3596; Ukomo wa muda.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kanuni ya Parkinson inasema kwamba jukumu huwa linachukua muda ambao limepangiwa kufanyika.
Kama kuna jukumu fulani unafanya na una siku nzima ya kulifanya, utalifanya kwa siku nzima.
Lakini kama umepewa masaa matatu tu ya kulifanya jukumu hilo hilo, litakamilika kwa muda huo pia.
Kadiri unavyokuwa na muda mwingi wa kufanya kitu, ndivyo unavyochelewa kukifanya.
Unajikuta ukipoteza muda mwingi zaidi pale unapokuwa ni muda mwingi.
Hivyo kama unataka kukamilisha jambo ndani ya muda mfupi na kutokupoteza muda, jiwekee ukomo wa muda.
Kwa kila jambo unalofanya, liwe kubwa au dogo, jiwekee ukomo wa muda wa kulifanya.
Ukomo huo wa muda unapaswa kuwa mfupi kuliko ilivyozoeleka.
Na ukishajiwekea huo ukomo, unaufuata kweli kama ulivyouweka.
Kuijenga hiyo kuwa nidhamu, unapaswa kufanya jambo kwenye muda uliopanga.
Na muda huo ukiisha, hupaswi kufanya tena jambo hilo.
Unapokuwa na muda wenye ukomo wa kufanya jambo, huupotezi kwa mambo yasiyokuwa na tija.
Utakazana na yale yaliyo muhimu ili kukamilisha.
Na hayo pekee ndiyo yanayohitajika.
Kuwa na ukomo wa muda huwa kunaondoa upotevu wa muda kwenye kutaka ukamilifu.
Watu wengi sana wameshindwa kukamilisha mambo kwa sababu wanasubiri mpaka yawe yamekalika kabisa.
Wakati mara nyingi mambo yanapaswa kukamilishwa vile yalivyo na siyo kusubiri mpaka yawe yamekamilika kabisa.
Huwa kuna kauli inasema kama unataka jambo lifanyike, mpe mtu ambaye tayari yuko bize.
Mtu huyo, pamoja na uhaba wake wa muda atakamilisha mengi kuliko watu ambao wana muda mwingi.
Hiyo ni kwa sababu ubize unamlazimisha mtu kuwa na ukomo wa muda.
Ukimpa mtu jukumu la kufanya kwa sababu umeona ana muda mwingi ambao hana cha kufanya, tegemea kuchelewa kukamilika kwa jukumu hilo.
Kadiri watu wanavyokuwa na muda mwingi wa kufanya jambo, ndivyo wanavyoupoteza kwenye mambo yasiyokuwa na tija kwenye jambo husika.
Rafiki, ni mara ngapi umeshindwa kukamilisha mambo uliyopanga? Kukosa ukomo wa muda kunachangia kwenye hilo.
Mara zote weka ukomo wa muda kwenye kila jambo unalofanya au kuwapa wengine safanye.
Ukomo wa muda unakulazimisha kuhangaika na yaliyo muhimu na kuachana na yasiyokuwa muhimu.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe