Kuna mali ambayo kila binadamu anaeishi duniani amepewa na wote tumepewa sawa. Hakuna aiezidishiwa wala aliepunguziwa mali hii. Mali ninayoizungumzia ni muda, wote tumepewa saa ishirini na nne kwa siku. Kila mtu anayo saa ishirini na nne kwa siku ila jinsi ya kutumia kila mtu anajua mwenyewe. Utofauti kwenye kutumia hizo saa ndio unaoleta utofauti wa mafanikio kati ya watu. Kuna ambao wanatumia muda wao vizuri na wanafanikiwa na kuna ambao wanatumia hovyo na kuishia kutofanikiwa mipango yao.
Mafanikio yoyote yanaanza na matumizi mazuri ya muda. Muda ni mali ya thamani sana kwenye maisha yako kwa sababu muda ukishapotea haurudi tena. Wengi kama sio wote waliofanikiwa kwenye nyanja mbalimbali kimaisha walitumia ama wanatumia vizuri muda wao. Wanaelewa thamani ya muda na hivyo wanaulinda sana usipotee bila ya kufaidika nao.
Kwa bahati mbaya sana muda huwa unapotea taratibu na kimyakimya sana bila ya sisi kugundua kwamba muda unapotea. Baadae ndipo tunakuja kushtuka kwamba muda umekwenda na hatujafikia malengo tuliyojiwekea. Tuchukue mfano mmoja wa upoteaji wa muda kwa maisha ya kawaida ya kitanzania. Hebu jiulize kila siku kuanzia saa kumi na moja jioni mpaka saa nne usiku(muda wa wengi kulala) huwa unafanya nini cha maana? Katika muda huo kuna saa tano, tukitoa saa moja la kupumzika yanabaki saa nne. Sasa jiulize huwa unayatumia vp hayo masaa (saa kumi na mbili mpaka saa nne usiku). Wengi wetu hatuna chochote cha maana ambacho huwa tunafanya kwenye huo muda, wengi wanakuwa kwenye foleni kurudi majumbani, kuangalia tv, tamthilia ama kupiga soga na ndugu na jamaa. Sio matumizi mabaya sana ila ni matumizi sahihi ya muda ukizingatia malengo uliyojiwekea? Kama unapoteza saa 4 kwa siku ina maana kwa wiki unapoteza saa 28 ambayo ni siku moja na saa 4. Kwa mwezi unapoteza saa 120 ambayo ni siku 6, kwa mwaka unapoteza saa 1460 ambayo ni siku 60 ama miezi miwili. Kwa miaka sita unakuwa umepoteza mwaka mmoja. Yaani kwa miaka sita kuna mwaka mmoja ni sawa na hukuishi kabisa. Hichi ni kiwango kidogo sana ila kuna wengi wanapoteza masaa mengi kwa siku na siku za mwisho wa wiki ndio usiseme kabisa.
Unawezaje kupunguza upotevu wa muda? Na uutumieje muda ambao ungeupoteza kama huna cha kufanya? Nitayajibu hayo kwenye sehemu itakayofuata……..