Kama upo kwenye kundi la watu elfu moja na wote mnapiga kelele, labda mnamwita mtu, uwezekano wa sauti yako wewe kusikika na mnaemwita ni ndogo sana. Inabidi uwe na sauti ya juu, nguvu nyingi na uvumilivu wa kutosha. Sasa kama huna vyote hivyo ndio unakubali kushindwa? Hapana, usikubali kirahisi hivyo, kuna njia rahisi sana kwa sauti yako kusikika na mnaemuita kushinda wenzako. Njia hiyo ni kujitenga na kundi. Badala ya kukazana kupaza sauti katikati ya kundi ambapo sauti hiyo inaishia kumezwa na sauti za wengine, unaweza kujitenga na hilo kundi na kukaa pembeni kabisa na kutumia sauti yako ya kawaida kusikika.

  Kwenye maisha ya sasa kila unachotaka kufanya tayari kinafanywa na watu wengine wengi. Ukiingia kukifanya kama wao wanavyofanya utatumia nguvu nyingi na mwisho wa siku utachoka kwa sababu wao wameshafanya hivyo kwa muda mrefu. Hivyo njia rahisi ya kuweza kufanya kama hao wengi wanavyofanya ni kujitenga nao. Inabidi utafute kitu kitakachokutofautisha wewe na wenzako wanaofanya unachofanya wewe, ili uweze kuonekana kwenye hilo kundi. Hii inatumika kwenye maisha ya kawaida, kwenye ajira na kwenye biashara. Wengi hufikiri kujitofautisha kunahusika kwenye biashara tu ili kupata wateja, si kweli kujitofautisha kuna tumika sana hata kwenye ajira. Huwezi kufanya yanayofanywa na kila mtu halafu ukategemea kupandishwa cheo ama kuwa kiongozi. Wote wanaopewa uongozi wana vitu vya tofauti, vinavyowafanya waonekane kutoka kwenye kundi kubwa la wafanyakazi.

  Kwa kutumia mfano wa kujitofautisha na kundi unaweza kuona ni rahisi sana kujitofautisha, inaweza kuwa rahisi, lakini mbona watu wengi hawajitofautishi? Hilo ni swali ambalo inabidi ujiulize sasa hivi na upate majibu kwa nini mpaka sasa hujajitofautisha ama unajitofautisha vipi na kundi linalokuzunguka. Kujitofautisha kunahusisha sana ubunifu ambao kila mtu anao. Anza sasa kutumia ubunifu na kipaji chako kujitofautisha na kundi linalokuzunguka ili uweze kufikia mafanikio yako.