Kuna usemi maarufu sana tunaopenda kuutumia. Usemi huo unasema “mwenye nacho huongezewa”. Usemi huu una ukweli kwa asilimia mia moja. Ila tunapoutumia tunashindwa kuelewa kwamba kuna kitu tunakosea.

  Tumekuwa tukitumia usemi huu wa mwenye nacho huongezewa tunapowaangalia watu waliofanikiwa. Mara nyingi watu wanatumia usemi huu kwa watu wenye fedha na kuona kwamba kwa kuwa wao wana fedha hivyo wanaendelea kupata zaidi. Na ni kweli inatokea hivyo.

  Usemi huu wa mwenye nacho huongezewa unatumika kwenye kila nyanja ya maisha. Tatizo kubwa wengi wetu hatujui kama tunacho ama hatujui tulichonacho. Wale wanaobahatika kujua wanacho na kujua walichonacho wamejikuta wakipata zaidi na zaidi. Wale ambao hawajui walichonacho wameishia kuamini kwamba wao hawapati zaidi kwa sababu hawana.

  Ni mara ngapi umemwangalia mtu unayeona amefanikiwa kuliko wewe na kutoa kauli hizi zinazoanza na kama….

kama ningekuwa na bahati kama yeye……

kama ningekuwa na elimu aliyopata yeye….

kama ningekuwa na kazi ama cheo alichonacho yeye….

kama ningekuwa na akili kama yeye……

kama ningepata nafasi aliyoipata yeye…..

kama ningekuwa nimetoka kwenye familia yenye uwezo kama yeye…..

kama, kama, kama…….

  Hizi kama umeshazitoa mara nyingi na katika nyakati tofauti tofauti ukijiaminisha kwamba kilichofanya mtu afanikiwe na wewe ushindwe ni kwa sababu kuna vitu fulani amepewa na wewe huna.

pekee

  Ni kweli kabisa kuna vitu wenzako wamepewa ila wewe huna ila ukweli mchungu zaidi ni KUNA VITU UMEPEWA WEWE NA WENZAKO HAWANA.

  Unaona wao wamefanikiwa kwa sababu wamejua vile walivyopewa na wamejua jinsi ya kuvitumia. Na wewe hujafanikiwa kwa sababu huenda hujui kile cha pekee ulichonacho ama unakijua ila hujaweza kukitumia ili kupata mafanikio.(soma; hizi ndizo fursa unazozipita kila siku)

  Unaposema yeye kafanikiwa kwa sababu fulani ambayo wewe huna ni sawa na kujitukana wewe binafsi na kujiona wa chini sana.

  Kumbuka wewe ni wa pekee na una vipaji na uwezo mkubwa sana ambao hauwezi kulinganishwa na binadamu mwingine yeyote duniani.(soma; wewe ni wa pekee). Tambua vipaji na uwezo mkubwa ulio ndani yako na ujue jinsi unavyoweza kuvitumia kufikia mafanikio.

  Unapojua kipaji cha kipekee ulichonacho na kuanza kukitumia utajikuta unajua zaidi na zaidi. Kwa kujua zaidi unajikuta unafanya kwa utofauti na hii ndio inayokuletea mafanikio.

  Mwenye nacho huongezewa, na wewe pia unacho. Ili uanze kuongezewa ulichonacho ni lazima kwanza ujue unacho na pia ukijue ulichonacho.