Kwa mfumo wa elimu wa Tanzania, mtu anaesoma mpaka ngazi ya shahada(degree) anakuwa ametumia sio chini ya miaka 17 kwenye elimu. Na wengi wanatumia mpaka miaka 20 kwenye elimu.

elimu bora

  Kwa mfano kwa mtanzania wa kawaida anatumi miaka ifuatayo kwenye elimu;

shule ya awali miaka 2

shule ya msingi miaka 7

shule ya sekondari miaka 6

chuo kikuu miaka 3 – 5.

  Kama mtu alirudia mitihani kwa kufeli ama alipitia ngazi za cheti na stashahada(diploma) miaka inazidi kuwa mingi(zaidi ya 20).

  Na kama mtu atataka kuendelea kupata shahada nyingine za uzamivu na uzamili(masters na Phd) miaka inazidi kuongezeka.

  Ukiangalia kwa makini kwa miaka yote hii (miaka 15-25) tuliyokaa kwenye elimu elimu bora tuliyoipata ni kujua kusoma na kuandika, basi.

  Mambo mengi tunayoyafanya kwenye maisha bada ya elimu yana uhusiano mdogo sana na tuliyokuwa tunafundishwa shuleni. Ila chochote unachofanya kwenye maisha ni lazima kitahusisha kusoma na kundika.

  Unaweza kufanya chochote unachotaka kwa kujua tu kusoma na kuandika. Na kwa ulimwengu wa sasa ni kujua kusoma na kuandika lugha ya kiingereza.

  Hizi ni zama za taarifa na taarifa zinapatikana kwa urahisi sana kuliko kipindi chochote(soma; zama za taarifa). Hakuna kinachoshindikana kwa kujua kusoma na kundika.

  Mtandao wa internet umejaa taarifa nyingi sana, vitabu vingi mno vimeandikwa kwa kila kada, na kama bado hiyo haitoshi vitendo vingi vimerekodiwa na kuwekwa kwenye mtandao kama video, na pia vitabu vimesomwa na kurekodiwa hivyo kurahisisha usomaji kwa kusikiliza(soma; audio books).

  Kwa kuwa na utaratibu wa kujisomea kwa chochote kile unachofanya unajiongezea ujuzi mkubwa na unaweza kufanya mengi zaidi na kwa ubunifu zaidi(soma; zoezi zuri la kufanya kila siku). Vitabu vimejaa busara na ujuzi mwingi ambapo yeyote anaetaka kuupata anaweza kuupata kwa urahisi sana.

elimu bora2

  Mtandao wa internet kwa sasa una kila kitu kinachofanyika ama kinachohitajika kufanyika. Kama unataka kujifunza chochote ukiingia tu kwenye mtandao wa Google na kukitafuta unapata maelezo mengi ya jinsi ya kukifanya. Na ukiingia kwenye mtandao wa YouTube unakuta video zenye njia za kufanya kile unachotaka kufanya.

  Japokuwa mfumo wa elimu ni mbovu, kitu kizuri tulichojifunza kwenye elimu ni kujua kusoma na kuandika. Kama ukijielewa kwa kujua hivyo tu tayari upo kwenye njia nzuri ya kufika kule unakotaka kufika hata kama huna degree, masters ama PhD.

Kujua kusoma na kuandika ndio elimu bora uliyoipata kwenye maisha yako ya elimu.