3583; Matatizo ya nani yanakusumbua?

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Matatizo ni sehemu ya maisha.
Japo unatamani sana maisha ambayo hayana matatizo.
Lakini ni maisha ambayo yatakuchosha.

Kinachofanya maisha yawe na maana ni matatizo mbalimbali tunayokabiliana nao.
Na kinachotuwezesha kupata mafanikio makubwa ni matatizo pia.

Wapo wanaodhani mafanikio ni kutokuwa na matatizo kabisa.
Lakini mafanikio ni kuweza kutatua matatizo makubwa zaidi.
Kiwango chako cha mafanikio kinategemea kiwango cha matatizo unayotatua.

Lakini hapo kuna tahadhari, juu ya aina ya matatizo unayohangaika nayo.
Maana unaweza kusema mbona masikini wana matatizo mengi lakini hawafanikiwi?

Jibu ni masikini na wengi walioshindwa wanahangaika na matatizo yao wenyewe.
Wakati matajiri na waliofanikiwa wanahangaika na matatizo ya wengine.

Hapa pia tunapata kitu kingine muhimu sana kuhusu mafanikio.
Kwamba unapaswa kusumbuka na matatizo ya wengine kama unataka kufanikiwa.
Na kadiri unavyosumbuka na matatizo makubwa na yanayowagusa wengi, ndivyo unavyoweza kujenga mafanikio makubwa zaidi.

Ukihangaika na matatizo yako mwenyewe, inakuwa ni wewe tu, ambaye pia siyo mteja mzuri.
Ukihangaika na matatizo ya watu wengine, unawagusa wengi, na huko kuna wateja wazuri.

Mara zote hangaika na matatizo, lakini siyo matatizo yako mwenyewe, bali ya wengine.
Hangaika na matatizo magumu na yanayowasumbua watu wengi.
Hayo ndiyo yana mafanikio makubwa ndani yake.

Kama una matatizo mengi na hujafanikiwa, ni kwa sababu unatumia muda mwingi kwenye matatizo yako mwenyewe.
Hebu badili hilo, uanze kuhangaika na matatizo ya wengine na kuyatatua kwa namna bora kwao.
Hapo utafungua milango ya mafanikio makubwa kwako.

Rafiki, umekuwa unasumbuka na matatizo yako mengi lakini hufanikiwi?
Badilika, acha kuhangaika na matatizo yako na anza kuhangaika na matatizo ya wengine. Angalia matatizo makubwa na yanayowasumbua wengi, njoo na suluhisho la uhakika na mafanikio makubwa yatakuwa yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe