Tofauti kubwa kati ya binadamu na viumbe wengine ni uwezo mkubwa tuliopewa binadamu wa kuweza kubadili mazingira yanayotuzunguka. Binadamu tunauwezo mkubwa wa kugundua vitu vya aina mbalimbali. Pamoja na kuwa na uwezo huo mkubwa wa kugundua mambo bado sio wote wanaogundua vitu vipya. Kuna tofauti gani kati ya wagunduzi na watu wengine?

  Kabla ya kitu chochote kugunduliwa ni lazima mgunduzi aone matokeo ya kitu anachotaka kufanya kabla hata hajaanza kukifanya. Ni lazima mgunduzi aone picha kamili ya matokeo ya kile anachofanya. Picha hiyo ndio inampa nguvu na hamu kubwa ya kufanya ili kufikia picha hiyo. Kuweza kuiona picha isiyokuwepo ndio tofauti kubwa ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa ama wagunduzi na watu wengine.

                              ndoto

  Picha hiyo inapatikana vipi? Picha hiyo inapatikana kwa kuwa na ndoto. Ndoto tunayozungumzia hapa sio ya kulala na kuota usiku, hapana, hii ni hali ya kuona mbele na kuwa na kiu ya kufanya jambo ili kufikia kule unakoona. Ndoto ndiyo inayotengeneza picha kubwa ya mambo yatakavyobadilika kwa wewe kufanya kile unachohitajika kufanya.

  Bila ya kuwa na ndoto ni vigumu sana kufanya mabadiliko kwenye maisha yako na maisha ya wanaokuzunguka. Ndoto ndiyo inayokufanya kutengeneza malengo ya maisha yako na mipango ya kuitekeleza.

  Kwa nini wengi hawaleti mabadiliko? Watu wengi wanapita duniani bila ya kuleta mabadiliko yoyote hata kwa wao binafsi kwa sababu wanaamua kutokuwa na ndoto. Japokuwa hakuna gharama yoyote kuwa na ndoto lakini wengi hawataki tu kuota. Wewe ndoto yako ni nini?

  Huwezi kufanikiwa maishani kwa kufanya tu kila linalokuja mbele yako, lazima uwe na ndoto kisha uweke malengo na mipango ya kufikia ndoto hiyo. Lazima ujue unakokwenda ili ujue jinsi ya kufika huko.

  Ota ndoto yako na iwe ndoto kubwa ambayo kila siku inakupa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii ili uweze kuifikia.