachofanya kwenye biashara ili wafurahie kuwahudumia vizuri wateja.

Mzunguko unaishia kwa wateja kupenda bidhaa/huduma wanazopata kwenye biashara yako.
Hapo lazima wawe na maumivu au mahitaji yanayotimizwa na kile wanachopata kwako.

Ukiunganisha yote hayo kwa pamoja, unaona jinsi mzunguko wa upendo ulivyo na nguvu.
Wewe kupenda wafanyakazi, wafanyakazi kupenda wateja na wateja kupenda bidhaa/huduma ambayo ndiyo wewe unaipenda na inayokusukuma kuwa kwenye biashara.

Rafiki, upo kwenye biashara ambayo unaona mafanikio ni magumu kupatikana? Anza na bidhaa/huduma ambayo ina thamani kwa wateja, ajiri watu unaopenda kufanya nao kazi, hakikisha wanapenda wanachofanya ili wawapende wateja na hilo litawafanya wateja waipende bidhaa/huduma unayouza.

Zungusha upendo na kwa hakika utafanikiwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe