Kwenye siku yako kuna mambo mengi sana yanayotokea. Kwanzia unapoamka mpaka unaporudi kulala kuna mlolongo mkubwa wa matukio, mengine ulipanga mengine yamejitokeza yenyewe. Siku hazifanani na hata uipange siku yako kwa kiasi gani bado kuna baadhi ya vitu ambavyo hukupanga ama hukudhani vinaweza kutokea, ila vinatokea.

  Kwa kuwa siku imeisha ni vyema kuitafakari siku nzima kwa undani na kujipanga kwa ajili ya kesho. Jipongeze kwa yale uliyofanikiwa kukamilisha na jifunze kwa yale uliyoshindwa na yale yaliyojitokeza wakati hukuyapangilia. Usitumie muda mwingi kujilaumu kwa makosa uliyofanya, bali jifunze kutoka kwenye makosa yako. Jua kwa nini yametokea na ungefanya nini kuyazuia.

  Usisahau kuipanga siku ya kesho kabla hujalala. Pia weka nafasi ya kufanya yale yanayoweza kujitokeza ambayo hukuweka kwenye mpango wako.