3580; Njia pekee ya mkato inayofanya kazi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Mimi huwa siyo muumini wa njia za mkato za mafanikio.
Nimekuwa nikisisitiza mara zote umuhimu wa kukaa kwenye mchakato sahihi ili kujenga mafanikio ya uhakika.

Wengi wamekuwa hawasikilizi, wanakimbizana na njia za mkato na kuishia kupoteza siyo tu fedha, bali muda na heshima.

Unakuta mtu alikuwa anaaminiwa na kuheshimiwa na watu vizuri tu.
Anatumia imani na heshima hiyo kuwaingiza watu hao mahali pasipofaa kwa kuhangaika na njia za mkato.

Matokeo yake ni mtu kupoteza imani na heshima.
Ni bora upoteze pesa utazipata tena, ila muda na heshima, vikienda vimeenda.

Tukirudi kwenye mada ya njia za mkato, leo nataka nikushirikishe njia pekee ya mkato ambayo inafanya kazi kwa uhakika.

Njia hiyo ni tofauti kabisa na njia nyingine.
Ni ya mkato kwa sababu inakupunguzia muda ambao ungepaswa kusubiri ndiyo ufanikiwe.

Rafiki, njia ninayokushirikisha hapa ni kuiga kile ambacho tayari kinafanya kazi, kisha kukifanya kwa ubora.

Unataka njia ya mkato ya kufanikiwa kwenye biashara? Angalia kile ambacho tayari watu wanakinunua kwa wingi, kisha kiuze kwa namna ambayo hawakipati pengine popote.

Unataka njia ya mkato ya kufanikiwa kwenye ajira? Angalia yale anayofanya bosi wako kisha yafanye kwa ubora wa hali ya juu.

Rafiki, kwenye mafanikio huna haja ya kugundua upya tairi.
Tayari matairi yaliyopo yanafanya kazi vizuri, yatumie hayo.

Kuna watu wengi tayari wameshafanikiwa, angalia yale waliyofanya na wakafanikiwa, kisha yafanye zaidi.

Huna haja ya kuja na ugunduzi mpya.
Kwanza utakuchelewesha, maana ni mpaka uwasukume sana watu ndiyo waelewe.

Nenda na kile ambacho tayari watu wamekielewa.
Kifanye kwa namna ya tofauti na upate mafanikio makubwa.

Tukiwa hapa hapa kwenye njia za mkato, kuna moja rahisi sana halafu watu wanaipuuzaga sana.
Na huwa inawagharimu sana.

Unakuta mtu ana mtaji labda wa milioni moja na anataka kuanza biashara.
Anatafuta ushauri wa biashara, anaambiwa anunue kitabu cha elfu 10 ajifunze misingi ya biashara.
Anaona hiyo ni pesa kubwa sana, anaingia kichwa kichwa na kupoteza milioni moja.

Fikiria mwenyewe hapo, mtu anapoteza milioni moja kwa sababu ya kuokoa elfu 10. Anapotea zaidi.
Ambacho mtu anashindwa kuelewa ni kwamba, kulipa elfu 10 upate maarifa ni moja ya njia za mkato.
Kuna mambo utajifunza na kuepuka ambayo yangekupotezea muda na fedha.

Rafiki, mara ngapi umehangaika kutumia akili zako mwenyewe na kuishia kupoteza? Usijicheleweshe tena, tumia njia ya mkato inayofanya kazo. Iga yale ambayo tayari yanafanya kazi na yafanye kwa ubora wa hali ya juu kabisa.
Utapata matokeo mazuri kama hayo pia.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe