Umewahi kusikia mtu mwenye muujiza kiasi kwamba akitaka kula samaki anakaa ndani anafanya miujiza yake samaki anatoka kwenye maji mpaka alipo mwenye muujiza? Hakuna kitu kama hicho. Kama unataka kula samaki inabidi uandae ndoano(ama kingine cha kuvulia), kwenda kwenye maji(mtoni, ziwani au baharini), kutega samaki, kusubiri mpaka ukamate samaki ndipo urudi ukale. Au badala ya kufanya hivyo inabidi ukafanye kazi nyingine upate fedha kisha ukanunue samaki ndio uweze kufurahia kitoweo hicho. Huwezi kuruka hatua yoyote kati ya hizo.

  Hakuna mtu yeyote anayeweza kukufanyia wewe muujiza, muujiza utaufanya mwenyewe kwa kuamua kufanya muujiza. Kila kitu kinaanza na wewe kufanya maamuzi ya kuyabadili maisha yako. Usikae ukidhani maisha yatakuwa rahisi, badala yake kuwa mgumu zaidi ya ugumu wa maisha. Amka nenda kafanye miujiza, dunia inakusubiri ukafanye mabadiliko.