Usemi wa elimu haina mwisho ni usemi maarufu sana ambao umekuwa unatumika sehemu nyingi na watu wengi. Pamoja na watu wengi kuujua msemo huu sina hakika kama wote tunafahamu maana halisi ya msemo huu. Wengi huchukua msemo huu kwa maana kwamba hata mtu awe na umri mkubwa kiasi gani anaweza kwenda darasani na kusoma(kama hakusoma) ama baada ya kuhitimu ngazi fulani ya masomo baadae wanaweza kurudi kusoma ngazi inayofuata. Kwa mfano kutoka cheti, stashahada, shahada, shahada ya uzamivu mpaka kuwa profesa. Hizo ni baadhi ya maana za usemi wa elimu haina mwisho, ila kuna maana kuu zaidi ya usemi huo.
    Maana halisi ya elimu haina mwisho ni kwamba kila siku na kila wakati tunatakiwa kujifunza. Kujifunza hakuishii darasani tu, tunatakiwa kujifunza hata kama tumeshamaliza masomo. Wengi wetu hufikiri tukishamaliza tu masomo ndio mwisho wa kujifunza ama kusoma na tukitaka kuongeza elimu zaidi ni mpaka turudi tena darasani kuendelea kusoma ngazi inayofuata ya elimu. Wengi wetu tunaacha kujiendeleza wenyewe kwa kujisomea mara tunapomaliza masomo.
   Elimu haina mwisho hivyo hakikisha kila siku kuna kitu unajifunza. Usikubali siku ianze na iishe bila ya wewe kujifunza chochote kipya. Unaweza kujifunza kwa kujisomea vitabu, kuzungumza na watu ama kwa kupitia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni au kupitia mtandao. Chochote unachojifunza(kizuri) kuna siku kitakusidia kwenye maisha ama kwenye shughuli zako unazofanya kujipatia riziki. Kwa ulimwengu wasasa huwezi kukosa kabisa njia ya kujifunza, ni wewe tu kuamua unajifunza nini. Waweza kuamua kujifunza njia bora zaidi za kufanya biashara na ujasiriamali, kujifunza uongozi, kujifunza siasa, falsafa, saikolojia na mengine mengi. Chochote utakachoamua kujifunza hakikisha unaongeza uelewa wako kila siku.
  Pia ni muhimu kujifunza kupitia makosa, kila mtu amewahi kufanya kosa fulani, iwe ni kwenye maisha ya kawaida au kwenye kazi. Hakikisha unajifunza kutokana na makosa unayoyafanya. Baada ya kufanya kosa usikae tu na kujilaumu ama kutafuta wa kumlaumu badala yake fikiria ni nini umejifunza kutokana na kosa ulilofanya. Hii itakuepusha kurudia kosa hilo ama kufanya kosa jingine linalofanana na hilo siku za mbeleni.