Duniani kuna makundi mawili ya binadamu, kundi la kwanza ni VIONGZI na kundi la pili ni WAFUASI. Weka mbali uongozi wa siasa ama uongozi mwingine wowote, hapa tunachukulia tabia tu za watu na kuna ambao wana tabia za uongozi na wengine ni wa kufuata wanachoambiwa. Kwa mfano wakichukuliwa watu mia moja na kuwekwa ndani ya chumba kimoja na wote hawajuani baada ya muda kuna ambao watakuwa wanawaongoza wenzao. Hii ina maana kwamba kuna watu wanatabia za uongozi wa wengine wafuasi.
Jitambue upo katika kundi gani, maana kujitambua tu kunatosha wewe kujipanga ili kuweza kufikia malengo yako. Hii ina maana kwamba kama wewe huna tabia yoyote ya uongozi na huna mpango wa kujifunza tabia za kiuongozi basi lazima ufanye kazi chini ya usimamizi. Kama huna tabia za uongozi ukijaribu kufanya kazi ya kujisimamia mwenyewe(kujiajiri) kuna uwezekano mkubwa sana wa kushindwa. Hivyo ni vyema kujua kama wewe utatoka kwa kusimamiwa ama kwa kujisimamia mwenyewe.
Njia rahisi ya kujua kama wewe ni kiongozi ama mfuasi ni kuyatafakari maisha mpaka hapa ulipofikia sasa. Je umekuwa ukifikiria ama kubuni mawazo yako na kuweza kuyafanyia kazi na watu wakavutiwa ama ukipewa kazi na kuelekezwa jinsi ya kuifanya huwa unaifanya vizuri sana? Kama ukigundua wewe ni mfuasi usikate tama, kama unapenda kuwa kiongozi basi unaweza kujifunza na kuwa kiongozi mzuri.
Kuna usemi maarufu kwamba “viongozi huzaliwa”, usemi huu hauna ukweli kwani viongozi pia HUTENGENEZWA, hivyo na wewe unaweza kujitengeneza na kuwa kiongozi mzuri. Hapo ulipo umetengenezwa kuwa hivyo, nguvu kubwa sana ya jamii, elimu zimetumika kukutengeneza ulivyo, hivyo basi ukijitambua na kutumia nguvu sawa na hiyo unaweza kujitengeneza vyovyote utakavyo.