Rafiki yangu mpendwa,

Kama vitu viwili vinafanana kwa kila kitu, basi kimoja hakina umuhimu.

Hapa nazungumzia kwenye kila eneo la maisha yetu, kwenye kazi , biashara na hata maisha kwa ujumla.

Kwa mfano kama una uhitaji wa kitu fulani, na wapo watu wawili ambao wanatoa kitu hicho, lakini wanafanana kwa kila wanachofanya, huna namna ya kuwatofautisha au kuchagua yupi wa kwenda. Unachagua kwenda kwa yeyote tu.

Hii ina maana kwamba, kama mmoja akiondoka, hakuna kitu ambacho watu wanakosa, wala hawatashangaa kwamba ameondoka, kwa sababu alichokuwa anatoa, yupo mwingine anayetoa pia.

Kwenye maisha yako rafiki yangu, kwa chochote unachofanya, epuka sana kufanya kile ambacho kuna mwingine anaweza kufanya kama unavyofanya wewe. Kama huwezi kufanya kitu chochote kwa utofauti mkubwa na wengine wanavyofanya, basi unajiweka kwenye nafasi ya kutokuwa muhimu.

Tatizo kubwa

Njia pekee ya kutengeneza mafanikio kwenye maisha yako ni kuitengenezea umuhimu kwenye chochote unachofanya. Kama umeajiriwa basi hakikisha unakuwa muhimu sana kwenye ajira hiyo kuliko mwajiriwa mwingine yeyote. Kama unafanya biashara hakikisha unakuwa muhimu sana kwenye biashara hiyo kuliko mfanyabiashara mwingine yeyote. Hata kwenye mahusiano yako na wengine, hakikisha unakuwa muhimu sana kuliko wengine wote.

SOMA; KAMA UNATAKA KUFANIKIWA BASI USIFUATE KUNDI

Na ili kuweza kutengeneza umuhimu wako kwenye chochote unachofanya, unahitaji kutengeneza thamani kubwa, thamani ambayo hakuna mwingine anayeweza kuitoa. Unahitaji kuchagua kufanya kile ambacho hakuna mwingine anayeweza au yupo tayari kufanya.

Unahitaji kutoa thamani ambayo haiwezi kupatikana sehemu nyingine yoyote. Unahitaji kutatua tatizo lolote unalokutana nalo kwa namna ambayo mtu anajua hakuna njia bora zaidi ya kulitatua tatizo hilo zaidi ya ulivyofanya wewe.

Kwa chochote unachofanya, tengeneza uzoefu ambao watu hawawezi kuupata sehemu nyingine yoyote ila kwako, ambapo watu wanajua hakuna mbadala mwingine ila wewe.

Na hili linawezekana iwapo utakubali kuusikiliza moyo wako na kufanya kile ambacho unajua ni muhimu na cha kipekee kabisa.

Kitu kimoja nilichojifunza kupitia wengi ni kwamba kila mtu anajua njia bora kabisa ya kufanya kile anachofanya. Kila mtu ana wazo la namna gani anaweza kufanya kwa ubora zaidi. Lakini ni wachache sana ambao wapo tayari kuweka kazi kufanya kile ambacho ni tofauti, kwa sababu siyo rahisi kufanya.

Siyo rahisi kabisa kufanya chochote unachochagua kufanya kwa utofauti wa hali ya juu. Kwa sababu wanaokuzunguka wanategemea ufanye kama wao wanavyofanya. Utakapoanza kufanya kwa utofauti, watakuona wewe ni mtu hatari kwao na kuanza kukurudisha nyuma, kwa kukukatisha tamaa na kukukosoa.

Lazima ujitoe sana kama kweli unataka kutengeneza utofauti, lazima uwe kiziwi usiyesikia wala kuelewa yale watu wanasema hayawezekani. Na lazima uchague kujisikiliza wewe mwenyewe kwanza kabla hujamsikiliza mwingine yeyote na uchague kufanya maamuzi na kusimamia maamuzi yako kwa namna yoyote ile mpaka uyafikie.

Usikubaki kabisa kuwa sawa na wengine, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kama mteja wako anakulinganisha na wengine na kusema hakuna tofauti, jua kabisa huna biashara na chochote unachofanya, huna muda mrefu wa kuendelea kufanya na hutaweza kufanikiwa.

Weka utofauti mkubwa kwenye chochote unachofanya, weka thamani kubwa sana, hata kama watu wanakulipa kidogo, usiangalie unacholipwa, angalia unachotoa. Kwa sababu unacholipwa huenda hakuna mwingine anayejua ila wewe, lakini kile unachotoa kila mtu atakiona na atakuhukumu kwa unachotoa, siyo unacholipwa.

Na kama unalipwa kidogo, ni kiashiria kwamba thamani unayotoa pia ni ndogo. Anza kutoa thamani kubwa na kiasi unacholipwa kitaongezeka. Kwa sababu ukiwa na upekee ambao hauwezi kupatikana popote, basi thamani yako inakuwa juu pia.

Angalia kazi mbili, kazi moja ni ya kufagia barabara ambapo mtu amefanya kazi hii kwa muda mrefu na ana uzoefu wa kutosha. Kazi nyingine ni upasuaji wa ubongo, ambapo kuna mtu kahitimu siyo muda mrefu. Je unafikiri katika watu hao wawili nani atalipwa sana? Bila shaka ni yule anayefanya upasuaji wa ubongo. Na hii ni kwa sababu ukiweka muda pembeni, ni mtu gani rahisi kupata pale unapohitaji watu zaidi, mfagiaji wa barabara au mpasuaji wa ubongo?

Ninachotaka kukuambia hapo rafiki yangu ni hichi, kadiri kile unachofanya kinavyokuwa rahisi kupatikana na kufanyika na wengine pia, ndivyo pia utakavyolipwa kiasi kidogo cha fedha. Na pale unapotoa kitu ambacho ni kigumu kupatikana, kitu ambacho hakuna wengine wanaoweza kufanya, wewe ndiyo unachagua ulipwe kiasi gani. Kwa sababu asiyetaka kulipa, ana machaguo gani mengine? Ana wapi pengine pa kupata kile anachotaka?

SOMA; HII HAPA NDIO BIASHARA INAYOLIPA

Nimalize kwa kukusihi hili rafiki yangu, chochote unachoruhusu mikono yako ishike, basi acha alama. Kifanye kwa namna ambayo hakuna mwingine anayeweza kufanya. Mfanye anayekutana na kazi yako aseme hii amefanya fulani hata kama haupo au hajaambiwa nani kafanya.

Na yote haya yanawezekana pale unapoamua kuweka thamani kubwa kabisa kwenye kile unachofanya. Unapochagua kwenda hatua ya ziada, unapochagua kufanya tofauti na wengine wanavyofanya na unapochagua kujisikiliza na kufanya kile ambacho wewe unajua ni muhimu na tofauti.

Leo pata muda wa kutafakari na kupima kila unachofanya, angalia matokeo unayotoa na kama yanapatikana kwa wengine, kama hakuna kinachokutofautisha wewe na wengine wanaofanya unachofanya, basi jua uwepo wako hauna umuhimu na unaweza kupotezwa wakati wowote. Chagua ni utofauti gani upo tayari kuutengeneza, chagua ni kwa namna gani unataka wengine wakuzungumzie na chakua kuanza kuchukua hatua mara moja ili kutengeneza thamani hiyo ya tofauti na kutengeneza umuhimu wako kwa wengine.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha