Katika watu zaidi ya bilioni saba duniani wewe pekee ndio uko ulivyo kwa tabia na kila kitu unachofanya na unachoweza kufanya. Hakuna mwenye uwezo wa kukufikia wewe kwa unayoweza kuyafanya, na wewe hakuna unayeweza kumfikia kwa anayoweza kuyafanya.

  Tatizo kubwa ni kwamba wengi hatufikii vile viwango vyetu. Kutofikia uwezo wako kunasababishwa sana na mazingira mtu unayoishi.

  Mara nyingi kuna vitu tunashindwa kuvifanya sio kwa sababu hatuna uwezo wa kuvifanya ila tu mazingira hayatupi nafasi ya kuvifanya. Ni vigumu sana kuwa muogeleaji mzuri kama utakuwa umezaliwa na kukulia eneo ambalo halina bahari, ziwa ama mto.

  Uzoefu pia una mchango mkubwa wa uwezo wa kufanya mambo fulani. Kuna mambo mengi ambayo huwezi kuyafanya sio kwa sababu huna akili ila tu ni kukosa uzoefu. Ina maana ukipewa nafasi ya kujifunza mambo hayo na kuyafanya kwa muda mrefu unaweza na wewe kuwa bora katika mambo hayo.

  Naandika haya kwa sababu kuna tabia ya watu kujiona ni wa chini ama hawana akili kwa sababu tu hawawezi kufanya mambo ambayo yanaonekana ni ya wenye akili.

  Kwa mfano mimi siwezi kufanya yafuatayo, kuendesha chombo chochote cha moto(ndege, gari, meli), kungea kichina, kiarabu, kihaya, kinyakyusa na lugha nyingine yoyote kuacha kiswahili, kiingereza na kichagga (nikiorodhesha nisiyoweza kuyafanya hapa itanichukua siku nzima), ila haimaanishi wanaoweza kufanya hivyo ambavyo siviwezi wana uwezo mkubwa kuliko mimi. Kama ningepewa mazingira waiyopewa wao bila shaka ningeweza kuyafanya hayo kama wanavyofanya wao. Kama ningezaliwa ama kukulia china basi haya maandishi yangekuwa kwa kichina.

  Usikatishwe tamaa na unaowaona wanaweza kuliko wewe, jua wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa na kama ukipata uzoefu unaweza kufanya vizuri zaidi. Kamwe usijishushe na kujiona wa chini.