Kuna uhusiano wa karibu sana baina ya sisi viumbe hai, wote tunazaliwa, tunakua, tunazaa, tunakula, tunatoa taka mwili na pia viumbe hai wote tunakufa. Tabia zote hizo zipo kwenye minyoo, mimea mpaka sisi binadamu. Pia kuna viumbe ambao tuna uhusiano wa karibu zaidi kwa mfano wanyama wote waliopo kwenye kundi la mamalia tuna tabia nyingi tunazofanana. Sisi binadamu na mbuzi wote tuko kwenye kundi la mamalia na tofauti yetu kubwa na viumbe wengine wadogo kama mijusi ni kwamba sisi(binadamu na mbuzi) tuna tabia zilizowazidi wako ambazo ni, tunazaa, kunyonyesha na pia kutunza watoto wadogo, na tuna ubongo ulioendelea zaidi. Samahani kama ulikuwa hulipendi somo la baiolojia, hata hivyo sio kwamba nakurudisha darasani ila tunakumbushana tu. Sasa twende kwenye hoja ya msingi, kila kiungo tulichonacho hata mbuzi anacho, kila kinachofanyika mwilini mwetu hata kwa mbuzi kinafanyika, tofauti kuu kati yetu na mbuzi ni uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi.

  Binadamu ubongo wetu una uwezo wa kufikiri, kugundua na kufanya maamuzi kutokana na mazingira tuliyopo. Tunaweza kugundua vitu vikubwa sana ambavyo wanyama wengine wote hawawezi kugundua, kama tukiweza kutumia uwezo wetu wa kufikiri. Sijawahi kusikia mbuzi kagundua kitu fulani, wewe umewahi kusikia? Ukimweka mbuzi mahali anakoweza kupata chakula na akapumzika basi habari yake imekwisha, hana la ziada. Mbuzi anafata kile anachokijua tu, hana muda wa kufikiria njia mbadala. Kwa mfano kukiwa na msafara wa mbuzi wengi halafu ukafunga kamba njiani wale mbuzi wa mwanzo watakaposhindwa kupita wataruka, na wanaofuatia nao wataruka, cha kushangaza utakapoiondoa kamba bado mbuzi wote waliobaki wakifika pale wataruka, na kamba hakuna.

  Naandika haya sio kwa sababu nataka kukusimulia hadithi ya maisha ya mbuzi ila kukufanya utafakari maisha yako yana tofauti gani na ya mbuzi. Na naomba unielewe vizuri sina lengo lolote la kukukashifu hapa ama kukufananisha na mbuzi, kuna ukweli unatakiwa kuujua na inabidi uujue hata kama ni mchungu.

Kama unafanya mambo yaleyale kila siku na hujisumbui kuja na njia mpya, huwazi wala hutumii ubunifu wako basi huna tofauti na mbuzi.

  Kama huwezi kuzidhibiti hisia zako za kutaka KUFANYA MAPENZI basi huna tofauti na mbuzi. Mbuzi akijisikia tu kufanya mapenzi anafanya ila kwa wewe binadamu una uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya maamuzi, hivyo inapofikia mtu anabaka basi hawezi kumcheka mbuzi.

  Akili yako ina uwezo mkubwa sana usiokuwa na kikomo. Tumia uwezo huo kufikiri na kupata njia mbadala za kutatua matatizo yako na kufikia malengo yako. Kwa lolote unalofanya ama unalotaka kufanya jiulize JE MBUZI ANAWEZA KUFANYA VIZURI ZAIDI YA NINAVYOFANYA?