Ukifuatilia vizuri historia ya dunia utaona kwamba kumekuwa na zama mbalimbali kwa kipindi chote binadamu wameishi duniani. Zilianza zama za mawe ambapo binadamu walitumia mawe kutengeneza zana na kazi. Katika zama hizo shughuli kubwa ya wanadamu ilikuwa kilimo na uwindaji. Baadae wakaongeza maarifa na kuweza kutengeneza zana kwa kutumia chuma na ikawa zama za chuma. Katika zama za chuma binadamu waliendelea kuongeza maarifa hatimaye yakawepo mapinduzi ya viwanda ama zama za viwanda. Katika zama za viwanda ilionekana binadamu wamefikia uwezo wa juu kabisa wa wa kufikiri na ugunduzi. Ila haijawa hivyo, uwezo wa binadamu umeongezeka maradufu na sasa zama za viwanda zimepitwa na wakati.
   Sasa tupo kwenye zama mpya na ni zama za taarifa. Katika zama hizi za taarifa, wenye taarifa sahihi ndio wanaotawala kila nyanja ya maisha. Kama ilivyokuwa kwenye zama za chuma na viwanda waliokuwa na mitaji ndio waliotawala. Katika zama hizi za taarifa kuwa tu na mtaji hakuwezi kukusaidia, inabidi pia uwe na taarifa sahihi ya nini kinaendelea duniani. Mabadiliko ya sasa yanatokea kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba kitu kilicho cha thamani sana leo miaka mitatu ijayo kitakuwa hakina thamani. Ukuaji huu wa kasi umewaacha wengi wakiduwaa kwenye zama za viwanda na hapo ndipo matatizo mengi yanapoanzia.
  Tafuta taarifa nyingi na sahihi kwa jambo lolote unalolifanya, iwe umeajiriwa, umejiajiri ama ni mjasiriamali. Kuna mambo mengi yanatokea na thamani yake inakwisha haraka, kama ukichelewa kuzipata taarifa utakuja kustuka wakati thamani yake imekwisha. Ni vyema kubadilisha mifumo yetu ya maisha na ufikiri ili kuendana na zama hizi za taarifa. Kuna mbinu nyingi nzuri ziliwanufaisha sana watu kwenye zama za viwanda ila kwa sasa ukizitumia utaishia kuumia. Mbinu kama fanya kazi kwa nguvu, weka akiba ya fedha kwa muda mrefu, tafuta ajira nzuri na kadhalika zilinufaisha sana watu kwenye zama za viwanda, ila kwa sasa zimeshuka thamani.
   Badala ya kufanya kazi kwa nguvu, kwenye zama hizi unatakiwa ufanye kazi kwa maarifa na bidii, kwa sababu kinachomlipa mtu kwenye zama hizi sio nguvu zako bali ugunduzi wako ama utofauti wako unaoleta matokeo mazuri.
  Badala ya kuhifadhi fedha kwa muda mrefu, kwenye zama hizi inabidi uwekeze kwenye uwekezaji unaolipa ili fedha yako izalishe na ikupatie faida. Ukihifadhi fedha kwa muda mrefu thamani yake inashuka kutokana na mfumuko wa bei. Kama ulihifadhi milioni moja mwaka 2000 ukienda kuichukua leo utaweza kupata vitu ambavyo ungevipata mwaka 2000??
  Badala ya kutafuta ajira nzuri inabidi ufikirie kutengeneza ajira kwa sababu sote ni mashahidi waajiriwa wamekuwa wengi kuliko ajira zinazopatikana. Ajira zimeshuka thamani na waajiriwa hawanyenyekewi tena kama zamani walipokuwa wachache.
TAFUTA TARIFA USIACHWE NYUMA.