Kama unataka kula ng’ombe unafanya nini? Unamchukua ngombe mzima mzima nakumweka kwenye sufuria kubwa, ukamchemsha kisha kumla? Hapana, hata mwendawazimu hawezi kufikiri ama kufanya hivyo.

  Sote tunajua ukitaka kumla ng’ombe kwanza unamchinja, unamkata vipande vidogo vya nyama, kisha unapika na kula nyama ya ng’ombe. Rahisi kama hivyo. Ila ukikaa na kuanza kufikiria jinsi ya kuweza kumla ng’ombe mzima mzima bila kumkata vipande ni dhahiri utakata tamaa ya kula nyama.

  Mfano huo wa ng’ombe ni muhimu sana kuutumia kwenye maisha ya kawaida. Kwa jukumu, ndoto ama tatizo lolote linalkukabili ni rahisi sana kama utafikiria kwa mfano huo.

unassembed

  Kama una ndoto ama malengo makubwa sana ambayo unahisi huwezi kuyafikia ama yanakuogopesha ni vyema ukagawa kwenye vipande vidogo ambavyo ni rahisi kwako kukamilisha. Ukitaka kufikia malengo yako kwa wakati mmoja utaishia kukata tamaa kwa kuwa ni vigumu kufanya hivyo. Kama tulivyoona kwenye malengo ya fedha, kujaribu kupata milioni ishirini kwa mwaka ni jambo linaloweza kukuumiza kichwa sana, ila kupata shilingi elfu kumi kwa saa ni rahisi zaidi. Jambo lolote linakuwa rahisi sana ukishaigawa kwenye vipande vidogo.

  Kama una kazi kubwa ambayo inakuumiza jinsi ya kuimaliza, usiangalie sana kuimaliza kwa pamoja bali igawe kazi hiyo kwenye majukumu madogo madogo na kuyakamilisha mwisho unajikuta umeshamaliza kazi yote na ukiwa na furaha. Kuwaza jinsi ya kuimaiza kazi yote kwa pamoja ni kitu ambacho kitakuletea msongo wa mawazo.

  Hali kadhalika unapokutana na tatizo lolote usiumizwe na ukubwa wa tatizo. Angalia jinsi unavyoweza kuligawa tatizo hilo kwenye sehemu ndogo ndogo na kisha kuanza kutatua sehemu hizo. Mwisho wa siku tatizo linakuwa limekwisha na wewe hujaumia sana.

  Kwa lolote unalokutana nao kwenye maisha kumbuka kugawa kwenye sehemu ndogo ndogo. Kama mtu anaweza kumla tembo kwa kumchinja hakuna kinachoshindikana kama kikigawanywa kwenye sehemu ndogo ndogo.