3594; Unajifunza kutoka kwa nani?

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli inayosema; Mpumbavu hajifunzi kabisa, mjinga hujifunza kwa makosa yake mwenyewe na mwerevu hujifunza kutoka kwenye makosa ya wengine.

Swali ni je wewe unajifunza kutoka kwa nani?

Kama umekuwa unarudia makosa yale yale, maana yake hujifunzi kabisa.
Na hilo ni hatari sana kwenye maisha yako, kwa sababu unayapoteza bila sababu yoyote.

Kama umekuwa unafanya makosa kwanza ndiyo ujifunze, angalau unajifunza.
Lakini unajichelewesha kufanikiwa kwa sababu unapoteza muda mwingi kwenye kufanya makosa ambayo wengine walishayafanya na kutoa njia ya kuyakwepa.

Na kama umekuwa unajifunza kutoka kwenye makosa ya wengine na kuepuka kuyarudia, upo kwenye njia ya mkato, ambayo pia ni ya uhakika kwako kufanikiwa.

Kutokujifunza kabisa ni mzigo mkubwa, siyo tu kwako mwenyewe, bali na kwa wanaokuzunguka pia.
Kuna makosa utatarudia ambayo yatawaathiri wengi na siyo wewe peke yako.

Kujifunza kutokana na makosa yako kuna afadhali, lakini kunakuchelewesha.
Makosa ya kufanya mpaka ufanikiwe ni mengi sana.
Kama unataka uyarudie mwenyewe, utajichelewesha sana.

Huwa hakuna njia ya mkato ya mafanikio inayofanya kazi kwa uhakika.
Lakini kujifunza kutokana na makosa ya wengine ni njia pekee ya mkato inayofanya kazi.

Ujumbe mkuu wa kuondoka nao hapa ni jifunze kutokana na makosa ya wengine na usiyarudie.

Swali ni unajifunzaje kutokana na makosa ya wengine?

Moja; angalia mambo ambayo watu walioshindwa wanafanya na usiyafanye. Huu ni ushauri wa bure na unaofanya kazi vizuri kabisa.
Una watu wengi wanaokuzunguka, angalia wale ambao hutaki kuwa kama wao na epuka kufanya yale wanayofanya.
Maana hayo ndiyo makosa yao.

Mbili; omba ushauri kwa wale waliofika kule unakotaka kufika.
Chochote unachotaka kufikia, kuna watu ambao tayari wameshafikia.
Watu hao walishafanya makosa mengi na kujifunza kutokana na makosa ya wengine.
Uzuri ni watu hao huwa tayari kushirikisha yote waliyojifunza.
Ni wewe tu kuwauliza na kusikiliza kwa makini.

Tatu; soma vitabu vya watu waliofanikiwa kwenye maeneo mbalimbali.
Vitabu vya wasifu wa watu, huwa vinaeleza mengi, ambayo ni darasa tosha la maisha kwa yeyote aliye tayari kujifunza na kuzingatia
Kwa gharama kidogo na muda, unaweza kujifunza chochote unachotaka kujifunza.
Uzuri ni wengi waliofanikiwa wameandika vitabu. Pamoja na baadhi ya walioshindwa, wameandika au kuandikiwa vitabu.
Unapokuwa tayari kujifunza, njia za kujifunza ni nyingi sana.

Rafiki, umekuwa unajifunza kutoka kwa nani?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini jinsi ambavyo umekuwa unajifunza na hatua za tofauti unazokwenda kuchukua baada ya kujifunza hapa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe